





Na Mwandishi Wetu
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Mhe. Mohamed Mchengerwa amesema kuwa kazi ya kuleta maendeleo aliyofanya wilayani Rufiji ni sehemu ya ibada, siyo siasa.
Alisema hakujielekeza katika mlengo wa kisiasa, kwa kuwa anaamini kuwa kuwaletea wananchi maendeleo ni jambo linalompendeza Mwenyezi Mungu na ni tendo la kizalendo.
Mchengerwa aliyasema hayo Ikwiriri wakati wa kutoa salamu za shukrani kwa Mufti wa Tanzania, Shekhr Aboubakar Bin Zuberi, na wananchi walioudhuria hitma ya Alhaj Omary Rashid Mchengerwa, aliyefariki dunia Februari 24, 2025, mjini Medina, Saudi Arabia.
Amesisitiza kuwa kazi ya kuleta maendeleo imefanyika kama sehemu ya kutekeleza maelekezo ya Mufti wa Tanzania, aliyewataka viongozi kujitoa kwa dhati katika kuwatumikia wananchi.
“Tumefanya kazi kuhakikisha vijiji vyote 38 vina umeme. Tumeongeza shule za sekondari kutoka 4 hadi 27, shule za kidato cha tano na sita kutoka 1 hadi 7, shule za msingi kutoka 23 hadi 67, vituo vya afya kutoka 3 hadi 9. Tumekarabati Hospitali ya Wilaya ya Utete na kujenga barabara za lami zaidi ya kilomita 20,” amesisitiza Mhe. Mchengerwa.
Kwa mafanikio hayo, Mhe. Mchengerwa amesema ni kwa neema ya Mwenyezi Mungu ambaye amewajalia wananchi wa Rufiji kumpata Rais, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ambaye amesikiliza kero na changamoto za wananchi hao na kuhakikisha zinatatuliwa kwa kupeleka fedha za ujenzi wa miundombinu ya umeme, elimu, afya, na barabara.