Wakulima wa mpunga wilayani Same mkoani Kilimanjaro, wameeleza kushangazwa na uamuzi wa Serikali kuruhusu uagizaji wa mchele kutoka nje ya nchi, wakati wao wamekosa wanunuzi wa tani 15,000 za bidhaa hiyo hapa nchini.

Wametaja tatizo la ukosefu wa soko la mchele wilayani humo msimu huu, kama chanzo cha wao kuyumba kiuchumi kiasi cha kushindwa kumudu mahitaji ya kifamilia kama vile kugharamia masomo ya watoto wao.


Wakizungumza na JAMHURI hivi karibuni, wakulima hao wamedokeza kuwa waliokuwa wanunuzi wakuu wa mchele wilayani humo, kwa sasa wamegeukia kununua unaoagizwa kutoka nchi za India, China na Thailand.


Mhina Joseph, mkulima wa mpunga katika Kata ya Ndungu wilayani Same, amesema wanunuzi wa mchele wilayani humo wamekuwa wakitoka zaidi katika mikoa ya Arusha, Tanga, Dar es Salaam na Morogoro. Mkulima huyo amehoji sababu ya Serikali kuruhusu uagizaji wa mchele kutoka nje ya nchi, huku akisema, “Mpaka sasa tumehifadhi zaidi ya tani 15,000 za mchele maghalani, wanunuzi hawaonekani, tumekosa fedha za kuwapeleka watoto shule. Mimi binafsi nina tani tatu za mchele, sijapata wanunuzi.”


Mwingine aliyejitambulisha kwa jina la Juma Ibrahim, amesema hali ya wakulima wa mpunga wilayani humo inazidi kuwa mbaya, baada ya kukosa soko la mavuno yao, kwani wote hutegemea kilimo hicho kujipatia fedha za kujikimu na familia zao.


“Mimi pekee nimeshavuna tani tatu na nusu za mchele, na bado ninaendea kuvuna, hali huku ni mbaya sana. Tumelima mpunga mwingi lakini hakuna anayekuja hata kuuliza bei.


“Tumeshangaa kusikia Waziri Mkuu [Mizengo Pinda] anasema Serikali imeruhusu wafanyabiashara kuagiza mchele kutoka nje ya nchi wakati huku [wilayani Same] tuna mchele mwingi uliokosa wanunuzi,” amesema Ibrahim.


Kwa upande wake, Yohana Ali amesema kukosekana kwa wanunuzi wa mchele uliovunwa, kunawapa wasiwasi kuwa wataishia kupata hasara kwa kushindwa kurudisha fedha nyingi walizotumia kugharamia kilimo hicho.


“Tumelima mpunga kwa gharama kubwa, Mungu ametujaalia tumepata mavuno mengi tu lakini tumekosa matajiri [wanunuzi]. Tunaomba Serikali ituletee wanunuzi,” amesema Ali.


Naye Mbarugu Hamis amesema matarajio yake ya kuuza zaidi ya tani tano za mchele uliotokana na mavuno ya msimu huu, yanazidi kufifia kwani hadi sasa hajapata mteja wa kuununua.


Omari Mganga ni Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji cha Msufini katika Kata ya Ndungu.

Naye amekiri kuwa mavuno ya mpunga ni mengi katika eneo hilo lakini yamekosa soko.


“Hapa watu wamevuna sana mpunga lakini hakuna wanunuzi wa mchele, wakulima wameshindwa kumudu gharama za mahitaji yao ya kifamilia. Wanunuzi hawapatikani hata kwa bei ya Sh 1,000 kwa kila kilo ya mchele,” amesema Mganga na kuongeza: “Tunaomba Serikali itusaidie kuleta wateja huku wanunue mchele hata kwa bei ya Sh 1,000 kwa kilo moja. Tumesikia mkoani Mwanza mchele unauzwa Sh 1,600 kwa kilo moja. Sisi huku tumechanganyikiwa, mchele umekosa wanunuzi.”

 

Alipotakiwa na JAMHURI kuzungumzia suala hilo, Mkuu wa Wilaya ya Same, Herman Kapufi, amekiri kuwa kwa sasa mchele unapatikana kwa wingi wilayani humo ila umekosa soko.


“Ni kweli wakulima wamekosa soko, bei si kubwa ikilinganishwa na gharama ya uzalishaji. Kwa sasa gunia lenye mchele [kilo 100] linauzwa kati ya Sh 45,000 na Sh 55,000, kiasi ambacho hakirudishi gharama ya uzalishaji,” amesema.


Kwa upande mwingine, Kapufi ameeleza kuwa bei ya mchele imeshuka msimu huu kutokana na mazoea ya wakulima kukoboa mpunga kienyeji badala ya kutumia mashine maalumu kwa shughuli hiyo.


“Kwa kawaida bei ya mchele huwa inashuka kila msimu wa mavuno, lakini pia kitendo cha wakulima wengi kuchambua mpunga kienyeji badala ya kutumia mashine husika, kimechangia kushuka kwa bei na hata kukosa wateja,” amesema.


Hata hivyo, kiongozi huyo ameahidi kuwasiliana na uongozi wa kitengo cha kilimo wilayani humo, kuangalia namna ya kuwasaidia wakulima hao kupata soko la mchele waweze kujikwamua kiuchumi.