Kama tujuavyo Bunge la Mabadiliko ya Katiba limekumbwa na vurugu na misukosuko kiasi cha kutia aibu Taifa letu.
Nashindwa kusema Bunge hilo liliendelea kujadili Rasimu ya Katiba kwa ukaidi wa nani. Maana wakati wote magenge mbalimbali ya watu waliendelea kudai Bunge hilo lisitishe shughuli zake, hasa baada ya wabunge wanaounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) kususia Bunge hilo.
Japokuwa si rahisi kutaja mambo yote yaliyosababisha Bunge la Katiba kukumbwa na vurugu na misukosuko, jambo moja ni wazi. Mchakato wa Katiba haukuandaliwa vizuri au kwa umakini.
Hapa hatuna sababu hata ndogo ya kutilia shaka lengo la Rais Jakaya Kikwete la kuanzisha mchakato wa katiba. Rais Kikwete alianzisha mchakato wa mabadiliko ya Katiba kwa lengo zuri kabisa la kuwaachia Watanzania Katiba bora ambayo wangeikubali wananchi walio wengi. Maana hakuna kitu kinachokubalika na watu wote.
Lakini kama yalivyo mambo mengine nchini kwetu Tanzania, malengo yetu ni mazuri wakati wote lakini utekelezaji ni mbovu wakati wote pia. Kwa kifupi waliopanga ratiba ya utekelezaji wa mchakato wa Katiba hawakuwa makini, hawakufanya kazi nzuri.
Kwa hiyo, Rais Kikwete hataweza kutuachia Katiba mpya kama alivyokusudia. Katiba, kama mwongozo wa utawala, ni kitu muhimu sana. Ni sheria mama au sheria kuu ya nchi.
Lakini haikushughulikiwa kwa umakini ili nchi iwe na utawala bora.
Kwanza kabisa idadi ya watu waliounda Bunge la Katiba ilizidi watu 600. Idadi hii ni kubwa mno kwa mambo mawili. Kwanza, idadi kubwa mno ya wajumbe wa Bunge la Katiba ilisababisha wajumbe wengine kutochangia mawazo yao juma zima. Kwa kuwa hawakuwa na jambo la kufanya walimaliza juma zima wakizomea. Wasingeweza kukaa kimya juma zima.
Pili, wajumbe wa Bunge la Katiba waliokaa kimya wakati wote waliendelea kupokea posho ya shilingi 300,000 kwa siku. Kwa hiyo, tuliendelea kuwalipa mshahara watu ambao hawakuwa wafanyakazi. Juu ya yote, idadi kubwa mno ya wajumbe wa Bunge la Katiba ilisababisha wajumbe wengine kuwa watoro.
Halafu aina ya wajumbe walioteuliwa kuingia kwenye Bunge la Katiba pia ilibidi iangaliwe kwa umakini. Walijaa wanasiasa zaidi kuliko wataalamu. Ni kweli hii si mara ya kwanza kwa nchi yetu Bunge kujadili Katiba ya nchi. Mwaka 1962 Bunge la Tanganyika lilijadili na kupitisha sheria iliyofanya Tanganyika kuwa Jamhuri yaani nchi inayoongozwa na rais. Tanganyika ikawa Jamhuri Desemba 9, 1962, Rais wake akiwa Mwalimu Julius Nyerere.
Mwaka 1965 Bunge la Tanzania lilijadili na kupitisha sheria iliyofanya Tanzania nchi ya chama kimoja. Tanzania ikaanza kufuata rasmi mfumo wa chama kimoja Julai 1,1965. Mwaka 1992 Bunge la Tanzania lilijadili na kupitisha sheria iliyorejeshea nchi mfumo wa vyama vingi. Tanzania ikawa rasmi nchi ya mfumo wa vyama vingi kuanzia Julai 1,1992.
Ni vyema tukazingatia kwamba nyakati zote hizo mijadala ndani ya mabunge ya Katiba iliendeshwa kwa utulivu. Sababu yake moja kubwa ni kwamba Tanzania ilikuwa nchi ya chama kimoja. Kwa hiyo, walikuwa wamoja lakini kulikuwa na kasoro zake.
Kasoro moja kubwa ya Katiba hizo zilizopitishwa wakati wa mfumo wa chama kimoja ni kwamba wajumbe wa Bunge la Katiba wote walikuwa wa chama kimoja. Walitumia fursa hiyo kupitisha mambo ya kujipendelea na ya kulinda maslahi ya chama chao.
Chukua, kwa mfano, Katiba ya Kudumu ya mwaka 1977 tunavyotaka kubadilisha ambayo ilifanyiwa marekebisho mwaka 1992 ili kuruhusu mfumo wa vyama vingi.
Kwanza sheria ya vyama vingi ilivyotungwa mwaka 1992 ilizua watu binafsi kugombea udiwani, ubunge na urais. Pili, sheria hiyo ilikataza Tume ya Uchaguzi kuhojiwa na kufikishwa mahakamani. Tatu sheria hiyo pia ilikataza ushindi wa Rais kuhojiwa mahakamani. Kwa hiyo, nchi ya Bunge la chama kimoja mambo yalipita kiulaini kabisa.
Leo mambo ni tofauti, katikati ya mfumo wa vyama vingi hakuna Bunge linaloweza kupitisha sheria yoyote kiulaini. Ni muhimu kuzingatia pia kwamba Bunge la vyama vingi wabunge wanatawaliwa zaidi na ushabiki wa kisiasa kuliko maslahi ya Taifa.
Kwa hiyo, Bunge la Katiba lilipoanza Februari 18 mwaka huu, ilitokea misuguano iliyotokana na ushabiki wa kisiasa. Lakini baada ya watu wa UKAWA kususia Bunge hilo wakidai kuwa walikuwa wanatetea katiba ya wananchi, wabunge wa chama tawala walitumia nafasi hiyo kupitisha mambo ya kujipendelea na kujiandalia mazingira ya kuendelea kuwa wabunge bila kubughudhiwa.
Kwa hiyo, walifuta kipengele katika Rasimu ya Katiba kilichotaka wapiga kura wamwajibishe mbunge asiyefaa wakati wowote hata kabla ya uchaguzi. Wametaka pia ubunge usiwe na kikomo baada ya Rasimu ya Katiba kutaka mtu aliyewahi kuwa mbunge kwa vipindi vitatu vya miaka mitano mitano asigombee tena ubunge.
Wajumbe wa chama tawala wanataka ubunge uwe ajira yao ya maisha, wanataka wafe na ubunge! Basi ili kupata Katiba bora isiyopendelea chama chochote cha siasa, ilitakiwa Katiba ijadiliwe na kupitishwa na wataalamu ambao si wanasiasa na ambao si mashabiki wa vyama vya siasa moja kwa moja.
Ilitakiwa wajumbe wa Bunge wawe mawakili wa Serikali na mawakili wa kujitegemea. Hao wangeweza kutuletea Katiba bora isiyotegemea upande wowote. Wala tusingehitaji kupata kura ya maoni.
Kasoro nyingine iliyojitokeza katika mchakato wa Katiba ya Tanzania ni ratiba ya mchakato huo kukosa kutoa nafasi kwa wajumbe wa Katiba kufanyiwa semina nzuri elekezi. Chukua, kwa mfano, ukurasa wa kwanza kabisa wa Rasimu ya Katiba kuna taarifa iliyotolewa na Rais Jakaya Mrisho Kikwete, Januari 22, 2014. Taarifa hiyo inasomeka ifuatavyo:-
Toleo hili la Rasimu ya Katiba (la pili) linachapishwa kwenye Gazeti la Serikali kwa mujibu wa kifungu cha 20 (2) cha Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, sura ya 83, na itawasilishwa kwenye Bunge Maalum la Katiba, kwa ajili ya KUJADILIWA NA KUPITISHWA.”
Kama wajumbe wa Bunge la Katiba wangeelimishwa vya kutosha kwamba Bunge lilikuwa ilimeitwa ili kujadili na kupitisha Rasimu ya Katiba, huenda watu wa UKAWA wasingesusia Bunge kwa madai kwamba walikuwa wanatetea katiba ya wananchi. Walishindwa kuelewa mambo mawili.
Kwanza, kwamba Bunge halikuitwa kwa lengo la kupitisha kila kitu moja kwa moja bila kujadiliwa. Shughuli ya kwanza ya Bunge ilikuwa kujadili. Na katika kujadili kwa uadilifu mkubwa kwa maslahi ya Taifa hakukosekani kukuta maeneo ya kuongeza au kurekebisha kabla ya kupitishwa kuwa sheria.
Kwa maana hiyo kama wajumbe wa UKAWA na Jaji mstaafu Joseph Warioba wangezingatia kuwa Bunge halikuitishwa kwa lengo la kupitisha moja kwa moja maoni ya wananchi bila kujadiliwa, wasingelalamikia kuongezwa au kurekebishwa maeneo mbalimbali ya katiba.
Pia wangejua kuwa halikuwa jukumu la Bunge kutoa Katiba ya wananchi moja kwa moja. Katiba ya wananchi ingepatikana baada ya wananchi kupiga kura ya maoni.
Huko nyuma nimedokeza kwamba Rasimu ya Katiba ilipaswa kujadiliwa kwa uadilifu mkubwa na kwa maslahi ya Taifa, ukweli ni kwamba baada ya wajumbe wa UKAWA kususia Bunge la Katiba wajumbe wa chama tawala hawakujadili Rasimu ya Katiba kwa uadilifu mkubwa na kwa maslahi ya Taifa.
Kuna uadilifu gani mnapotaka msiwajibishwe na wapiga kura na mnapojiongezea miaka saba ya kuendelea na ubunge? Na tangu lini kujipendelea kumekuwa sehemu ya uwadilifu?
Halafu tuangalie suala la kura ya maoni. Wenzetu hawawezi kuitisha kura ya maoni na mambo ambayo ni mchanganyiko wa mambo mengi, wanaitisha kura ya maoni ya kukubali au kukataa jambo moja.
Kwa mfano, ukiitisha kura ya maoni ya kuwataka wananchi waamue kama wanataka muungano au hawataki ni sawa kabisa. Hilo ni jambo moja. Kadhalika ukiitisha kura ya maoni ya kuwataka wananchi waamue kama wanataka Serikali mbili au tatu ni sawa. Hilo pia ni jambo moja.
Lakini si sahihi kuitisha kura ya maoni inayowataka wananchi waamue suala la muungano, idadi ya Serikali, madaraka ya Rais, maadili ya uongozi na utumishi wa umma, miiko ya uongozi wa umma, haki za binadamu, wajibu wa raia, wajibu ya mamlaka ya nchi, uraia katika Jamhuri ya muungano, madaraka ya Bunge, madaraka ya mahakama na kadhalika.
Mambo yote haya hayakuhitaji kupigiwa kura isipokuwa kama kutakuwa na kijitabu ambacho kitakuwa na vifungu ambavyo mpiga kura atatakiwa kuandika NDIYO au HAPANA au vinginevyo.
Huwezi kumtaka mtu apige kura moja kwa jambo fulani ambalo ni mchanganyiko wa mambo mengi tofauti. Unataka akubali au akatae yote kwa mpigo?
Halafu kuna jambo lingine ambalo waliomba ratiba ya mchakato wa Katiba hawakuliona jambo hilo ni hili hawakupanga Bunge la Katiba lingefika mwisho namna gani. Matokeo yake baadhi ya watu walimtaka Rais asitishe Bunge ilidhihirika kuwa Rais hakupewa madaraka hayo.
Ni katika mazingira hayo yote tunaweza kukubaliana kwamba mchakato wa Katiba haukuandaliwa kwa ufanisi. Nani anabisha?