Na Isri Mohamed

Mshambuliaji wa timu ya Taifa ya Tanzania, Mbwana Samatta ameitwa tena katika kikosi cha timu ya taifa kitakachoingia kambini Oktoba 4, mwaka huu kwa ajili ya kujiandaa na mchezo dhidi ya DR Congo wa kufuzu AFCON.

Akizungumza baada ya kutaja majina ya wachezaji 23 walioitwa, Kaimu kocha mkuu wa Taifa Stars, Hemed Morocco amesema timu ya taifa ni timu ya Watanzania wote na kila mchezaji ambaye anapafomu vizuri akiwemo Samatta basi ataitwa kikosini.

Mbali na Samatta Kocha Morocco ametangaza maingizo mapya kwenye kikosi cha Stars akiwemo Beki kisiki wa Simba sc, Abdulrazack Hamza na Nassor Saadun wa Azam fc, ambao wamefanya vizuri katika michezo ya hivi karibuni ya klabu zao.

Aidha Kocha Morocco amesema anaendelea kuwafuatilia wachezaji wa Tanzania wanaocheza katika nchi mbalimbali na atakapojiridhisha na viwango vyao wataitwa Stars.

Tanzania itashuka dimbani nchini Congo Oktoba 10, kuvaana na timu yao ya Taifa na mechi ya marudiano itachezwa jijini Dar es Salaam katika dimba la Mkapa, Oktoba 15, 2024.

Please follow and like us:
Pin Share