Mshambuliaji mpya wa Aston Villa ya Uingereza na nahodha wa Taifa Stars, Mbwana Samatta, ameendelea kung’ara kwa kuchaguliwa kuwa Mtanzania kijana mwenye ushawishi mkubwa kwa mwaka 2019.
Samatta ameibuka kidedea katika kura zilizoendeshwa na Kampuni ya Avance Media.
Taarifa iliyotolewa mwishoni mwa wiki na kampuni hiyo imeeleza kuwa hii ni mara ya pili kwa Samatta kushinda, kwani alishinda mara ya kwanza kura hiyo ilipoanzishwa mwaka 2017, wakati huo akichezea Klabu ya KRC Genk ya Ubelgiji. Mwaka 2018 Samatta alishika nafasi ya pili.
Samatta ni mchezaji wa kwanza kutoka Tanzania kusajiliwa na klabu inayoshiriki Premier League ya Uingereza. Alikamilisha usajili huo katika dirisha la usajili wa majira ya baridi mwezi uliopita na tayari amekwisha kuichezea timu hiyo mechi mbili na kufanikiwa kufunga goli moja.
Kampuni hiyo imeeleza kuwa katika matokeo ya kura ya mwaka huu, Samatta alifuatiwa kwa karibu na mshindi wa mwaka 2018 wa kura hiyo, ambaye ni Mtendaji Mkuu wa Ayo TV, Millard Ayo.
Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe, Jokate Mwegelo, ameshika nafasi ya tatu huku nafasi ya nne ikienda kwa mwanamuziki mahiri barani Afrika, Diamond Platnumz na mwanzilishi wa taasisi ya Msichana Initiative, Rebecca Gyumi, ameshika nafasi ya tano.
Jokate Mwegelo, ambaye alishinda kupitia kundi la Sheria na Utawala, pia amechaguliwa kuwa mwanamke mwenye ushawishi nchini kwa mwaka wa pili mfululizo.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi Mkuu wa Avance Media, Prince Akpah: “Kura hiyo inalenga kuwapata Watanzania vijana 50 ambao wana ushawishi mkubwa nchini.”
Anasema watu hao ni wale ambao mambo waliyoyafanya yameleta mabadiliko au ni viongozi ambao wamewezesha nchi kupiga hatua.
Watu hao wanatoka katika sekta tofauti kama vile ujasiriamali, wanamuziki, wanaharakati, watumishi wa umma na wanasiasa.
Baadhi ya vijana maarufu ambao wamo katika orodha ya washindi 59 wa mwaka 2019 ni pamoja na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, Carol Ndosi (Mtendaji Mkuu wa Alta Vista Events), mchekeshaji Idris Sultan, mwanamitindo Flaviana Matata, mwanamuziki Harmonize, Mwanasheria Jebra Kambole na mwandishi Rahma Mwita.
Pia wamo mwanamuziki Nandy, mshambuliaji wa Simba na Taifa Stars, John Bocco, mchezaji wa JS Soura (ambaye amehamia TP Mazembe) Thomas Ulimwengu, Naibu Waziri Juliana Shonza, mtangazaji wa Clouds FM Hamisi Mandi B Dozen, Doreen Peter Noni (Mtendaji Mkuu wa 102.5 LAKE FM), kundi la muziki la Navy Kenzo, mwanariadha Alphonce Simbu, mwanamuziki Rayvanny na mtangazaji wa Clouds FM, Perfect Crispin.