Mbunge wa Arusha Mjini (Chadema), Godbless Lema amehoji sababu za Bunge kutogharamia matibabu ya Tundu Lissu aliyepo nchini Ubelgiji tangu Januari 7, 2018 akipatiwa tiba ya mazoezi.
Lema ametoa kauli hiyo Jana Februari 8, 2018 bungeni mjini Dodoma wakati akichangia taarifa za utekelezaji wa shughuli za kamati za Bunge za Utawala na Serikali za Mitaa, Katiba na Sheria na Sheria Ndogo.
Lissu ambaye ni mbunge wa Singida Mashariki (Chadema) alishambuliwa kwa zaidi ya risasi 30 akiwa ndani ya gari lililokuwa nje ya makazi yake mjini Dodoma Septemba 7 mwaka jana, kupatiwa matibabu Hospitali ya Mkoa wa Dodoma ambapo siku hiyo hiyo alihamishiwa Hospitali ya Nairobi, Kenya.
Alipelekwa Ubelgiji Januari 7 kwa ajili ya tiba ya mazoezi na mara kadhaa familia yake imelishutumu Bunge kuwa kimya kuhusu matibabu ya mbunge huyo ambaye pia ni Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS).
Katika mchango wake, Lema alianza kwa kutoa pole kwa Spika wa Bunge, Job Ndugai aliyedai kuwa yupo nchini India kwa matibabu.
“Mheshimiwa Spika anatumia fedha za Serikali kupata matibabu na mbunge Lissu tumeendelea kumtafutia fedha za matibabu mitaani tena kwa mkopo,”amesema Lema.
Amebainisha kuwa kitendo cha Ndugai kutibiwa na fedha za Serikali huku Lissu ambaye ni mnadhimu wa Kambi Rasmi ya Upinzani bungeni akishindwa kupewa msaada na Bunge ni jambo ambalo halikubaliki.
Wakati akieleza hayo, alikatishwa na Mwenyekiti wa Bunge, Andrew Chenge akimtaka ajielekeze kwenye hoja tatu za taarifa za kamati huku mbunge wa Kishapu (CCM), Suleiman Nchambi akisema bima walizonazo wabunge zinawawezesha kupata matibabu.
“Kama hawana mawasiliano mazuri na Bunge nawashauri na nawapa taarifa wawasiliane na ofisi ya Bunge,” amesema Nchambi.
Kauli ya Nchambi iliibua mvutano bungeni, huku mbunge wa Tarime Vijijini (Chadema), John Heche akisikika akisema kauli ya mbunge huyo wa Kishapu ni sawa na kucheza na uhai wa mtu.
Kufuatia hali hiyo, Chenge aliingilia kati na kuwatuliza wabunge hao kwa kuwataja kwa majina, akiwemo Heche na mbunge wa Iringa Mjini (Chadema), Mchungaji Peter Msigwa.
Mwenyekiti huyo alipomtaka Lema kuendelea na mchango wake, mbunge huyo aliendelea kuzungumzia matibabu ya Lissu na kubainisha kuwa suala hilo linahusu utawala bora, si vinginevyo kama inavyodaiwa na Nchambi.
“…, Huyu (Nchambi) anasimama anaongea mzaha kuna watu wamepotea mmoja anaitwa Ben Saanane (msaidizi wa mwenyekiti wa Chadema-Freeman Mbowe) haya ni mambo yanayohusu utawala bora na sheria,” amesema Lema.
Amesema kujadili matibabu ya Lissu na masuala ya utekaji hawana lengo la kushutumu, bali ni kutaka mambo yarejee katika mstari.
Licha ya Lema kuendelea kuchangia taarifa hizo za kamati huku akikatishwa mara kwa mara, muda wake ulipomalizika alitakiwa na Chenge kuketi ili kumpisha mchangiaji mwingine.