Na Cresensia Kapinga, JamhuriMedia, Songea
Mbunge wa viti Maalum Mkoa wa Ruvuma Mariam Madalu Nyoka, ametoa kiasi cha sh.milioni 2 pamoja na mashuka ya wagonjwa 15 katika zahanati ya kijiji cha Muhepai ililiyopo kata ya kilagano halmashauri ya Songea vijijini mkoani Ruvuma, ili kuunga mkono jitihada za serikali katika kuboresha huduma za afya kwa wananchi pamoja na kuboresha mazingira ya kufanyia kazi wahudumu wa afya na kutoa faraja kwa wagonjwa.
Mbunge Nyoka amekabidhi fedha na shuka hizo jana ikiwa ni ahadi yake aliyoitoa Oktoba mwaka jana ya kuchangia fedha na shuka kwenye zahanati hiyo ambapo alisema kuwa ni sehemu ya ahadi zake za kuleta maendeleo ndani ya jamii.
“Ndugu zangu wananchi wa kijiji hiki cha Muhepai pamoja na viongozi mliombata nami mwaka jana mwezi kama huu nilitoa ahadi hapa ya kuchangia na mimi kiasi cha sh. Milioni 2 na shuka kumi za wagonjwa kwenye zahanati yetu hii lakini leo nimekuja kwa ajili ya kutekeleza ahadi yangu nimekuja na sh. Milioni 2 kutekeleza ahadi ile na niliahidi shuka 10 lakini nimeleta shuka 15 za wagonjwa “alisema mbunge Nyoka .
Alisema kuwa kati ya majukumu yake ambayo anaweza kufanya kwa wakati huu ni vyema ayafanye na amefanya hivyo ikiwa ni jitihada za kuunga mkono Serikali pamoja na Mbunge wa Jimbo la Peramiho Jenista Mhagama ambaye pia ni Waziri wa Afya.
Mbunge Nyoka amekuwa akichangia shughuli mbalimbali za maendeleo katika Mkoa wa Ruvuma, akishirikiana na jamii katika masuala ya afya, elimu, na maendeleo ya kiuchumi.
Naye Diwani wa kata ya Kilagano Festus Nchimbi amemshukuru mbunge huyo kwa niaba ya wananchi wa kata hiyo kwa kuwa aliahidi na ametekeleza na kwamba chama cha mapinduzi kilimwamini basi na wananchi hao watakuwa na amani wakati wanamchaguwa hawakukosea hasa kwa utekelezaji huo wa kuunga mkono jitihada za Serikali kuhakikisha unaunga mkono wananchi wa kata ya Kilagano hususani kijiji hicho cha Muhepai.
Kwa upande mwingine Mbunge Nyoka pia amejikita katika kusaidia ujenzi wa nyumba za makatibu wa UWT wa Chama cha Mapinduzi (CCM)Wilaya zote za Mkoa wa Ruvuma ambapo jana amekabidhi mifuko 100 ya saruji na matofari ya block 1000 kwa ajili ya ujenzi wa nyumba ya katibu wa UWT Songea vijijini.
Alisema kuwa mradi wa nyumba ya Katibu wa UWT Wilaya ya Songea vijijini umeanzishwa ili kutoa makazi bora kwa viongozi wa wanawake katika eneo hilo na kwamba Nyumba hiyo kukamilika itasaidia katika kuimarisha uongozi wa wanawake na shughuli za maendeleo.
Alieleza zaidi kuwa ujenzi wa nyumba hiyo unalenga kutoa mazingira mazuri kwa katibu kufanya kazi zake kwa ufanisi na pia kuhamasisha wanawake wengine kushiriki katika shughuli za maendeleo ya kijamii.
Kwa upande wake mwenyekiti wa UWT Wilaya ya Songea vijijini Schola Ngonyani alisema kuwa yeye pamoja na kamati yake yote ya utekelezaji na wanawake wote wa Wilaya ya Songea vijijini wanapokea zawadi aliyowapatia ya mifuko ya saruji 100 na tofari 1000 kwani sasa nyumba yao itakuwa imekamilika.