MBUNGE wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi amepelekwa mahabusu katika Gereza la Ruanda mkoani Mbeya baada ya kukosa dhamana katika kesi ya uchochezi inayomkabili.
Sugu na Mratibu wa Chadema Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, Emmanuel Masonga wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Mbeya leo Januari 16 na kupelekwa mahabusu jana Jumanne Januari 16, baada ya Wakili wa Serikali, Joseph Pande kuiomba mahakama kuzuia dhamana kutokana na usalama wa washtakiwa kutokana na kosa walililotenda.
“Kosa walilolitenda washtakiwa ni kutoa maneno ya fedheha yanayomtaja rais kuwa muuaji hivyo wakiwa nje wanaweza kupata matatizo kwa wananchi ambao hawajapendezwa na maneno hayo,” alidai Wakili Pande.
Hakimu Mkazi wa Mahakama hiyo, Michael Mteite alikubaliana na ombi hilo ambapo aliahirisha kesi hiyo hadi Januari 19, mwaka huu atakapotoa uamuzi wa dhamana.
Washtakiwa hao wanadaiwa kufanya uchochezi kwa kutoa lugha ya fedheha dhidi ya Rais John Magufuli, Desemba 30, mwaka jana akiwa katika viwanja vya mikutano vya shule ya msingi Mwenge iliyopo jijini Mbeya ambapo Sugu anadaiwa kutamka kuwa rais ni muuaji