Na Bwanku M Bwanku, JamhuriMedia, Kagera
Mbunge wa Jimbo la Bukoba Vijijini lililopo mkoani Kagera amewahakikishia wananchi wa kata ya Kemondo kwamba ndani ya mwezi mmoja ujao mradi wa maji Kemondo utakua umeanza kutoa maji na wananchi watapata huduma hiyo bila changamoto yoyote kwenye kata hiyo huku akimshukuru Rais Samia kwa kuhakikisha miradi ya maji inakuja Bukoba Vijijini na kukamilika ili wananchi wapate huduma hiyo.
Rweikiza ameyasema hayo wakati wa mwendelezo wa ziara yake Jimboni anayoitumia kufanya mikutano kwenye vijiji mbalimbali na wananchi ili kuwapa mrejesho wa kazi mbalimbali alizozifanya Jimboni, kusikiliza na kutatua kero za wananchi na kusukuma ajenda za maendeleo za wananchi.
“Mradi wa maji Kemondo, ndani ya mwezi mmoja ujao mwezi wa nne maji yanatoka Kemondo. Ule mradi walitengeneza chanzo pale wakaweka mabomba mpaka Kanazi, tanki limejengwa siku nyingi ili maji yaende Katerero, Kyema mpaka Bujugo na kazi hiyo imeisha itabaki kununua pampu kubwa kutoa maji hapa yapande mpaka Kanazi ni pampu kubwa.
“Nimepambana kwelikweli pampu zimenunuliwa Uturuki kwa fedha nyingi sana lakini pampu zikakwama Dar es Salaam kwasababu mnajua mambo ni mengi serikali inafanya mengi muda mwingine inaelemewa.
“Nikafuatilia akalipwa kiasi na mashine zimekuja hapa Kemondo na sasa tunataka zifungwe tutesti ziwashwe maji yapande Kanazi yaanze kusambaa kwa wananchi.
“Narudia mpaka mwezi wa 4 mwishoni maji ya Kemondo tayali yanamwagika kwenye mabomba, yanatoka kwenye ziwa yanatibiwa yanaingia kwenye tanki tayali wananchi kupata maji. Yataenda kata ya Katerero, yanakwenda mpaka Bujugo na kwingine Maruku baadae na zile kata mbili za Muleba Kaskazini kwa baadae.
“Kaja mtu mmoja hapa anasema Mbunge hana majibu kuhusu maji, sasa nilivyokua naomba maji toka kipindi cha Magufuli hapa sijui alikuwa wapi? Mnaniona Bungeni anavyohoji mawaziri kuhusu maji mnaniona, juzi kwenye ziara ya Mwenyekiti wa UWT- Taifa Mama Chatanda nimehoji kuhusu maji, sasa mtu akisema Mbunge hana majibu ya maji huyo anatudharau sisi kwamba hatuna akili.” amesema Mbunge Rweikiza.
Aidha mbunge Rweikiza amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuwakumbuka wananchi kuwaletea mradi mkubwa wa maji ambapo ametembelea vijiji vilivyopo kwenye mpango wa kupata visima vya maji ambavyo ni Taitoke, Lugaze, Kamuli na Kahyoro ambako amewaeleza wananchi vijiji hivyo ambavyo vina shida ya maji vinakwenda kupata maji baada ya kupata mradi wa visima vitano vikubwa vitakavyojengwa ambapo aliambatana na Mainjia wa maji watakaokuja kukagua na kuchimba kisima kirefu chenye maji ya kutosha na kujenga tanki ili maji yasambae kwa vitongoji na kwa watu wote.