Mahakama Kuu Kanda ya Mbeya imemtaka Mbunge wa Rungwe Magharibi, Saul Henry Amon, kubomoa na kujenga upya nyumba ya Serikali namba 162, kiwanja namba 1103, kitalu ‘S’ eneo la Mafiati Jijini Mbeya, iliyokuwa ikimilikiwa na Simbonea Kileo.
Akitoa hukumu hiyo katika kesi ya madai namba 16 ya 2015, Februari 8, mwaka huu, iliyofunguliwa na Simbonea Kileo dhidi ya Gladness Kimaro; Saul H. Amon, J.A. Kandonga na Mashango Investment Co. Ltd, Jaji Atuganile Ngwala amewataka wadaiwa hao kujenga upya nyumba ya Serikali waliyoibomoa, kulipa gharama za kesi, ndipo kesi Namba 24 ya mwaka 2009 ianze kusikilizwa upya katika Mahakama ya Wilaya.
Nyumba hiyo iliuzwa kwa njia ya mnada kwa kiasi cha Sh milioni 250 kwa Amon, ambaye aliibomoa baada ya kuuziwa wakati shauri likiwa linaendelea mahakamani.
Taarifa iliyotolewa na Ofisi ya Msajili Msaidizi wa Hati, Mkoa wa Mbeya, inaonesha hati hiyo yenye namba 11443-MBYLR aliyopewa Simbonea Kileo baada kuuziwa nyumba hiyo na Wakala wa Majengo (TBA) kwa taratibu zote zinazotakiwa, imebadilishwa jina la mmiliki na kusomeka Saul Henry Amon.
Pamoja na mmiliki huyo wa pili kupewa hatimiliki ya nyumba hiyo, hakuna taarifa zozote zilizotolewa kwa mmiliki wa awali kwamba hatimiliki aliyokuwa nayo imehamishiwa kwa mtu mwingine, jambo ambalo ni kinyume cha utaratibu.
Hatimiliki hiyo inaonesha ilibadilishwa Aprili 1, 2007 na kuwa itadumu kwa kipindi cha miaka 33 huku mmiliki huyo mpya wa eneo hilo akilipa kodi ya ardhi kiasi Sh 24,540 kwa kiwanja hicho.
Kileo amesema hakupewa taarifa yoyote kutoka kwa wauzaji, au Mahakama za kumtaka akabidhi hati hiyo ili umiliki uelekezwe kwa Amon zaidi ya kutolewa kwenye nyumba yake na dalali.
Msajili wa Hati, Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Subira Sinda, amesema kama uamuzi ulitolewa na Mahakama ilitakiwa mmiliki wa nyumba hiyo apewe taarifa (notice) kwa njia yoyote na kama haikufanyika hivyo ilikuwa ni kinyume cha utaratibu.
“Kipengele cha miaka 25 ambacho ni kati ya masharti kwa mtu anayeuziwa nyumba na Serikali kinaweza kuondolewa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali iwapo atakuwa na haja ya kufanya hivyo, lakini sielewi kilichofanyika huko Mbeya, labda atafutwe Msajili Msaidizi wa Hati,” amesema.
Kileo, ambaye ni mtumishi wa umma, aliuziwa nyumba na Serikali na kukabidhiwa hati yenye Namba 11443-MBYLR iliyotolewa Oktoba 2007 baada ya kumaliza kulipa deni lote alilokuwa akidaiwa, amesema sakata hilo lilikithiri kwa mizengwe ya kila namna.
Amesema mwaka 2012 Mwanasheria wa Serikali aliwataka TBA kufungua kesi dhidi ya mnunuzi na muuzaji wa nyumba ya Serikali, lakini kwa makusudi hawakuweza kufanya hivyo na kuyaacha masharti waliyoyaweka yakikiukwa.
Awali, mbunge huyo alipohojiwa na gazeti hili kuhusu nyumba hiyo iliyouzwa kwa mnada ulioibua mzozo mkubwa, alisema baada ya kuinunua aliiuza tena kwa mtu mwingine ambaye hakutaka kumtaja jina.
Kileo alikopeshwa na Serikali nyumba hiyo kupitia Wakala wa Majengo kwa mkataba namba 1531, lakini iliuzwa kwa mbunge huyo Julai 5, 2012 kwa amri ya Mahakama ya Wilaya ya Mbeya baada ya ndoa yake kuvunjika mwaka 2007 kutokana na kutelekezwa na mkewe, Gladness Kimaro (ambaye ni mdaiwa wa kwanza katika shauri hilo), na watoto wake watatu tangu Januari 2001.
Kileo amesema kabla ya nyumba hiyo kupigwa mnada, alimjulisha Meneja wa TBA Mkoa wa Mbeya, ambaye alimshauri apeleke nyaraka zote zinazohusiana na kesi hiyo Makao Makuu ya Wakala wa Majengo Jijini Dar es Salaam, na baada ya kukabidhi nyaraka hizo, Juni 2012 hakuna hatua zozote zilizochukuliwa hadi nyumba hiyo inauzwa na kubomolewa.
Anasema, baada ya kuona hakuna hatua zozote zinazochukuliwa, aliomba ushauri kwa Mwanasheria wa Serikali ambaye alimshauri kupitia Mwanasheria wa TBA kwamba afungue kesi dhidi ya mnunuzi wa nyumba ya Serikali kupinga uuzwaji wa nyumba hiyo.
“Kwa upande wangu nilikuwa tayari nimefungua kesi ya kupinga mnada huo pamoja na kuomba marejeo. Kesi ya kupinga mnada huo ilimalizika kwa kufutwa kwa mnada huo na kuamriwa mnunuzi arudishiwe fedha zake,” amesema.
Licha ya kupewa amri ya zuio na Baraza la Ardhi na barua kutoka TBA Mkoa wa Mbeya zikimtaka Kandonga asiuze nyumba hiyo, aliendelea na utaratibu huo.
Amesema pamoja na zuio jingine kutoka kwa Meneja wa TBA mkoani Mbeya, la kuuza nyumba ya Serikali kwa kuwa ni kinyume na utaratibu na masharti ya nyumba zilizouzwa na Serikali kwa watumishi wake kwa barua ya Julai 4, 2012, lakini alikaidi maelekezo hayo.
Katika mkataba wa mauziano kati ya TBA na mtumishi wa umma anayeuziwa nyumba, vifungu namba 9 na 10 vinaeleza kwamba mtumishi yeyote aliyeuziwa nyumba ya Serikali au mrithi wake, hawaruhusiwi kuuza nyumba hadi hapo itakapotimia miaka 25 kuanzia tarehe aliyopewa hatimiliki.
Kwa kuzingatia vifungu hivyo vinavyoeleza masharti kwa mnunuzi wa nyumba ya Serikali ikiwamo kuuza au kubadili matumizi yake baada ya kipindi cha miaka 25 tangu alipokabidhiwa hati, nyumba hiyo ilipaswa kuuzwa Oktoba 2032.
Mmoja wa mawakili wa Kileo, Justinian Mushokorwa, ameliambia JAMHURI kuwa tangu ilipotolewa hukumu na Jaji Ngwala kwamba wadaiwa katika shauri hilo wajenge nyumba waliyoibomoa, ndipo maombi mapya yaanze kusikilizwa, hakuna utekelezaji wowote uliofanyika.
“Sharti lilitolewa ni kujengwa nyumba iliyobomolewa na ndipo shauri lianze kusikilizwa; na wadaiwa kushindwa kutekeleza amri hiyo ya Mahakama ni kuchelewesha maombi kuanza kusikilizwa upya,” amesema Wakili Mushokorwa.
Amesema madai yote katika shauri hilo ni yale yale ambayo yamekuwa yakiripotiwa mara kwa mara; na kwamba taratibu nyingine za kisheria zinaendelea kuchukuliwa. Hata hivyo, wakati Jaji Ngwala akitoa uamuzi huo, wadaiwa wote wanne hawakuwapo mahakamani.