DODOMA

Na Suleiman Sultan

Mbunge wa Viti Maalumu (CCM), Khadija Hassan Aboud, amesifu utendaji wa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi, akisema ameleta mabadiliko katika utoaji haki, kupunguza  dhuluma, uonevu na kuondoa migogoro mingi nchini.

Akizumgumza na gazeti hili jijini Dodoma, Khadija anasema Lukuvi ameipa heshima serikali kwa utatuzi wa migogoro na kuwapa haki waliodhulumiwa.

“Ipo haja wizara hii ikaongezewa bajeti ili kuwaongezea hamasa ya kazi waziri, naibu wake na watendaji wengine. Hawa wanajituma sana huku wakizingatia sheria na kutoa uamuzi bila upendeleo,” anasema Khadija. 

Khadija anasema viongozi na maofisa wa Wizara ya Ardhi husimamia vema sheria za nchi wakionyesha nia ya kuziondoa kabisa zile zama za uonevu, hasa vijijini.

“Wapo waliodhulumiwa mashamba baada ya wazazi wao kupoteza maisha. Wengine wamedhulumiwa kwa kuwa tu ni wanyonge, hawana fedha za kupata hatimiliki za viwanja na mashamba. 

“Kuna wengine wameporwa na ndugu zao waliouza ardhi bila wahusika kushirikishwa. Yapo mashamba yamevamiwa na ndugu wa familia moja,” anasema akibainisha baadhi ya sababu za migogoro mingi ya ardhi nchini. 

Anasema ardhi ni rasilimali adimu inayoweza kumpa manufaa mwananchi fukara na kutajirisha ikiwa ataitumia kwa malengo maalumu, hivyo akaitaka Wizara ya Ardhi kuwa makini kuwasaidia wananchi maskini wasitapeliwe. 

Anashauri wakazi wa vijiji waelimishwe zaidi kuhusu umiliki na matumizi bora ya ardhi, sambamba na kutambua haki zao.

“Kwenye baadhi ya halmashauri za wilaya kumefanyika ghiliba kubwa. Watu wameporwa ardhi kinyume cha sheria. Wapo maofisa ardhi, wapimaji na maofisa mipango miji wamehusika kudhulumu watu kwa kufuta hati za umiliki halali au kubadilisha ramani kinyume cha sheria,” anasema Khadija.