Na Mwamvua Mwinyi, JamhuriMedia, Kibaha

MBUNGE wa Jimbo la Kibaha Mjini Silvestry Koka na Mkuu wa Wilaya ya Kibaha Nickson John, wameungana kuanzisha kliniki ya wasanii kwa ajili ya kuibua vipaji ili kuwainua na kuwaendeleza walengwa .

Koka aliyaeleza hayo, wakati wa semina elekezi kwa wanachama wa Chama cha Waigizaji Kibaha Mjini (TFDAA).

Alifafanua ,lengo la kliniki hiyo ni kuwainua wasanii ili wafanye kazi hiyo kibiashara kwani serikali inathamini sanaa na kuweka mazingira mazuri.

“Rais Samia Suluhu Hassan ni mpenda michezo namba moja kwani ametengeneza na kuboresha mazingira na anatambua mchango wa wasanii hivyo nimeona niunge mkono jitihada hizo kwa kuwaandalia kliniki hiyo,”alisema Koka.

Alisema kuwa watashirikiana na Mkuu huyo wa Wilaya ambaye naye ni mwimbaji ambapo watashirikiana na wataalamu wa sanaa ili kiwapata wasanii wenye vipaji.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Kibaha Nickson John alisema kuwa watatafuta wasanii watatu au wanne wa muziki na sanaa ambapo watawatumia waimbaji wakiwemo Nandi, G Nako, Jux na Weusi na wataalamu wa fani ya uigizaji.

Kwa upande wake Rais wa Shirikisho la Sanaa za Maonyesho Cynthia Henjewele alisema kuwa wasanii wanapaswa kujisajili ili wapate fursa mbalimbali zikiwemo za mikopo.

Awali mwenyekiti wa Jumanne Kambi (TFDAA) alisema kuwa wana malengo ya kufanya uzinduzi wa mfuko wa chama Novemba mwaka huu na wangetamani Rais wa awamu ya nne Dk Jakaya Kikwete awe mgeni rasmi.

Ofisa habari wa chama hicho Ally Kinyunyu alisema kuwa mafunzo hayo yatawasaidia kutambua fursa mbalimbali na kupata uzoefu kutoka kwa waliofanikiwa kwenye sanaa.