MBUNGE wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi amerudishwa rumande katika Gereza la Ruanda mkoani Mbeya hadi Jumatatu wiki ijayo ambapo kesi yake ya kutoa maneno ya uchochezi itakaposikilizwa mfululizo.
Sugu na Mratibu wa Chadema Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, Emmanuel Masonga wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Mbeya kwa mara ya pili siku ya leo, baada ya kukosa dhamana Januari 16 aliposomewa mashtaka kwa mara ya kwanza.
Hakimu Mkazi wa Mahakama hiyo, Michael Mteite aliiahirisha kesi hiyo mpaka leo lakini imeshindikana kusikilizwa na hivyo Mbunge huyo kurudishwa tena mahabusu hadi Jumatatu ambapo kesi hiyo itasikilizwa tena.
Sugu na Msonga wanadaiwa kufanya uchochezi kwa kutoa lugha ya fedheha dhidi ya Rais John Magufuli, Desemba 30, mwaka jana akiwa katika viwanja vya mikutano vya shule ya msingi Mwenge iliyopo jijini Mbeya ambapo Sugu anadaiwa kutamka kuwa rais ni muuaji.