Na Mwandishi Wetu,JamhuriMedia,Dodoma

Mbunge wa Jimbo la Ukonga,Jerry Silaa,ameahidi kutembea pamoja na wabunge wenzake katika kuhakikisha kuwa sheria zinazobinya sekta ya habari zinakuwa rafiki.

Ameyasema hayo Novemba 8, 2022 wakati akizungumza na uongozi wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), na Wadau wa Haki ya Kupata Habari (CoRI), jijini Dodoma.

Uongozi wa TEF na CoRI walikutana na mbunge kwa nia ya kuzungumzia baadhi ya vipengele vilivyopo kwenye sheria ya habari ya mwaka 2016 vinavyokandamiza uhuru wa habari nchini.

Jerry amesema kuwa katika kufanikisha mchakato huo atashirikiana na wabunge wenzake ili sekta ya habari iondokane na vikwazo hivyo ambavyo vinachangia kukosekana kwa uhuru wa habari.

“Mimi na wabunge wenzangu tutashirikiana katika kuhakikisha kuwa sheria ambazo zinabinya uhuru wa habari zifanyiwe marekebisho. Dunia imebadilika na hatuwezi kubaki hapa tulipo,’amesema Jerry.

Naye Deodatus Balile, Mwenyekiti wa TEF alimuelezea mbunge huyo kuwa sheria ya habari ya mwaka 2016 imeweka mazingira ya kumuhofisha mwandishi wa habari.

Balile amesema kuwa ndani ya sheria hiyo kuna vipengele mbalimbali vinaua tasnia ya habari akitolea mfano kipengele kinachompa nguvu Mkurugenzi wa Idara ya Habari (MAELEZO) kufungia chombo cha habari kwa namna anavyoona inafaa.

“Katika safari ya mabadiliko haya, tumeungana taasisi zote za habari ili kuwa na kauli moja.Tumeunganisha nguvu ili kufikia lengo la kuondoa vipengele hivyo ambavyo vinabana sekta ya habari,” amesema.

James Marenga,Mjumbe wa CoRI kutoka Taasisi ya Vyombo ya Habari Kusini mwa Afrika (MISA), tawi la Tanzania alimweleza Jerry kwamba, tasnia ya habari haina tofauti na tasnia nyingine nchini katika utendaji kazi.

Marenga amabaye ni wakili wa kujitegemea amesema,ikiwa mawakili wanatengeneza taratibu zao na kuzifanya kuwa rejea katika kazi zao, inashindikanaje wanahabari nao wakajiwekea utaratibu wa ‘kujihukumu’ kama ilivyo tasnia nyingine?

“Mimi ni mwanasheria, katika taasisi yetu tulitengeneza ‘cord of conduct’ wenyewe na hizo ndio zinatuongozi, ni busara na wanahabari wakawa na utaratibu wao kisheria unaosimamiwa na wenyewe katika kuhakikisha maadili ya uandishi wa habari yanafuatwa,’’ amesema.

Jessy Kwayu,Mkurugenzi Mkuu wa Media Brains Inc Ltd amesema, sheria ya habari ya mwaka 2016 ilipitishwa katika mazingira ambayo si rafiki.

“Vipengele 19 vya sheria hiyo vilijaribiwa kwenye sheria za nchi, vikaonekana kutoingia katika mizani ya kisheria,’’ amesema Kwayu.