Na Deodatus Balile, JamhuriMedia, Bukoba

Julai 23, 2024 niliandika makala yenye kichwa cha habari kisemacho: “Rais Samia ana maamuzi magumu.”

Makala hii niliiandika baada ya Rais Samia Suluhu Hassan kutengua uteuzi wa aliyekuwa Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye na Waziri Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, January Makamba na Naibu wake, Stephen Byabato.

Utenguzi wa watatu hawa ulitokana na mambo mengi. Kwa Nape na Makamba, ilitajwa kuwa waliamini wao wako karibu na Rais Samia kwa kiwango cha kujiamini kuwa kila wanachomwambia anakitekeleza, na inadaiwa walianza kupanga safu za uongozi.

Waliamini wao wakiondoka serikalini, mambo yasingekwenda, kumbe Julai 22, 2024, Rais akaamua kuwatengua. Waliondoka, Serikali haijayumba na kila kitu kinakwenda sawa.

Sitanii, ukiacha mazonge mengine yaliyokuwa yanaendelea katika ‘mitkasi’, Nape aliponzwa zaidi na kauli yake ya jinsi ya kuhesabu kura aliyoitoa akiwa pale Kashai, Bukoba, akimweleza Mbunge wa Bukoba Mjini (CCM), Stephen Byabato, kuwa atamsaidia kuhakikisha anapata ushindi iwe kwa njia halali au haramu. Kauli hii iliwachefua Watanzania.

Na kwa kweli viongozi wengi wa CCM walikuwa wamejiwekea utaratibu wa kutoa kauli za kibabe kama hizo, ila baada ya Nape kutenguliwa, wakajua Rais Samia hapendi wizi wa kura na sasa kauli zimepungua kwa kiasi kikubwa.

Ilikuwa imeelekea kuzoeleka kuwa upigaji kura nchi hii hauna maana tena. Kilio hiki kimeendelea kuwapo na hata uchaguzi wa Oktoba, mwaka huu, wapigakura wengi wana wasiwasi iwapo matokeo yatatokana na sanduku la kura au goli la mkono.

Rais Samia amesema bayana kuwa uchaguzi huu utakuwa huru na wa haki.

Naomba ninukuu nilichokiandika Julai 23, 2024 kuhusu Byabato, kisha nifafanue kichwa cha habari cha makala hii kinachosema: “Mbunge Byabato ameiweza Bukoba.” Niliandika hivi:

“Byabato. Huyu naye chumvi imetiwa kwenye kidonda. Sijui kama anakubaliana na kauli ya Nape au aliipinga pale mkutanoni Kashai!

“Ila kwa vyovyote iwavyo, kwa siasa ninazozifahamu za Bukoba, hapa nimshauri kwa nia njema tu, kuwa mafao yake ya ubunge ayapangie mradi mzuri, awekeze. Kwa ubunge wa Bukoba Mjini; ni bora apite anaaga. Najua hawakosekani watu wa kumtia moyo hewa, wakamwambia kuwa anakubalika, atatoboa. Mimi huwa ni muwazi. Byabato unafahamu mlango ulioingilia kwenye ubunge hapo Bukoba, sina uhakika kama mlango huo bado uko wazi.

“Usiponisikiliza ukawa sawa na Rais Joe Biden wa Marekani wiki za kwanza alivyoshupaa ndani ya chama cha Democrat, majuto ni mjukuu. Nakushauri tena, mafao yako ufungue mradi utakaosaidiana na uwakili wako, maisha yaendelee.

“Sitanii, heri mimi ninayekushauri hadharani, maana najua kwa kukushauri hivi utaniongeza katika orodha ya watesi wako. Ukumbuke kilio ulichoangua pale stendi, Mradi wa Stendi uliotelekezwa Kyakailabwa, soko la Bukoba, barabara za baadhi ya mitaa kwa kata zote 14 za Jimbo la Bukoba, hasa zile 8 za Green Belt – Nyanga, Kagondo, Buhembe, Nshambya, Kahororo, Kibeta, Kitendaguro na Ijuganyondo

“Kata za katikati ya mji za Bakoba, Bilele, Hamugembe, Kashai, Miembeni na Rwamishenye, nazo wanalia hali ya usalama si shwari, wizi umezidi. Kimsingi, najua hukosi marafiki wa kukwambia; “ni wewe tu!” Lakini usiponisikiliza mafao yako ukayaekeza katika kutafuta ubunge kipindi cha pili, utajuta. Na kama huamini kauli yangu, wapigie simu Balozi Hamisi Kagasheki na Joseph Mujuni Kataraiya. Ni wana CCM wenzako, watakusaidia ushauri wa kichama.”

Nimerudia chapisho hili kwa ujumla wake, kutokana na ninacholenga kukiandika hapa. Baada ya kuandika makala hii, Byabato alinipigia simu tukazungumza kwa saa mbili. Alitaka nimweleze mambo makuu matatu hadi manne ninayoamini yatamfanya ashindwe uchaguzi. Niliweka bayana kuwa mimi sina ugomvi naye kama yeye, ila ugomvi wangu ni yeye kushindwa kuleta maendeleo katika Jimbo la Bukoba.

Nilitaja yafuatayo: Nilimwambia ameshindwa ujenzi wa soko, ameshindwa ujenzi wa Barabara ya Nyangoye, ameshindwa ujenzi wa Stendi ya Mabasi Nyanga, ameshindwa bonde na ujenzi wa Daraja la Mto Kanoni. Suala la barabara za mtaani, nalo nilitaja ila kimsingi baada ya ufafanuzi wake, ilionekana ni tatizo la Halmashauri ya Mji, naye anaendelea kuwabana.

Nilimwambia akiweza mawili kati ya hayo manne makubwa, mimi nitamuunga mkono. Kwa unyenyekevu mkubwa akaniambia kama ni hayo, nisiwe na wasiwasi, anachagulika. Nikiri nilishangazwa na kiwango cha kujiamini cha Byabato katika simu ile. Akasema daraja na kingo za Mto Kanoni vitajengwa, Barabara ya Nyangoye itajengwa kupunguza ukali wa mlima, stendi nayo itajengwa na soko litajengwa.

Sitanii, maelezo haya nikiri niliyachukulia kama sanaa (usanii) ya hali ya juu. Jumamosi iliyopita nimekuja Bukoba kwa ajili ya kula Sikukuu ya Pasaka na mama yangu mzazi, Ma Angelina.

Nilipotoka ‘airport’, nikataka kufika Kanoni kwa nia ya kununua senene kidogo. Nilianza kushitushwa na jengo la Shihata kuvunjwa. Wananchi wakanieleza kuwa Daraja la Kanoni limefungwa; zinajengwa njia nne kutoka Rwamishenye hadi Kastam.

Nikauliza, nikabaini kuwa ujenzi wa Daraja la Mto Kanoni, ni hatua inayoendana na ujenzi wa kingo za mto huo. Nyangoye, tayari mlima umekatwa na barabara sasa imeondoa hatari iliyokuwapo. Soko la Bukoba nalo nikakuta tayari wafanyabiashara wamehamia Machinjioni na ujenzi umeanza. Stendi ya Mabasi ya Mkoa nayo mkataba umesainiwa inajengwa Nyanga.

Kwa hakika baada ya kuyashuhudia haya, nimempigia simu Byabato. Nimemwambia kwa upande wangu hana deni tena. Alichoahidi amekitekeleza. Nafahamu baada ya Jimbo la Bukoba kushikiliwa kwa muda mrefu na Mzee Samwel Ntambala Luhangisa, aliingia John Mjuni Kataraiya. Aliishia kipindi kimoja, likachukuliwa na Wilfred Lwakatare wa CUF.

Lwakatare naye hakukatiza zaidi ya kipindi kimoja, likachukuliwa na Balozi Khamis Suedi Kagasheki, ambaye naye alikaa vipindi viwili 2005 – 2015, ila Lwakatare akarejea 2015 – 2020 zamu hii kupitia CHADEMA.

Mwaka 2020 Byabato akaingia. Kipindi chote hiki Jimbo la Bukoba lilikuwa ni uwanja wa mapambano ya kisiasa. Miradi hiyo niliyoitaja kuwa sasa Byabato amewezesha kuanza ujenzi wake, ilikuwa inajadiliwa tu. Nyumba ya Mzee Muhazi pale Nyangoye, iliwekewa alama ya ‘X’ mwaka 1980, lakini hadi mwaka huu ndipo imebomolewa kupisha ujenzi wa barabara ya Nyangoye.

Sitanii, Byabato ametafuna mfupa uliowashinda wenzake. Naelewa siasa za hapa Bukoba, kuna mgogoro wa maneno kati yake na baadhi ya viongozi wa serikali. Kubwa ambalo liliwashinda wengi; Soko la Bukoba, ilikuwa linakwamishwa na “maseneta 54” waliokuwa wanamiliki vizimba zaidi ya 200 vya soko hilo na kukodisha kwa wafanyabiashara wadogo.

Mfano, seneta mmoja alikuwa anakodisha kizimba kwa Sh 200,000, wakati yeye halmashauri ya mji analipa Sh 60,000 tu kwa mwezi.

Byabato alifanya mkakati maseneta hawa wakanyang’anywa vizimba. Ni wazi hawamfurahii. Ni wazi walikuwa na uwezo wa kifedha na wanapenya katika ngazi mbalimbali za serikali. Hawa pamoja na miradi hii iliyokwama tangu mwaka 1980 kuanza, wameamua kufumba macho gizani. Wamefunga kitambaa usoni wasiione.

Mimi nasema kinachotafutwa ni maendeleo ya Jimbo la Bukoba na si kumfurahisha yeyote awaye. Kwa umri wangu huu wa zaidi ya nusu karne, alichokifanya Byabato, sijakishuhudia kitambo. Naamini wajumbe ndani ya CCM hawatavutwa na maneno, bali wapite katika maeneo haya ya miradi niliyoyataja, kisha wakati wa kupiga kura za maoni waamue kama wanachagua maendeleo au majaribio ya wabunge. Ukiniuliza, ninasema: “Mbunge Byabato ameiweza Bukoba, apewe nafasi nyingine.” Mungu ibariki Tanzania.

+255 784 404 827