BUSEGA
Na Mwandishi Wetu
Mbunge wa Busega, Simon Songe, amemnusuru Diwani wa Mkula, Goodluck Nkalango, kupewa kesi ya uhujumu uchumi.
Nkalango na viongozi kadhaa wa Kijiji cha Kijilishi wanadaiwa kutorosha fedha za umma takriban Sh milioni 7.8.
Mkuu wa Wilaya ya Busega, Gabriel Zacharia, aliwaweka rumande Nkalango, mtendaji na mwenyekiti wa Kijiji cha Kijilishi (majina yanahifadhiwa) wanaodaiwa kutorosha fedha hizo ambazo ni asilimia 10 ya mauzo ya madini zilizopaswa kuingia kwanza kwenye akaunti ya mkurugenzi wa halmashauri.
Akizungumza na JAMHURI, Songe anasema Nkalango aliwekwa ndani akituhumiwa kuwachochea viongozi wenzake kutorosha fedha.
“Ni fedha za ahadi ya mwekezaji kwa kijiji kilichotoa ardhi ya uchimbaji madini, kwamba angekipatia asilimia 10 ya mauzo kama sheria inavyoelekeza,” anasema mbunge.
Anasema wananchi walipeleka taarifa kwake wakilaumu diwani wao kuwekwa kizuizini kwa kupigania kile walichokiita haki yao.
Kwa mujibu wa mbunge huyo, wananchi walimtaka kusaidia kumtoa rumande diwani kabla wao hawajachukua uamuzi wa kwenda kituo cha Polisi kumtoa.
“Nikawasiliana na DC, baada ya kumweleza kisa kizima, akaniambia nimwelekeze diwani na viongozi wengine wakaweke fedha kwenye akaunti ya mkurugenzi, si mikononi mwa mtu,” anasema.
Anasema alipowasiliana na Nkalango, alimwambia kuwa yeye hana fedha hizo bali zipo kwa viongozi wa kijiji.
Anasema walikuwa na hofu kwamba fedha hizo ambazo ni haki yao zikiwekwa kwa mkurugenzi hawawezi kuzipata tena wakati zimo kwenye mipango yao ya maendeleo.
“Viongozi hao waliziweka hizo fedha kwenye akaunti ya kata wanayoamini kuwa ni salama zaidi kwao, kisha wakanipa risiti niipeleke kwa DC,” anasema mbunge.
Wananchi wamemweleza mbunge kwamba DC amekosea kwa kuwa asilimia 10 ya mauzo ya madini ni haki ya kijiji isipokuwa fedha za halmashauri ni Sh 1,000 wanazopewa na mwekezaji kwa kila mfuko wa mchanga wa madini unaotolewa mgodini.
Alipoulizwa kuhusu sakata hilo, Zacharia amemtaka mwandishi kufanya uchunguzi wa kina na kuondoa kila aina ya shaka inayoweza kuwapo kwenye mazingira ya sakata hilo.
“Serikali ina utaratibu wake wa kufanya kazi, na anayevunja sheria za nchi ni lazima ashughulikiwe kwa mujibu wa sheria pasipokujali nafasi ya mtu huyo, bila uonevu wala upendeleo,” amesema DC.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Busega, Sundi Muniwe, hakuwa katika nafasi nzuri ya kulizungumzia hilo, akisema kwa ufupi kuwa: “Ni kweli (diwani aliwekwa rumande) lakini kwa sasa niko kanisani, nitakutafuta baadaye.”
Hata hivyo hadi tunakwenda mitamboni, Muniwe hakumtafuta mwandishi wa JAMHURI.
Akizungumza na mwandishi baada ya kutolewa rumande, Nkalango amesema:
“Sisi ni viongozi wa wananchi. Mimi nina dhamana ya kuwawakilisha, hivyo mkuu wa wlaya hakuwa na sababu ya kunifuata usiku na bunduki akiwa na askari polisi na kunidhalilisha kwa Sh milioni 7.8 ambazo hakuwa na uhakika kama ziko kwangu.
“Nipo tayari kueleza ukweli halisi wa tukio hili popote, lakini si kuaibishana mbele ya familia kama majambazi.”
Inadaiwa kuwa afya ya mmoja wa viongozi waliowekwa rumande huku akiwa mjamzito ilidhoofika na mara tu baada ya kutolewa, alilazimika kupelekwa haraka hospitalini kupata huduma ya kwanza, kisha kuruhusiwa baada ya afya yake kuimarika.