Kwa mara nyingine ndugu msomaji naomba kukupa heri ya mwaka mpya 2018. Najua utakuwa umeshangaa leo inakuwaje naandika juu ya uchaguzi na naacha kugusia suala la muhogo. Muhogo sitauacha. Chini ya makala hii naeleza fursa mpya iliyopatikana ya muhogo. Kelele nilizopiga zimeanza kuzaa matunda. Mungu anaipenda Tanzania na nitaeleza kwa kina kwa nini napigania muhogo.

Mwishoni mwa wiki Kamati Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), imeteua wagombea ubunge wawili kushiriki Uchaguzi Mdogo katika majimbo ya Kinondoni, Dar es Salaam na Siha, Kilimanjaro. Walioteuliwa ni Dk. Godwin Mollel (Siha) na Maulid Mtulia (Kinondoni).

Sitanii, Mollel amejiuzulu ubunge kutoka CHADEMA na Mtulia amejiuzulu ubunge kutoka Chama cha Wananchi (CUF). Wawili hao wamesema wamejiunga CCM baada ya kuridhishwa na utendaji wa Rais John Pombe Magufuli. Binafsi sina tatizo na uamuzi wao, ila napata shida na gharama zinazoambatana na uamuzi wao.

Nimepata kusema hapa siku za nyuma kuwa uchaguzi mdogo unagharimu taifa hili wastani wa Sh bilioni 3. Kiasi hiki ni kikubwa mno. Kingeweza kujenga barabara za kawaida za kiwango cha lami (barabara za mtaa) zisizopungua kilomita 20 au zaidi kwa wastani wa Sh milioni 150 kwa kilomita ya barabara za mtaa.

Kiasi hiki kama yangejenga madarasa kwa gharama ya Sh 8,000,000 kila darasa, basi nchi hii ingeweza kutumia kiasi hicho cha Sh bilioni 3 kujenga madarasa 375. Kwa majimbo mawili ina maana nchi hii ingeweza kujenga madarasa 750. Ukitumia nguvu za wananchi darasa likajengwa kwa nusu ya hiyo bei, unaweza kujenga madarasa 1,500.

Sitanii, shule nyingi zina wastani wa madarasa 8 hadi 10. Kwa shule za sekondari zikiwa na mikondo 3 kuanzia kidato cha kwanza hadi cha 4, basi inakuwa na madarasa 12. Hii ina maana kwa kutumia mkondo wa Sh milioni 8 kwa chumba cha darasa, fedha za uchaguzi mdogo katika majimbo mawili zinaweza kujenga shule mpya 125. Tukitumia mfumo wa nguvu za wananchi, tunaweza kujenga shule mpya 250!

Ndugu zangu Watanzania. Wakati umefika tufikiri jinsi ya kuepuka gharama hizi. Tubadili sheria ama iruhusu wabunge wanaoamua kuhama, wahame na ubunge wao au chama alichotokea kiteue mtu awe mbunge au izuie wabunge waliohama kugombea tena ndani ya miaka 5 kupunguza vishawishi vya kuhama na gharama zisizo za lazima kwa walipa kodi.

Sitanii, kichwa na makala hii kinasema; “Mbowe kususa uchaguzi unaua upinzani”. Maoni niliyotoa hapo juu ni kwa ajili ya siku za usoni. Ni wazi kuwa nchi yetu kwa sasa sheria yake ya uchaguzi inaruhusu yanayotokea kutokea. Sheria inaendelea kuwa sheria hadi inapobadilishwa, hata kama ni sheria mbaya.

Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) nasema hakiutendei haki upinzani kwa kukataa kushiriki uchaguzi. Kimekataa kushiriki Longido, Songea Mjini na Singida Kaskazini kwa maelezo kuwa Uchaguzi Mdogo wa Madiwani wa Desemba, CCM iliuvuruga, iliumiza wafuasi wake, ililazimisha ushindi na kadhalika.

Nasema inawezekana hayo yalitokea. Freeman Mbowe na Chadema wanapaswa kufahamu jambo. Kwamba vyama vyote vya siasa vinatuuzia falsafa za jinsi ya kutuletea maendeleo ya taifa letu na mtu mmoja mmoja kwa haraka. Hii ni sawa na mechi ya soka. Kila timu inatumia mbinu zinazoiwezesha kutwaa ushindi.

Tofauti iliyopo kati ya soka na siasa ni kwamba wakati ushindi wa soka furaha huishia katika furaha ya kisaikolojia kwa mashabiki, ushindi wa kisiasa ni maisha ya wananchi. Unakipa chama nguvu ya kubadili Katiba, Sera, Sheria na miongozo mbalimbali. Unakipa chama mamlaka ya kuamua mfumo wa uchumi. Chama kinaweza kubana fedha hadi benki zikafungwa au kikaachia hadi fedha zikawekwa kwenye soksi kama enzi za Mzee Ruksa (Ali Hassan Mwinyi).

Sitanii, siasa siyo dansi kusema washiriki watakumbatiana wakati mchezo unaendelea. Mbowe ukitaka kufahamu ugumu waulize CCM wakati wanapanga mikakati ya kumwondoa Mwingereza enzi za TANU. Chadema mnajinadi kama makamanda. Siwaelewi kuondoa makamanda mstari wa mbele. Huo uonevu mnaoutaja utaonekanaje bila ninyi kushiriki? Shirikini mwonewe dunia ishuhudie mliovyoonewa ndipo mpate la kusema.

Leo tunaelezwa kuwa hata mgombea wa CCM akishindwa kuna maelekezo kuwa atangazwe kuwa ameshinda. Hizo ni hisia. Simamisheni wagombea, mpate kura asilimia 90 kisha atangazwe mwenye asilimia 10 ndipo muithibitishie dunia hicho mnachosema. Ikiwa mbinu zilizotumika kwenye udiwani tayari mmezibaini, basi panga mkakati mpya wa ushindi. Kuendelea kutoshiriki uchaguzi wakati mkidai mnazuiwa mikutano ya hadhara ni kusaliti upinzani. Ukisusa, wenzio wala! Mungu ibariki Tanzania