Mwezi mmoja wa kampeni, Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) umetamba kuwa utashinda Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba, 25, mwaka huu.
Ukawa wanaowakilishwa na mgombea urais kutoka Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Edward Lowassa, wanasema Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimeaqnza kupoteza matumaini, kiasi kwamba sasa kinampigia debe Lowassa pasipo kujua.
Ukawa wanasema wamenasa siri za CCM wanaoshutumiana kwa kuacha kunadi sera, badala yake kumnadi Lowassa kwenye mikutano yao ya kampeni.
Kwa mfumo huo, Mwenyekiti wa Chadema na mmoja wa wenyeviti weza wa Ukawa, Freeman Mbowe, anasema CCM wameishiwa hoja ndiyo maana kwa sasa hawaishi kuzusha juu ya Lowassa na mkakati wa Chadema pamoja na vyama vinavyounda Ukawa.
Katika mahojiano maalumu na JAMHURI, Mbowe anahoji: “Nini maana ya CCM kuunda timu ya makada 32 kufanya kampeni? Mimi nadhani wanampigia debe mgombea wetu (Lowassa) bila wao kujua.
Anasema kwamba timu hiyo imeshindwa kazi wakati kampeni zinaingia mwezi wa pili kwani wanasita kumpigia debe mgombea Dk. John Magufuli kwa sababu Ukawa imewabana kila eneo ambalo wangeweza kulinadi.
“Kama wajanja watoke kwenye majimbo yao kama sisi waje kwenye kazi waliyotumwa na makada wao… waache majimbo yao, waje kwenye kampeni kama Watanzania watawaelewa,” anasema Mbowe kwa kujiamini.
“CCM wanajua hali ni mbaya. Ndiyo maana unaona wanamchukua Makamba (Yusuph), wanamchukua Rais Kikwete ambaye hayumo kwenye orodha ya wapiga kampeni za Magufuli. Wamewachukua wazee wastaafu -Mzee Warioba (Joseph), Mkapa (Benjamin) na Mzee Ali Hassan Mwinyi.
“Hebu msikilize alivyosema Mheshimiwa Sumaye kwamba mabango ya CCM yamekosa neno CCM na badala yake yameandikwa tu ‘Chagua Magufuli’, wanajua watu kwamba wamewachoka. Safari hii hatuwaachii,” anasema Mbowe na kuongoza:
“Watanzania kwa sasa wanatuelewa, na ndiyo maana wanajitokeza kwa wingi kwenye mikutano kusikiliza sera za mabadiliko. Yote yanayoelezwa na mgombea wetu yanatekelezeka.
“Chadema iko Ukawa, lakini vyama vingine vya upinzani nao wanamzungumzia Lowassa na Chasema tu, ukitaka kujua kwamba wamekosa hoja hawazungumzii hata vyama vingine, unasema wewe chama cha upinzani wakati unampinga mpinzani mwenzako, siasa za ajabu kabisa.”
Kauli ya Mbowe kwamba CCM ina hali mbaya kwenye uchaguzi huu kuanzia ngazi ya udiwani, ubunge na urais, inaungwa mkono na mmoja wa makada wa CCM ambaye amesema: “Lowassa ametuingiza hasara kubwa.
“Unaona hawa wasanii, na hawa makada wengine ambao hawako kwenye orodha. Inabidi kuwalipia kwenda kwenye kampeni ili kuwapata watu kumsikiza mgombea wetu. Inabidi hata wazee nao wakodiwe usafiri na kulipiwa malazi ili kwenda kumpigia debe Magufuli, Lowassa katutia hasara.
“Wakati ule, tulisikia tetesi kwamba Lowassa angetoka CCM, lakini tukapuuza, lakini sasa kwa muda uliobaki, lazima tuongeze nguvu.” Anasema kada huyo kwa masharti ya kutotaja jina lake gazetini.
Lowassa, Waziri Mkuu wa kwanza wa Serikali ya Awamu ya Nne, alijiondoa CCM na kujiunga Chadema, ambayo ilimpa fursa ya kutimiza ndoto yake ya kugombea urais, akiwakilisha vyama vinne vya Chadema, NCCR-Mageuzi, Chama cha Wananchi (CUF) na National League for Democracy (NLD).
Lowassa alijiunga Chadema Julai 28, mwaka huu ambako amekuwa akivuta wafuasi wengi kwenye shughuli za Ukawa, hali inayoashiria uwezekano wa kuwapo kwa upinzani mkubwa kwenye Uchaguzi Mkuu unaotajwa kuwa mgumu kwa pande zote mbili.
Kabla ya kuanza kwa kampeni Agosti 22, mwaka huu, CCM ilitangaza Kamati ya Kampeni yenye wajumbe 32, wengi wao wakiwa ni wale waliowahi kuvaana na Lowassa katika masuala tofauti.
Kamati hiyo iko chini ya Mwenyekiti wake, Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana akisaidiwa na Makamu Wenyeviti wawili ambao ni Rajabu Luhwavi (Bara) na Vuai Ali Vuai (Zanzibar) ambao pia ni manaibu wake kwenye chama.
Pia wamo wale waliotemwa kwenye mbio za urais ndani ya CCM, wajumbe wa Kamati ya Bunge iliyochunguza sakata la Richmond, wajumbe ambao walikuwa kambi ya Lowassa alipokuwa kwenye mbio za urais ndani ya chama hicho, wajumbe ambao ni maarufu kwa kurusha vijembe dhidi ya wapinzani na wajumbe ambao walishaweka bayana uhasimu wao na Lowassa.
Ndani yake wamo January Makamba ambaye pia ni Mbunge wa Bumbuli mkoani Tanga; Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi ya CCM, Abdallah Bulembo; wakati Wajumbe waliotemwa kwenye mbio za urais ni Dk. Asha-Rose Migiro, Samwel Sitta, Mwigulu Nchemba, Dk. Harrison Mwakyembe, Lazaro Nyalandu, Steven Wassira, Bernard Membe, Livingstone Lusinde, na Makongoro Nyerere.
Pia wamo; Nape Nnauye, Christopher ole Sendeka, Sadifa Juma Khamis, Shamsi Vuai Nahodha na Sofia Simba. Vilevile, wamo makada waliowahi kutangaza hadharani kuwa mahasimu wa Lowassa tangu alipokuwa ndani ya CCM, akiwamo Anthony Diallo. Kundi jingine ni la makada vijana kama Ummy Mwalimu, Steven Masele na Pindi Chana.
Mkurugenzi wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Dk. Hellen Kijo-Bisimba, anasema anasema kwamba alitarajia timu hiyo ya CCM kurusha makombora makali kwa upinzani kwa kuwa CCM hawajiamini.
“Watu wanaifahamu CCM, elimu ya uraia watu wameielewa. Wana hoja gani, ukiona hata katika ngazi ya jamii mtu au watu wanamzungumzia mtu ujue umeishiwa sera. Huo ndio mtazamo wangu,” amesema Dk. Kijo-Bisimba.
Kwa upande wake, Lowassa anayewania nafasi ya kuongoza chini ya mwavuli wa vyama vinavyounda Ukawa, amepuuza hoja za makada wa CCM wanaodai kwamba hafai, badala yake amejibu, “Wapuuzeni.”
Lowassa amesema kwamba wanaodai kwamba ana shamba kubwa; na kwamba hulitembea kwa chopa ni waongo, ila amewapa kazi moja tu kuhakikisha kwamba wanajibu matatizo ya umasikini Tanzania wakati nchi ina umri wa nusu karne.
“Naomba kura kwa kila mmoja. Naomba mkaniombee kura ili Oktoba 25, mnipigie kura mimi. Niwahakikishieni sina ardhi kama wanavyodai. Mimi si mwendawazimu hivi, huyo anayesambaza uongozo huo aache au achukue hilo eneo liwe mali yake,” amesema Lowassa.
Wakati huohuo, timu ya kampeni ya mgombea urais kupitia Ukawa imefanya tathimini ya kampeni za mgombea wao, Lowassa na kusema: “Tayari Watanzania wamemwelewa, na atashinda kwa asilimia zaidi ya 70.”
Meneja Kampeni Msaidizi wa Chadema, John Mrema, amezungumza na JAMHURI na kusema chama hicho kina watafiti wa ndani ambao wametoa tathimini ya wiki mbili za kampeni, wakisema Lowassa atashinda kwa kishindo.
Katika mahojiano hayo maalumu, Mrema ambaye yuko kwenye ziara ya Lowassa, anasema tathimini imefanywa katika mikoa ya Dar es Salaam, Iringa, Njombe, Ruvuma, Rukwa, Katavi na Kigoma ambako mgombea wa Chadema ameshapita.
Pia anasema kwamba utafiti huo umejumulisha kampeni zilizofanywa na Mgombea Mwenza, Juma Duni Haji ambaye mbali ya Dar es Salaam ametembelea mikoa ya Lindi, Mtwara na Pwani ambako pia kwa mujibu wa utafiti wao, wamefanya vema.
“Kuna tafiti si ya macho, ni ya kisayansi, inayofanywa na wataalamu wetu, kampeni zinaendelea vizuri na mgombea wetu anakubalika kwa zaidi ya asilimia 70, Lowassa atashinda urais,” anasema Mrema.
Kwa mujibu wa Mrema, tathimini hiyo imemfurahisha hata mgombea mwenyewe, Lowassa, ambaye aliishia kuwajibu kwamba ataunda Serikali ya mchakamchaka.
Mrema amezungumzia hilo ikiwani ni siku chache tangu Jumuiya ya Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM) kutoa tathimini inayosema, Dk. John Magufuli wa CCM anakubalika kwa asilimia 85.
Anasema kwamba jambo hilo linampa faraja mgombea wao, kwani tayari amechangia mawazo akisema, “Watanzania wa 1995 si wa leo,” hivyo CCM ijiande kisaikolojia mara baada ya matokeo ya mgombea urais.
Amesema kwamba Lowassa amewaambia na kutoa maagizo kuwa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) itende haki wakati wa kuhesabu kura na itangaze matokeo sahihi badala ya kupindisha.
“Sisi tuna imani na Tume ya Uchaguzi,” anasema Mrema na kufafanua kuwa Lowassa anafanya kampeni za kistaarabu badala ya kuwatangazia vita kati ya askari na majambazi kwani Tanzania inaheshimu utawala wa sheria.
“Kuua mtu kwa kukusudia ni kinyume cha Ibara ya 14 ya Katiba. Sasa kiongozi anayetaka kuheshimu Katiba lazima apime kauli na utekelezaji wa masuala mbalimbali ya sheria.
“Lowassa hakusema kwamba atamwachia moja kwa moja Babu Seya. Alichosema ataangalia taratibu za kisheria, lakini mpinzani wake ameagiza baadhi ya Watanzania wauwawe.
“Mahakama ni chombo pekee kinachoweza kumtia mtu hatiani kwa kusema huyu ni jambazi na ana adhabu zake kubwa tu, lakini leo Polisi wataua na kusema huyo ni jambazi.
“Watanzania wapime hilo na kuangalia aina ya kiongozi anayejipigia debe kuua. Kuua si jambo la kawaida,” anasema Mrema na kuongeza: “Labda watu wana uelewa mdogo kuhusu sheria na masuala ya utawala bora.”