LowassaUchaguzi Mkuu wa mwaka huu umeiweka nchi katika historia nzuri na mbaya, kutokana na kuimarika kwa vyama vya siasa vya ushindani huku dosari nyingi zilizojitokeza.

Idadi kubwa ya wananchi waliojiandikisha kwenye daftari la kudumu la wapiga kura walijitokeza katika kampeni za vyama vya siasa, kuwasikiliza wagombea waliokuwa wakijinadi na kushiriki katika Uchaguzi Mkuu.

Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, ambaye amefanikiwa kutetea kiti chake katika Jimbo la Hai, mkoani Kilimanjaro, anasema: “CCM haiwezi kunikatisha tamaa, hila na hujuma zao zina mwisho.”

Anasema, ipo siku CCM itaondoka madarakani pamoja na kwamba “ina historia ya kupora ushindi katika kila mwaka Bara na Visiwani. Mwisho wa CCM upo si kwamba utafika.”

Katika jimbo hilo, Mbowe amefanikiwa kutetea kwa kupata kura 51,124 dhidi ya Dastan Mallya wa CCM aliyevuna kura 26,996 huku wagombea wengine, Nuru Mohamed wa ACT-Wazalendo kura 318 na Ndashuka Issack wa APPT-Maendeleo aliyepata 279.

Waliokuwa makada wa CCM na kuamua kujiunga na upinzani wakinadi mabadiliko akiwamo mgombea wa urais wa Chadema kupitia Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA), Waziri Mkuu mstaafu, Edward Lowassa, wamefanikiwa kuibomoa CCM katika ngome zake ambazo hazikuwahi kuchukuliwa na vyama vya upinzani tangu kufanyika kwa Uchaguzi Mkuu wa vyama vingi mwaka 1995 .

Jimbo la Tanga Mjini

Ngome za CCM zilizotwaliwa na wapinzani katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu ni Jimbo la Tanga Mjini lililotwaliwa na Chama cha Wananchi (CUF), ambako mgombea wake, Musa Mbarouk, aliibuka mshindi kwa kupata kura 58,675 dhidi ya Omari Rashid Nundu wa CCM aliyepata kura 57,014.

Pamoja na ushindi huo wa kiti cha ubunge, CUF inatarajia kuongoza Halmashauri ya Jiji la Tanga baada ya kushinda kata 16 kati ya 27 na CCM ikiambulia kata 11 za jimbo hilo.

Mbarouk kabla ya kuchaguliwa kuwa mbunge wa jimbo hilo, alikuwa Diwani wa Kata ya Ngamiani Kusini kwa miaka kumi mfululizo, na kwamba amefanikiwa kupata ushindi huo licha ya upinzani mkali kutoka kwa mpinzani wake wa CCM.

 

Jimbo la Mtwara Mjini

Katika Jimbo hilo, Maftaha Nachuma amefanikiwa kuing’oa CCM kwa kuzoa kura 26,655 dhidi ya kura 24,176 alizopata Husnain Murji aliyekuwa ameshikilia jimbo hilo tangu mwaka 2010, akipokea kijiti kutoka kwa Mohamed Sinani.

 

Jimbo la Tandahimba

Katika Jimbo la Tandahimba, Ahmed Katani wa CUF ameibuka mshindi kwa kura 55,156 dhidi ya mpinzani wake wa CCM, Shaibu Salimu Likumbo, aliyepata kura 41,088. Jimbo hilo lilikuwa likiongozwa na Juma Abdallah Njwayo.

Katani anasema ushindi wake umetokana na kutendeka kwa haki katika uchaguzi mkuu jimboni humo tofauti na Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010.

Anasema licha ya polisi kuonekana kwa wingi katika mikutano yake ya kisiasa, hakuna mtu yeyote aliyekamatwa ama kunyanyaswa na kufanya wananchi wapige kura kwa amani.

 

Jimbo la Ndanda

Mgombea ubunge wa Jimbo la Ndanda kwa tiketi ya Chadema, Cesil Mwambe, ndiye aliyeibuka mshindi kwa kupata kura 26,247 na kumbwaga mgombea wa CCM, Mariam Kasembe, akiambulia kura 26,215 ikiwa ni tofauti ya kura 15.

 

Jimbo la Serengeti 

Jimbo la Serengeti mkoani Mara kwa mara ya kwanza limechukuliwa na upinzani baada ya mgombea wa Chadema, Marwa Chacha, kutangazwa mshindi kwa kupata kura 40,059 dhidi ya kura 39,232 alizopata Dk. Stephen Kebwe wa CCM.

Licha ya kuongoza kiti cha ubunge katika jimbo hilo, pia Chadema inatarajiwa kuongoza Halmashauri ya Serengeti baada ya kushinda kata 18 huku kata 12 zikichukuliwa na CCM.

Hii ni mara ya pili kwa mbunge huyo kuwania nafasi hiyo. Mwaka 2010 aligombea na kuangushwa na Dk. Kebwe huku sababu kubwa ya kushindwa kwake mwaka huo ni chama chake kutoeneza mizizi katika maeneo mengi ya jimboni humo.

Hata hivyo Jimbo la Serengeti limekuwa na historia ya kuongozwa na wabunge kwa kipindi kimoja tu cha miaka mitano. Kabla ya Dk. Kebwe lilikuwa chini ya Dk. James Wanyancha aliyepokea kijiti kutoka kwa Dk. Deogratius Mwita.

 

Jimbo la Kilombero

Katika Jimbo la Kilombero, mgombea ubunge wa Chadema, Peter Lijualikali, ameshinda ubunge kwa kupata kura 62,158 huku mpinzani wake, Abubakar Assenga wa CCM, akiambulia kura 44,092.

Jimbo hilo lilikuwa likishikiliwa na CCM kwa muda mrefu na kabla ya kuchukuliwa na Chadema lilikuwa likiongozwa na Abdul Mteketa ambaye alipokea kijiti kutoka kwa Castor Ligallama.

 

Jimbo la Mlimba

Katika Jimbo jipya la Mlimba, Suzan Kiwanga ameibuka na ushindi baada kuzoa kura 40,068 na kumbwaga mpinzani wake, Godwin Kunambi wa CCM aliyeambulia kura 34,883.

Kiwanga ambaye ni Mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa Morogoro anakuwa mbunge wa kwanza kutoka chama hicho kuongoza jimbo hilo katika mkoa huo. Kiwanga alikuwa mbunge wa viti maalum kupitia Chadema. 

Kufuatia upepo wa kisiasa ambao umevuma kwa kasi kubwa mwaka huu na kuhatarisha anguko la CCM, wachunguzi wa masuala ya kisiasa wanawapongeza wanawake waliojitokeza kuwania nafasi hizo kwa ujasiri na kujiamini badala ya kusubiri uwakilishi wa Viti Maalum.

 

Jimbo la Mikumi

Kwa upande wa Jimbo la Mikumi, mgombea ubunge wa Chadema, Joseph Haule au Profesa Jay kwa jina la kisanii, ameshinda kwa kupata kura 32,259 dhidi ya 30,425 alizopata Jonas Nkya wa CCM.

Mbunge huyo anasema kitendo cha kuchelewesha kwa makusudi matokeo kililenga kupora haki, lakini baada ya msimamo wake na wananchi wa jimbo hilo ameibuka mshindi kwa kumuacha mpinzani wake kwa zaidi ya kura 1,800.

Majimbo haya yaliyotwaliwa na upinzani yametoa funzo kubwa sana kwa chama tawala ambacho kimekuwa na uongozi wa mazoea ambao umekuwa kero na kusababisha upinzani kuchukua nafasi.

Orodha kamili ya wabunge wa upinzani na majimbo yao kwenye mabano ni kama ifuatavyo; James Mbatia (Vunjo) na Zitto Kabwe ambaye sasa ataongoza Jimbo la Kigoma Mjini baada ya kutumikia Jimbo la Kigoma Kaskazini kwa miaka 10 iliyopita akiwa Chadema. Kwa sasa atatumikia kupitia ACT-Wazalendo.

Wabunge wanaotoka Chadema ni Esther Matiko (Tarime Mjini), Pauline Gekul (Babati Mjini), Mwakajoka Frank (Tunduma), James ole Millya (Simanjiro), Joshua Nassari (Arumeru Mashariki), Wilfred Lwakatare (Bukoba Mjini) na Eshter Bulaya (Bunda Mjini).

Wabunge wengine wa Chadema ni Bilango Samson (Buyungu), Mchungaji Peter Msigwa (Iringa Mjini), John Mnyika (Kibamba), Peter Lijualikali (Kilombero), Onesmo ole Nangole (Longido), Joseph Haule (Mikumi), Joseph Mbilinyi (Mbeya Mjini) na Susana Kiwanga (Mlimba).

Pia wamo Julius Kalanga (Monduli), Mgumba Omari (Morogoro Kusini Mashariki), Anthony Komu (Moshi Vijijini), Pascal Haonga (Mbozi), Cesil Mwambe (Ndanda), Joseph Selasini (Rombo), Naghenjwa Kaboyoka (Same Mashariki) David Silinde (Momba) na Tundu Lissu (Singida Mashariki).

Wengine ni Saed Kubenea (Ubungo), Joseph Mkundi (Ukerewe), Waitara Mwita (Ukonga), Gipson ole Meseyeki (Arumeru Magharibi), Marwa Ryoba (Serengeti), Dk Godwin Mollel (Siha), John Heche (Tarime Vijijini), Jaffar Michael (Moshi Mjini) na Willy Qambalo (Karatu).

Kutoka CUF wako Vedasto Edger (Kilwa Kaskazini), Saidi Bungara (Kilwa Kusini), Zubery Kuchauka (Liwale), Hassan Hassan Babali (Mchinga), Abdallah Mtolea (Temeke), Magdalena Sakaya (Kaliua), Maftah Nachuma (Mtwara Mjini), Ahmad Katani (Tandahimba) na Mussa Mbarouk (Tanga Mjini).