TABORA
Na Mwandishi Wetu
Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Freeman Mbowe, amesema kushindwa kwao katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana hakukuchangiwa na aliyekuwa mgombea urais wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. John Magufuli pekee, bali ni pamoja na uzembe walioufanya.
Akizungumza na wajumbe wa kamati za utendaji za Chadema Kanda ya Magharibi, Mbowe anasema hakuna haja ya kumsingizia Magufuli, bali na wao pia wamehusika kwa kutokuwa makini katika mambo ya msingi.
Kanda hiyo inaundwa na mikoa ya Tabora, Kigoma na Katavi.
“Ndiyo maana ninataka kuanzia sasa tujipange na tutakuwa na usajili wa wanachama na kulipia ada kidijitali, kwa sababu tumegundua wenzetu walitupiga kisayansi, hivyo na sisi lazima tujipange,” anasema.
Anayataja maeneo yaliyosababisha kuanguka kwa Chadema na upinzani kwenye uchaguzi huo kuwa ni kutojipanga vizuri, kutokuwa na wagombea wenye sifa na kukubalika, pamoja na kukosa wanachama wapiga kura wenye sifa.
Anasema chama imara na endelevu kinahitaji kuwa na viongozi bora, wagombea bora wanaokubalika, ajenda inayokubalika na kutambulika, bila kusahau kuwa na mpangilio na rasilimali fedha za kujiendesha.
“Ada kwa wanachama wa kawaida itakuwa Sh 2,500 kwa mwaka na atakayehamasisha kuwapata wanachama kujisajili na kulipa ada, atapata Sh 500 kwa kila mwanachama kama kifuta jasho.
“Kutakuwapo kadi za wanachama wa viwango tofauti kama wa kadi za bluu za Sh 10,000 kwa mwaka, rangi ya fedha Sh 25,000 kwa mwaka, za dhahabu Sh 50,000, za platinum Sh 100,000 na za almasi Sh 200,000,” anasema Mbowe na kuongeza kuwa mwanachama anaweza kulipa kwa mwaka mmoja hadi mitano.
Anautaja mfumo huo wa kidijitali kwa jina la ‘Tunasonga Kidijitali’, ukihakikisha wanajipanga upya kutafuta wanachama hai wanaotambulika na kupanua wigo wa mapato na udhibiti wa mapato yenyewe, na kwamba shughuli hiyo imeanzia Tabora.
“Tukisajili wanachama milioni 10 kwa ada ya Sh 2,500 tuna uhakika wa kupata Sh bilioni 250. Kwa Tabora tukisajili asilimia 20 tu ya wapiga kura waliojiandikisha tunapata zaidi ya Sh milioni 91,” anasema.
Anasema kwa sasa Chadema inajipanga kujenga ofisi katika makao makuu ya kanda zote.
Katika hatua nyingine, Mbowe amewataka viongozi wa chama hicho kuwa na uelewa wa kutosha wa kufafanua hoja zinazoibuliwa na uongozi – kama katiba mpya na tume huru ya uchaguzi ili waweze kuzitetea badala ya kuzibeba kama zilivyo, kwa kuwa itakuwa haina maana.
Aidha, amewataka wanaume watambue kuwa wanawake wanaweza na wana msimamo wanaposimamia jambo lao, na kuahidi kuwa makini na kuchunga ulimi wake atakapokutana na Rais Samia Suluhu Hassan kuzungumzia mambo mbalimbali.
Uchaguzi Mkuu ndani ya chama hicho utafanyika mwaka 2023.