Mwanyekiti wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo(CHADEMA) Freeman Mbowe amemwambia Rais Samia kuwa ndani ya serikali na Chama Cha Mapinduzi kuna wahafidhina wanaotamani kukwamisha maridhiano na mchakato wa katiba mpya kuwa hawamtakii mema.
Mbowe ametoa kauli hiyo leo Machi 08,2023 wakati akihutubia kwenye kongamano la Wanawake Duniani lililoandaliwa na Baraza la Wanawake Chadema (BAWACHA) ambapo Rais Samia alihudhuria kama mgeni rasmi Moshi, Kilimanjaro.
“Yawezekana ndani ya Chama na Serikali yako kuna wahafidhina wanaotamani kukwamisha Maridhiano au Mchakato wa kuipata Katiba Mpya ikiwemo Tume Huru ya Uchaguzi kwa kisingizio cha kukilinda Chama Chako. Hawa hawakutakii mema. Nakusihi usikubali dhambi hiyo kwani adhabu yake atoae Mungu wetu hatutamani wala hatuombi imkute yeyote.”Amesema Mbowe.
Amesema wao wataendelea kutekeleza wajibu wao kama wapinzani kuishughulikia serikali na Chama cha Mapinduzi kikamilifu bila hofu wala woga.
Amesema Chadema wako tayari kusamehe na kusahau walikotoka kwa sababu ya Rais Samia ameonyesha roho nyepesi ya wazi na safi ya kubadilisha kule walikotoka.
Aidha Mbowe amelaani kitendo cha wabunge 19 wa Chadema kupelekwa bungeni ikiwa hawakutokana na maamuzi ya ndani ya chama hicho.
“Kitendo cha kupeleka Wabunge 19 ambao hawakutokana na maamuzi yetu ndani ya chama ni uvunjaji wa Katiba, ni uvunjaji wa maadili na kitendo hicho ni uhuni ambao hauwezi kuvumiliwa na mtu yeyote”amesema Mbowe
Mbele ya Rais Samia, Mbowe ameitaka CCM iliombe radhi taifa “kwa kujaza viongozi wasio wa haki na kweli”