Na Lookman Miraji,JamhuriMedia, Dar es Salaam
Shule ya kimataifa ya Al IRSHAAD kwa kushirikiana na wadau nchini wamefanikiwa kuwezesha mbio ambazo zimelenga kuwasaidia watoto wenye mahitaji maalumu.
Mbio hizo zijulikanazo kama Al Irshaad Marathon zimefanyika asubuhi ya jana Septemba 8 katika viwanja vya jeshi vilivyoko masaki, Dar es Salaam.
Mbio hizo zimefanyika mwaka huu ikiwa ni msimu wake wa pili tangu zilipofanyika rasmi kwa mara ya kwanza mwaka Jana.
Katika msimu wa pili wa mbio za Al IRSHAAD zimejumuisha makundi ya watu mbalimbali ikiwemo watoto, vijana pamoja wazee.
Katika hafla ya mbio hizo zilihudhuriwa na wageni kuyoka Jeshi la Polisi Wilaya Kinondoni ambapo mgeni rasmi alikuwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi Kinondoni, Mtatiro Kitinkwi ambapo aliwakilishwa na Mkuu wa Polisi wa Wilaya ya Kipolisi Kinondoni Matilda Kuyeto.
Akizungumza katika hafla ya mbio hizo Afande Kuyeto alianza kwa kutoa pongezi kwa uongozi wa shule za kimataifa za Al IRSHAAD kwa kuandaa mbio hizo ambazo zimewakutanisha wanamichezo zikiwa na lengo kuu la kuhamasisha jamii kutoa huduma na mahitaji kwa watoto wenye mahihitaji maalumu katika jamii.
Mbali pongezi hizo Afande Kuyeto ameelezea juu ya ushiriki wao kama jeshi la polisi katika mbio hizo ni kuunga mkono harakati zinazofanywa na wadau mbalimbali katika jamii kusaidia watoto wenye uhitaji maalum kwani watoto hao pia wana haki za msingi kama watoto wengine kwenye jamii ya kitanzania.
Ambapo kwa kulitambua hilo ametoa rai kwa wanajamii kwa pamoja kushirikiana kuwalinda watoto hao dhidi ya matukio mbalimbali ya unyanyasaji vikiwemo kubakwa na kulawitiwa vitendo ambavyo vinaonekana kushamiri kwa siku za hivi karibuni katika jamii zetu.
Aidha pia Afande Kuyeto ameongeza kwa kutoa wito kwa wazazi wenye watoto wenye mahihitaji maalumu kupata elimu kuhusu afya kwa watoto wakiwa bado wadogo .
Wakati wa hafla hiyo Afande Kuyeto amegusia pia juu ya maadhimisho ya miaka 60 ya Jeshi la Polisi nchini tangu kuanzishwa mwake ambapo kilele cha maadhimisho hayo kinatarajiwa kuwa Septemba 17 mwaka huu.
Katika kuadhimisha shughuli hizo hilo Afande Kuyeto amewasilisha maelekezo waliyopewa wao kama Polisi kutoka kwa Mkuu wa Jeshi la Polisi, Inspecta Jenerali wa polisi Afande Kamilius Wambura ambaye amelielekeza Jeshi la Polisi kushirikiana na jamii katika nyanja mbalimbali za kijamii.
“Tukiwa katika wiki ya maadhimisho ya kilele cha miaka 60 ya Jeshi la Polisi ,Mkuu wa Polisi Inspecta Jenerali Wambura ametuelekeza kushirikiana na jamii katika nyanja mbalimbali za kijamii, hivyo tunaomba wananchi kwa ujumla kuendelea kushirikiana na jeshi la polisi pindi wanapokuja kwao kwaajili ya kushirikiana katika mambo mbalimbali.
Kwani hata uwepo wetu hapa ni sehemu ya utekelezaji wa adhma hii ya dhana ya ushirikishwaji jamii. Polisi ni sehemu ya jamii na jamii ni nyie wananchi na tunawategemea sana katika utoaji wa taarifa ili kuendesha shughuli kwahiyo tunawategemea sana na tunawahitaji sana.” alisema.
Mbali na hotuba hiyo kutoka kwa kwa mgeni rasmi katika mbio hizo waandaji wakuu wa mbio hizo uongozi wa shule za Al IRSHAAD kupitia mwakilishi wake ameelezea kuwa wao kama waratibu wanafurahi kuona mbio hizo zinapiga hatua kadri siku zinavyozidi kwenda ukilinganisha na mara ya kwanza walipoanza.
Akizungumza mara baada ya hafla ya mbio hizo mwakilishi wa shule za Al IRSHAAD Neema Twalib amesema kwamba
“Leo tumefurahi kuona mbio hizi zimepata muitikio wa kutosha pia nasi pia tumefurahi kuona kuwa tunaweza kurudisha mchango wetu kwa jamii kwa kuwasaidia watoto wenye uhitaji maalum ili nao pia wajisikie kuwa wako katika jamii ambayo inawatambua na inawakubali na kuona kuwa wana haki zote kama watoto wengine.
Tumefurahi kuona watu wamehamasika katika msimu huu ukilinganisha na mwaka jana ambapo tuliendesha mbio hizi kwa mara ya kwanza lakini tumeona mabadiliko na tunaamini muitikio utakuwa ni mkubwa zaidi msimu ujao kwani tutaendelea kuhamasisha jamii”
Alimaliza kwa kusema hayo Neema Twalib.
Mbio hizo zimefanyika leo hii ambapo zilihusisha zoezi la utoaji wa zawadi kwa washindi wote walioshiriki mbio hizo kutoka katika unbali tofauti tofauti.