NA MOSHY KIYUNGI
Tabora

Mwimbaji mkongwe wa muziki wa Kilingala na
Kifaransa, Mbilia Bel, amestaafu rasmi muziki
Januari mwaka jana.
Mwana mama huyo mapema Januari 2017,
alitangaza kustaafu kwake wakati
akisherehekea miaka 40 kwenye muziki, pia
siku yake ya kuzaliwa kwa kutimiza miaka 58.
Mbilia mwenye umri wa miaka 59, alianza
kujiingiza kwenye kazi ya muziki akiwa na umri
wa mika 17, akiwa msichana mdogo ambapo
hadi sasa ametimiza miaka 40 tangu aanze
kazi ya uimbaji.
Mwanamuziki huyo alisema kuwa ameachia
albamu yake mpya ya mwisho inayoitwa

‘Signature’, inayohusu maisha yake
yanayoangazia uzuri wake na ubaya.
Amesema kwamba baada ya kuachana na kazi
hiyo ya uimbaji, ataendelea kuwa mshauri wa
wasichana chipukizi wanaowania kuingia katika
tasnia ya muziki hivi sasa.
Mwana mama huyo mashuhuri, yasemekana
kuwa kustaafu kwake kutoka kwenye tasnia ya
muziki kulikuja mwezi mmoja baada ya kuzuka
kwa taarifa kwamba amefariki dunia.
Alipata sifa kubwa katika miaka ya 1970 na
1980 kutokana na sauti yake nyororo.
Umaarufu wake ulipatikana baada ya kujiunga
na mwanamuziki, Tabu Ley Rochereau,
ambaye alikuwa akitunga naye nyimbo na
kuziimba kwa umahiri mkubwa.
Kwa mfano, wimbo wake wa ‘Eswi Yo Wapi’,
unaomaanisha ‘Kwa Nini Umekerwa?’, ukiwa ni
wimbo wa fumbo baada ya kuwa na uhusiano
wa kimapenzi na Rochereau.
Bel aliingia kwenye mahusiano ya kimapenzi na
Tabu Ley na hatimaye walifunga ndoa ya
kifahari ambayo ilifanyika ndani ya ndege.
Katika kipindi cha ndoa yao, Mbilia Bel na Tabu
Ley walifanikiwa kupata mtoto wa kike, Meledoy
Tabu, ambaye pia ni mwanamuziki hivi sasa.

Pamoja na kustaafu kwake, lakini katika ukanda
wa Afrika Mashariki, Mbilia Bel, ataendelea
kukumbukwa hasa kutokana na wimbo wake
wa ‘Nairobi’.

Wasifu wake

Majina yake halisi anaitwa Marie Claire Mbilia
Mboyo (Mbilia Bel), alizaliwa mwaka 1959 jijini
Kinshasa, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
Mwaka 1977, akiwa na umri wa miaka 17
aliacha shule na kujiunga na kundi la
mwanamke muimbaji maarufu wakati huo, Abeti
Masikini, akiwa mcheza ‘show’.
Baada ya miaka minne katika kundi hilo
alijiunga na mwanamuziki, Sam Mangwana,
katika maonyesho mbalimbali nchini Kongo.
Mwishoni mwa mwaka 1981 aliweza kufanyiwa
usaili na Tabu Ley na siku hiyohiyo kuajiriwa
katika kundi la Afrisa International na ndipo
alipopewa jina la Mbilia Bel.
Alikuwa mzuri wa sura, umbo na sauti yake ya
juu ‘soprano’, iliwezesha kundi la Afrisa kuanza
kupata umaarufu mpya.

Wimbo wake wa kwanza ‘Mpeye Ya Longo’
ambao tafsiri yake ni ‘Roho Mtakatifu’
uliorekodiwa mwaka 1982 ulikuwa ukieleza
kuhusu shida anazopata mwanamke
aliyeachwa katika ndoa na ulipendwa sana na
wanawake wa Kongo wakati huo.
Wimbo huo uliotungwa na Tabu Ley ulipendwa
zaidi, ulikuwa unaelezea matatizo ya
mwanamke na ulikuwa unaimbwa na
mwanamke.
Hatimaye wimbo huo ulishinda tuzo ya wimbo
bora nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo
(zamani Zaire) mwaka 1983, pia Mbilia
akashinda tuzo ya msanii mpya bora.
Katika kipindi hicho tasnia ya muziki wa Kongo
ilikuwa ikitawaliwa na wanaume watupu, kwa
hiyo wimbo huo ulikuwa ufunguo kwa waimbaji
wa kike wa Kongo na hatimaye hata waimbaji
wa kike hapa kwetu Tanzania.
Wimbo mwingine maarufu sana nchini ni
‘Yamba Ngaa’, unaomaanisha ‘Nipokee
Mpenzi.’ Ulitungwa na Tabu Ley na kuimbwa na
Mbilia Bel kwa sauti nyororo.
Kibao kilichofuata kilikuwa ni ‘Eswi Yo Wapi’
(Uliumizwa Wapi?), huu ulikuwa wimbo ambao

Mbilia na Tabu Ley walitunga kwa pamoja nao
ukawa maarufu sana.
Kutokana na kuwepo kwa Mbilia, umaarufu wa
Afrisa uliendelea kukua na kuanza kuvunja
ngome kongwe ya TP OK Jazz katika mauzo
na umaarufu.
Maonyesho ya bendi ya Afrisa yalijaza sana na
kivutio kikubwa kilikuwa Mbilia ambaye alikuwa
anajua kulitawala jukwaa na mara nyingi
alijiunga na wanenguaji wa Afrisa walioitwa
Rocherreautes kutokana na jina la Tabu Ley
Rochereau.
Kwa pamoja walikuwa wakicheza vizuri, kazi
ambayo ndiyo aliyoanzia katika ulimwengu wa
muziki.
Kama kawaida, umaarufu una matatizo yake,
kufikia mwaka 1986 uhusiano kati ya Tabu Ley
na Mbilia ukaanza kuingia nyongo, ukaibuka
uvumi kuwa Mbilia alitaka kujitoa maisha baada
ya onyesho kubwa sana Kinshasa lilioitwa
Music-Media ‘86.’
Utata ukazidi baada ya Tabu Ley alipoongeza
idadi ya wanawake katika bendi yake, hasa ujio
wa Kishila Ngoyi, ambaye alipewa jina la kisanii
la Faya Tess.

Pamoja na minong’ono hiyo, wasanii wote
wawili walikataa katakata kuwa kulikuwa na
tatizo baina yao.
Baada ya kuingia kwa Faya Tess, Afrisa ilifanya
safari ya maonyesho Afrika Mashariki ambayo
matokeo yake ndiyo nyimbo kama ‘Nadina’,
ambapo wimbo huo uliimbwa kwa Kiswahili na
Kilingala.
Hatimaye Mbilia Bel aliiacha Afrisa mwishoni
mwa mwaka 1987 na kuwa mwanamuziki wa
kujitegemea.
Baada ya kuvunjika kwa uhusiano wake na
Tabu Ley, Mbilia Bel aliunda bendi yake
mwenyewe na kuimba nyimbo nyingi kama
‘Manzili Manzili’ kwa lugha yao ya Kinyansi,
kutoka Jimbo la Bandundu, kusini magharibi
mwa DRC.
Baadaye alielekea Paris, Ufaransa alikojiunga
na mpiga gitaa, Rigo Starr Bamundele.
Huko alitengeneza albamu yake ya kwanza
iliyoitwa ‘Phénomène’, ambayo ilipata umaarufu
mkubwa nchini DRC na hata nje ya Kongo.
Lakini kazi zake zilizofuata hazikufikia umaarufu
ule na kwenye bendi aliyoihama ya Afrisa, pia
kukawa na matatizo kwani Tabu Ley naye
alionekana kuishiwa ari ya kutunga vibao vipya

na kusababisha kuwa mwisho wa Afrisa
International.
Mbilia Bel alikwenda nchini Kenya kutumbuiza,
akitokea Kongo Brazzaville. Alikuwa nchini
humo kwa mwaliko wa Pamela Olet wa
Kampuni ya Melamani Productions.
Lengo kubwa la ziara yake ya wiki mbili nchini
humo ilikuwa ni kueneza amani na
kuwatumbuiza mashabiki wake kwa nyimbo
zake zilizotia fora kama vile ‘Nakei Nairobi’
,
‘Eswi Yo Wapi’ na ‘Nadina’ alizoimba na
marehemu Tabu Ley aliyekuwa kiongozi wa
Afrisa International.
Mbilia mara baada ya kuwasili alisema
amefurahi kurudi jijini Nairobi baada ya miaka
16.
“Nawapenda sana mashabiki wangu wa Kenya
kwa sababu wananionyesha upendo na
wanafurahia nyimbo zangu,” alisema Mbilia
Bel.
Aidha, katika ziara yake hiyo alikwenda kuzuru
wafungwa wa jela ya wanawake ya Lang’ata
mjini Nairobi.
Hakusita kumsifia marehemu Tabu Ley kwa
kukuza kipaji chake akiwa mnenguaji,
akapanda ngazi na akawa mwimbaji.

Mwandishi wa makala hii anapatikana kwa
namba: 0784331200, 0767331200 na
0713331200

Mwisho