Hatimaye mkutano mkuu wa Chama Cha NCCR-Mageuzi umemfukuza uanachama mwenyekiti wa chama hicho Taifa, James Mbatia na pamoja na kumvua uongozi Makamu Mwenyekiti wa Chama hicho Angelina Rutairwa.
Mkutano huo unafanyika leo Jumamosi Septemba 24, 2022 jijini Dodoma na umehudhuriwa na wajumbe 224 kati ya 368 waliopo kwa mujibu wa Katiba ya chama chao.
Kaimu Mwenyekiti wa chama hicho, Haji Ambari Hassan kutaja amesema kuwa Mbatia anatuhuma saba zinazomkabili ambapo mbili zinamkabili Angelina.
Ambari amesema kuwa miongoni mwa tuhuma ambazo Mbatia anatuhumiwa nazo ni kuuza mali za chama,ikiwemo mashamba na nyumba katika maeneo mbalimbali.
Ambari amewaambia wajumbe hao kuwa viongozi hao walipelekewa hati ya mashtaka yao na walitakiwa kujibu ndani ya siku 14 kama katiba yao inavyotaka.
Aidha, mkutano huo ulitaka viongozi wote waliohusika na ubadhilifu wa mali akiwemo Mbatia kuchukuliwa hatua za kisheria.
Hata hivyo, amesema kuwa hakujibu mshtaka hayo na wala hakufika katika mkutano huo licha ya kualikwa ili aweze kujitetea mbele ya wajumbe badala yake walikimbilia mahakamani kuzuia kwa mara nyingine mkutano huo.
Mwenyekiti wa Baraza la Wadhamini ya chama hicho Joseph Selasini amesema halmashauri kuu ya chama hicho imewatimua uanachama wanachama 10 kwa utovu wa nidhamu uliokidhiri akiwemo Edward Simbeye.