Na Mwandish Wetu, JamhuriMedia, Mbeya

Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linamshikilia Anna Mwakilima (24), mkazi wa Mbuyuni, Wilaya ya Mbarali kwa tuhuma za wizi wa mtoto mwenye umri wa miezi miwili na nusu (jina la mtoto tunalihifadhi).

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Kamishna Msaidizi wa Polisi (SACP) Benjamin Kuzaga Kuzaga alisema kuwa Desemba 22, mwaka huu, Aneth Mgaya (20), mkazi wa kijiji cha Mwakaganga, wilayani Mbarali, aliibiwa mtoto wake mwenye umri wa miezi miwili na nusu na mwanamke ambaye alimfahamu kwa sura.

Alisema siku moja kabla ya tukio, majira ya saa 10 jioni, mtuhumiwa alifika nyumbani kwa Aneth na kuomba hifadhi ya kulala kwa madai kuwa alitokea mjini Mbeya na alikuwa anaishi kwa muda Ubaruku, Mbarali kwa ajili ya biashara ya vitenge.

Alieleza kuwa siku iliyofuata Desemba 22, 2024, saa moja asubuhi, Aneth aliamka na kutoka nyumbani kwake kwenda kununua vitafunwa eneo la jirani, huku akimwacha mtuhumiwa na watoto wawili. Baada ya kurejea nyumbani, hakumkuta mtuhumiwa wala watoto wake.

Kamanda Kuzaga alisema Aneth alitoa taarifa katika kituo cha Polisi na ufuatiliaji ulifanyika na kufanikiwa kumkamata mtuhumiwa huyo.

Alisema kuwa juzi saa 12 jioni, katika kijiji cha Mbuyuni, kata ya Mapogoro, wilayani Mbarali, Polisi walifanikiwa kumkamata mtuhumiwa Anna Mwakilima akiwa na mtoto huyo ambaye hajamdhuru.