Na Fredy Mgunda,JamhuriMedia, Iringa
JESHI la Polisi Mkoa wa Iringa kwa kushirikiana na Askari wa Uhifadhi kutoka hifadhi ya Taifa Ruaha wanamshikilia Cyprian Kasula miaka 42, mkulima na mkazi wa kijiji cha Kipera kwa tuhuma za kukutwa na kichwa cha Tembo kikiwa na meno yote mawili katika Hifadhi ya Taifa ya Ruaha.
Akizungumza na waandishi wa habari Iringa, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Iringa ACP Allan Bukumbi amesema kuwa wanamshikilia Cyprian Kasula miaka 42, mkulima na mkazi wa kijiji cha Kipera akiwa na kichwa cha Tembo kikiwa na meno yake mawili,Nyama ya Tembo,Mkia wa Tembo,Silaha tatu za kienyeji aina ya Gobore,Vipande vya nondo 35,makopo matatu ya unga wa baruti na Panga moja.
ACP Bukumbi amesema kuwa mtuhumiwa huyo alikutwa amekaa porini chini ya mti pamoja na mwenzake mmoja ambaye alifanikiwa kukimbia baada ya kuona askari wamefika eneo hilo na juhudi za kumtafuta zinaendelea.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Iringa amesema kuwa Agnes Chaula miaka 38, mama lishe na mkazi wa Mwangata D kwa tuhuma za kukutwa na vipande vitano vya meno ya Tembo.
ACP Bukumbi amesema kuwa mama lishe huyo anatuhumiwa kujihusisha na uwindaji haramu na taratibu za kumfikisha mahakamani zinaendelea.
Amesema kuwa Jeshi la Polisi Mkoa wa Iringa linamshikilia Christina Mponzi, miaka 34, mkulima na mkazi wa Kihesa akiwa na Madawa ya kulevya yanayodhaniwa kuwa ni Heroine kete 33, mtuhumiwa alikutwa ameweka kete hizo kwenye mkoba baada ya kufanyiwa upekuzi aligundulika kuwa na hayo na anashikiliwa kwa ajili ya upelelezi zaidi na kielelezo kimehifadhiwa kituoni.