Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Ngerengere
WATU watatu wamekamatwa na vipande 396 vya nondo za ukubwa wa milimita 16 zilizokuwa awali zimejengea uzio kuzuia kukatiza wanyama waharibifu akiwemo tembo katika Mradi wa ujenzi wa Reli ya Kisasa ya Standard Gauge (SGR)
Kamanda wa Kikosi cha Polisi Reli Tanzania, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP), Sebastian Mbuta, amesema kuwa kuna uharibifu wa miundombinu ya reli ya kisasa ya Standard Gauge (SGR) uliofanywa katika eneo la Ngerengere mkoani Morogoro na Dodoma.
Kamanda amesema kuwa miundombinu hiyo iliyoharibiwa ilikuwa isaidie treni iunganishwe na umeme pindi itakapoanza safari.
“Eneo hilo limenyofolewa na kuacha uwazi mkubwa ambako kumeondolewa vifaa hivyo ikilinganishwa na maeneo mengine yenye nondo ambako kuna mpangilio mzuri,” amesema.
Kamanda amesema kuwa watuhumiwa wametumia maji kuyeyusha ardhi na kuwarahisishia kung’oa nondo na kuacha mashimo.
Kamanda Mbuta, amefika eneo la tukio na kujionea uharibifu huo, sambamba na kufika kituo cha Polisi Ngerengere kushuhudia nondo zilizokamatwa.
ACP Mbuta amesema katika eneo la Ngerengere, tayari wamewatia mbaroni Florah Mbago (39), mkazi wa Kiburumo Ngerengere na Juma Kijiti KItu (66), mkazi wa Mgudeni Ngerengereaa waliokutwa na vipande 17 vya nondo za ukubwa wa milimita 16, mali ya kampuni ya nchini Afrika Kusini ya Rubis, waliopewa kandarasi ya kujenga kilometa 16 za uzio huo wa kuzuia wanyamapori kuvuka upande mmoja kwenda mwingine na kuharibu reli.
Akabainisha mtuhumiwa mwingine Living Emmanuel, (20) ambaye ni fundi wa kujenga uzio na mkazi wa Chamwino Ngerengere, yeye alikamatwa akiwa na vipande vya nondo vilivyokatwa 379, na upelelezi wa mashauri hayo unakamilishwa kwa haraka ili watuhumiwa wafikishwe mahakamani.
Kamanda ameongeza kuwa wamefanya jitihada mbalimbali kuzuia uhalifu katika njia ya reli kwa kushirikisha jamii kupitia mikutano mbalimbali ikiwemo ya ana kwa ana na kupitia vyombo vya habari, na kuahidi kuendelea kushirikiana na wananchi wanaotoa taarifa katika mapambano ya kuzuia vitendo vya uhalifu katika maeneo ya Reli.
Amesema katika kipindi cha mwaka jana pekee, jumla ya watuhumiwa 97 walikamatwa kwa kufanya uhalifu kwenye maeneo ya reli, na watuhumiwa hao wamefikishwa mahakamani na wengi tayari wamehukumiwa, hivyo kutoa wito kwa wananchi kuendelea kutoa taarifa ya vitendo vya kiuhalifuili kuhakikisha mali za Shirika la Reli na miundombinu yake inakuwa salama.
“Adhabu wanazopewa si ndogo, wengine wanafungwa hadi miaka 20, si adhabu ndogo, na ndio maana tukiwakamata tunawafikisha mahakamani kwa mujibu wa sheria, na wapo wengine huwa tunawapeleka kwa makossa ya uhujumu uchumi, reli hii ikianza kazi kila Mtanzania atafaidika na reli hii ya kisasa.
‘Nizidi kuwaomba wananchi waguswe kwa dhati kutoka moyoni kuwa hii reli ni ya kwetu, na yeyote atakayeona hujuma zozote kwenye miundombinu ya reli atoe taarifa kwa vyombo vya dola ama viomgozi kwenye maeneo yao” amesisitiza Kamanda Mbuta.
Kamanda amesema kuwa pia katika Mkoa wa Dodoma amekamatwa mtu mmoja Elia Elias, (24), maeneo ya Makulu akiharibu miundombinu ya reli kwa kubomoa nguzo nane za uzio wa SGR kwa kuzivunja kwa kutumia nyundo kubwa na kuchukua nondo zilizomo ndani yake kwa ajili ya kwenda kuziuza kama vyuma chakavu.
Kwa upande wake Meneja mradi wa ujenzi wa uzio huo wa kuzuia wanyamapori waharibifu wakiwemo tembo kwenye SGR kipande cha Ngerengere, Petter de Lange kutoka kampuni ya Rubis ya nchini Afrika ya kusini, amesikitishwa na kitendo kinachofanywa na baadhi ya Watanzania kuhujumu mali yao wenyewe, kwani reli hiyo kwani ikikamilika, italeta manufaa ya kiuchumi kwa Watanzania wote.
Amesema reli hiyo ni mahususi kuzuia mapito ya wanyamapori,eneo la Kidugalo, baada ya kufanya utafiti na kubaini eneo hilo ni mapito ya wanyamapori wakiwemo Tembo, na nia mahususi ni kulinda reli hiyo isipate madhara yeyote ikiwemo ajali kwa kugongana na mnyama kama Tembo na wengine.
Makosa mbalimbali ambayo watuhumiwa walikamatwa ndani ya himaya ya Reli na wengine walifikishwa mahakamani katika kupindi cha mwaka jana na mwaka juzi.
Kwa mujibu wa ACP Mbuta, ni pamoja na wizi wa vyuma vya reli aina ya sahani (Sole Plate), chuma aina ya Coprini, vipande vya nondo milimita nane na 16, kukamatwa na dawa za kulevya ikiwemo bangi na mirungi, mabomba ya urefu wa futi kumi ya kujengea madaraja ya reli,mabomba ya maji, mipira ya kusambaza maji, mifuko ya mbolea kwa ajili ya vilipuzi, wizi pamoja na uharibifu wa miundombinu.
Mwandishi wa habari hizi alifika eneo la Ngerengere na kushuhudia nondo zilizowekwa katika uzio wa kuzuia wanyama zikiharibiwa.