KAGERA: Waziri wa uchukuzi Profesa ,Makame Mbarawa amemtaka mkandarasi anayetekekeza mradi wa upanuzi wa bandari za Kemondo na Bukoba zilizopo wilayani Bukoba mkoani Kagera kuongeza Kasi ya ujenzi wa mradi huo ili kufikia mwezi Mei mwakani.
Profesa Mbarawa aliongozana na viongozi mbalimbali kutoka mamlaka ya Bandari Tanzania TPA wakati wa ziara yake mkoani Kagera alipofika kukagua upanuzi wa bandari za Bukoba na Kemondo zinazogharimu Sh bilioni 40.
Amesema kuwa amefurahia kuona ujenzi unaendelea kwa kasi ambapo ujenzi wa gati moja kwa kila bandari unapaswa kukamilika kwa wakati na haraka sana ifikapo Mei ili kuruhusu meli ya Mv Mwanza kutia nanga pindi itakapokamilika.
Amesema kuwa licha ya kuwa mkataba unaonesha mradi huo kukamilika mwezi julai mwaka 2024 ipo sababu ya mradi huo kukamilika mwezi Mei ili meli mpya ya Mv Mwanza inapokamilika iweze kuwa na eneo lake la kutia nanga.
“Serikali haina tatizo la fedha naomba usimamizi ufanyike kwa weledi na kazi ifanyike kwa bidii ili meli tu inapomalizika ya Mv Mwanza na ujenzi wa gati uwe umemalizika kwa weledi wa Mamlaka ya Bandari na TPA naamini litafanyika na tayari tushaongea na wataalamu wote wanaohusika na jambo hilo.
Kaimu Mkurugenzi kutoka Mamlaka ya Bandari nchini Mhandisi ,Juma Kijavara alisema kuwa kwa Sasa ujenzi huo unaendelea vizuri na mkandarasi yuko tayari kufanya kazi usiku na mchana ili kuwezesha mradi huo kukamilika kwa wakati .