Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akizungumza na wananchi wa eneo Kapunga, Wilaya ya Mbalali Mkoani Mbeya ambapo aliwaeleza wananchi hao maamuzi ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kufanya marekebisho kwenye tangazo la Serikali namba 28 ambalo limetoa hekta 74,000 kwa wananchi kwa ajili ya shughuli za kilimo na ufugaji endelevu. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

Na Mwandishi Wetu,JamhuriMedia

Wananchi wa Wilaya ya Mbarali mkoani Mbeya wameipongeza Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kumaliza mgogoro wa ardhi uliodumu kwa miaka 15 na hivyo kuwawezesha kuendelea kufanya shughuli zao za ufugaji na kilimo kwa uhuru na amani.

Wamesema kumalizika kwa mgogoro huo ambao ulihusisha wakazi wa wilaya hiyo wanaoendesha shughuli za ufugaji na kilimo katika eneo la Bonde la Usangu dhidi ya hifadhi ya Taifa ya Ruaha.

Pongezi hizo zimetolewa baada ya Waziri Mkuu Kassim Majaliwa kuwatangazia wananchi hao kuwa Serikali imefanya maboresho makubwa kwenye Tangazo la Serikali namba 28 na kuliacha nje ya mpaka wa hifadhi eneo lenye ukubwa wa zaidi ya hekta 74,000 kwa ajili ya kuwawezesha wananchi hao kufanya shughuli za kilimo na ufugaji. Mkutano huo umefanyika kijijini Kapunga.

“Tunamshukuru mama yetu, Mheshimiwa Rais Samia kwa uamuzi mkubwa alioufanya wa kuboresha GN 28, sasa tutalima kwa uhuru na tutaongeza uzalishaji kwa sababu awali tulikuwa tunalima kwa wasiwasi,” alisema Elibauti Mwinuka mkulima katika kata ya Itamboleo wilayani Mbarali.

Muonekano wa baadhi ya maeneo ambayo Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ameamua kutoa kwa wananchi kwa ajili ya shughuli za kilimo na ufugaji endelevu. Rais Dkt. Samia ameridhia kufanya marekebisho kwenye tangazo la Serikali namba 28 ambalo limetoa hekta 74,000 kwa ajili ya wananchi. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu

Kwa upande wake,Anle Kifute ambaye ni mkulima katika kijiji cha Kapunga amesema amefurahishwa na kauli ya Serikali ambayo inakwenda kuwaondolea migogoro katika maeneo yao na hivyo wataweza kuendesha shughuli zao bila ya usumbufu wa aina yoyote.

Naye,Mwenekiti wa Wafugaji katika ranchi ya Matebele-Madunguru, Lokordu Siloma amesema amefarijika kwa uamuzi huo wa Serikali pamoja na elimu ya ufugaji wa kisasa na wenye tija waliyopatiwa ambayo inakwenda kuongeza mnyororo wa thamani.

Kadhalika alimshukuru Mheshimiwa Rais Samia kwa kusikiliza kero zao na kuzipatia ufumbuzi na sasa wanakwenda kufuga kwa uhuru na kwa kuzingatia maelekezo yaliyotolewa. 

“Awali watu wenye uwezo walikuwa wanavamia maeneo ya ranchi na kuendesha shughuli za kilimo lakini kwa kauli hii wafugaji tutaachiwa ranchi zetu tulishe mifugo yetu. Tunaishukuru sana Serikali.” alisema.

Kwa upande wake,Majaliwa baada ya kutangaza maamuzi hayo ya Serikali, amewataka Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Zuberi Homera na Mkuu wa Wilaya ya Mbarali, Reuben Mfune wahakikishe wanasimamia vizuri sheria pamoja na kuendelea kutoa elimu kuhusu umuhimu wa uhifadhi na utunzaji wa vyanzo vya maji.

Pia, Waziri Mkuu alimuagiza Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mashimba Ndaki pamoja na viongozi wa Ranchi ya Usangu waende kwenye eneo hilo na kuwapanga upya wafugaji ili manufaa ya ufugaji yaonekane ikiwemo uanzishwaji wa viwanda vya kuchakata mazao ya mifugo.

Alisema Serikali imefanya maboresho hayo kwa lengo la kuwawezesha wakulima na wafugaji wilayani humo kuendesha shughuli kitaalamu na kuwaongezea tija.

“Marekebisho ya tangazo hilo yatawezesha baadhi ya vitongoji vilivyokuwa vimetangazwa awali kuwa ndani ya hifadhi kuachwa nje ya mipaka na kutumiwa na wananchi kwa ajili ya shughuli za kilimo na ufugaji” alisema.

Naye, Waziri wa Maji Jumaa Aweso alisema awali walishindwa kutekeleza mradi wa maji katika kijiji cha Kapunga wenye thamani ya shilingi bilioni 3.5 ambao kwa sababu walikuwa hawajui hatma ya wananchi hao kama wataendelea kubaki au wataondoka, hivyo baada ya kauli ya Serikali iliyotolewa leo amemuagiza Mhandisi wa Maji wa wilaya hiyo kuanza utekelezaji wa mradi huo.