Machi 21 na 22 mwaka huu, Rais Barack Obama wa Marekani alifanya ziara ya kihistoria nchini Cuba. Ya kihistoria kwa sababu hii ilikuwa ziara ya kwanza ya Rais wa Marekani nchini Cuba tangu miaka 88 iliyopita. Mara ya mwisho ilikuwa mwaka 1928 wakati rais wa Marekani alipozuru nchi hiyo.
Ziara hii ya Obama inatokana na tangazo lake la Desemba 2014 kuwa anakusudia kuanzisha uhusiano wa kidiplomasia na Cuba. Baada ya hapo Obama alikutana ana kwa ana na Rais Raul Castro wa Cuba wakati wa mkutano wa marais wa nchi za Amerika uliofanyika nchini Panama mnamo Aprili 2015.
Na mwezi uliofuata Marekani ikaiondoa Cuba kutoka orodha ya kile inachokiita “nchi za kigaidi”. Kisha Cuba ikafungua ubalozi wake nchini Marekani mwezi Julai 2015 na mwezi uliofuata ikafungua ubalozi wake katika Mji Mkuu wa Cuba (Havana)
Huu ndio mchakato uliomfanya Rais Obama kuizuru Cuba hivi majuzi na kusema anataka kufungua ukurasa mpya wa kirafiki badala ya kuendelea na vita baridi. Akasema anataka kumaliza uhasama uliokuwapo tangu Mapinduzi ya Januari Mosi, 1959 na kuanza uhusiano mpya baina ya Marekani na Cuba.
Rais Obama alichukua muda wa dakika 38 akizungumza na baadhi ya raia wa Cuba. Alitumia muda mrefu akijaribu kuwaelimisha maana ya demokrasia na haki za binadamu kama “inavyotekelezwa” nchini Marekani.
Alisahau kuwa nchini Marekani theluthi moja ya watoto wanaishi maisha ya ufukara, kuwa jumla ya raia milioni 48 wanaishi na njaa; kuwa miongoni mwa nchi ‘tajiri’ duniani Marekani inashika nafasi ya mwisho katika utoaji wa elimu kwa watoto.
Ni kwa sababu asilimia 95 ya mapato yote nchini yanaingia mifukoni mwa matajiri ambao idadi yao ni asilimia moja tu ya raia wote.
Akasema nchini Marekani kila raia ana haki ya kutoa mawazo yake na kuikosoa serikali. Alisahau kuwa kuna raia kama Edward Snowden ambaye yuko mafichoni na Chelsea Manning tayari amehukumiwa kifungo, kwa sababu wamefichua uhalifu wa kivita na ujasusi unaofanywa duniani na utawala wa Marekani.
Rais Obama pia alitoa somo kuhusu umuhimu wa kufuata sheria ili mtu asipoteze uhuru wake bila ya kuhukumiwa mahakamani. Alisahau kuwa serikali yake imeyakalia kimabavu maeneo ya Guantanamo ambayo ni mali ya Cuba. Siyo tu inakataa kuirudisha, bali inatumia maeneo hayo kama gereza la kuwafungia mamia ya watu wasiofikishwa mahakamani wala kufunguliwa mashitaka. Alipochaguliwa aliahidi kuwa atawaachia, lakini hajatimiza ahadi hiyo.
Raul Castro naye akakumbusha kuwa haki za binadamu na demokrasia si kupiga kura tu kila baada ya miaka minne (kumchaua Trump au Clinton), bali ni pamoja na haki ya kijamii, kiuchumi, kitamaduni, ya kufanya kazi, ya matibabu, elimu, hifadhi ya jamii, kutokubaguliwa, na kadhalika. Akasema nchini Cuba uhalifu mkubwa wa haki za binadamu unafanywa na Marekani huko Guantanamo.
Gereza hili katika ardhi ya Cuba limekuwapo kwa muda wa miaka 15. Tayari wafungwa tisa wamekufa na wengine wengi wamegoma kula. Mwaka 2008 Rais Obama alipokuwa akigombea urais aliahidi kuwa atalifunga gereza hilo kwa vile “linaiaibisha Marekani ulimwenguni”. Sasa anasema hawezi kulifunga kwa sababu Bunge lake (Congress) linakataa na linataka wafungwa waendelee kuteswa gerezani bila ya kufuata taratibu za kisheria na kikatiba. Hiyo ni Marekani inayotaka kuifundisha Cuba maana ya haki za binadamu!
Wakati Rais Obama alipokuwa akifundisha somo la demokrasia na haki za binadamu, waandishi walioambatana naye walimuuliza Rais Raul Castro kwanini anaendelea kuwaweka ndani “wafungwa wa kisiasa”. Mara moja Castro akajibu: “Nipe majina ya hao wafungwa nami nitawaachilia leo hii.”
Labda hao waandishi walikuwa hawajasoma ripoti ya asasi ya kimataifa ya haki za binadamu (Amnesty International) ambayo ilisema kuwa Cuba haina mfungwa wa kisiasa. Wa mwisho alifunguliwa Septemba, mwaka jana.
Pengine waandishi wangeelekeza swali lao kwa Rais Obama. Kwani nchini Marekani kuna wafungwa wa kisiasa. Kwa mfano, tovuti ya Jerico Movement ina picha na maelezo ya wafungwa hao zaidi ya 50.
Maarufu kati yao ni Mumia Abu Jamal ambaye anaugua ugonjwa wa manjano (Hepatitis C), lakini gereza linakataa kumpa matibabu, hivyo huenda akafa gerezani. Mwingine ni aliyekuwa akiitwa Rap Brown, ambaye sasa anajiita Imam Jamil Al-Amin. Hawa wamewekwa ndani kwa sababu za kisiasa.
Rais Obama aliwataka wananchi wa Cuba wasahau jinsi nchi yao ilivyokuwa ikishambuliwa na Marekani tangu Mapinduzi ya mwaka 1959. Shirika la Kijasusi la Marekani (CIA) lilifanya majaribio kadha ya kuiangusha serikali ya Cuba na kumuua Rais Fidel Castro (wakati ule) na wenzake. Jaribio kubwa ni lile la “ghuba ya nguruwe” (Bay of Pigs) mnamo mwaka 1961 wakati wananchi wengi wa Cuba waliuawa wakiilinda nchi yao.
Rais Obama alitaka Wacuba wasahau kuwa mwaka 1976 ndege yao ya abiria (Cubana de Aviación) iliripuliwa kutoka angani na abiria 78 wa kimataifa walikufa. Magaidi waliotenda uharamia huo walipewa hifadhi nchini Marekani . Anataka wasahau kuwa CIA walitega mabomu katika mighahawa na hoteli nchini Cuba miaka ya 1990.
Anataka Wacuba wasahau kuwa tangu mwaka 1960 Marekani imeiwekea Cuba vikwazo kamili. Wakati huo waraka kutoka Ikulu ya Marekani ilisema lengo ni kuizuia Cuba kufanya biashara na nchi za nje ili wananchi wake wateseke na njaa na ukosefu wa mahitaji ya lazima kama dawa na vipuli. Waraka ulisema “wananchi hao watakapobanwa na njaa ndipo watalazimika kuipindua serikali yao”.
Mbinu zote hizo ziligonga mwamba. Leo Rais Obama anasema tusahau yaliyopita wakati vikwazo vingali vinaendelea.
Na mbinu zao ziligonga mwamba kwa sababu Cuba inatoa matibabu kwa raia wote bila ya malipo. Cuba inaongoza katika uwiano wa madaktari na wananchi, yaani kwa kila raia 1,000 kuna madaktari 6.7. Ni nchi chache duniani zinaweza kuwa takwimu za aina hii.
Jarida mashuhuri la matibabu duniani (Lancet Journal) linasema kama mafanikio ya Cuba yangeigwa na nchi zinazoendelea, basi afya ya watu duniani ingefikia kiwango cha juu. Kwa mfano, Cuba imevumbua dawa inayotibu saratani. Wana dawa za aina nyingi ambazo zinaweza kuuzwa nchini Marekani kama kusingekuwa na vikwazo.
Cuba pia inatoa elimu bila ya malipo hadi ngazi ya chuo kikuu. Inaongoza duniani kwa kiwango cha bajeti kinachoelekezwa katika sekta ya elimu. Ina vyuo vikuu 22 vinavyofundisha madaktari. Kabla ya mapinduzi ya mwaka 1959 vilikuwapo vitatu tu.
Nchini Cuba wanawake wanawazidi wanaume katika idadi ya majaji, mawakili, wanasayansi, wanateknolojia na kadhalika. Asilimia 48 ya wabunge ni wanawake. Pia wanawake wanapewa likizo ya miezi tisa wanapojifungua, wakilipwa mshahara kamili. Baada ya hapo miezi mitatu hulipwa robo tatu ya mshahara.
Kwa mujibu wa shirika la afya duniani (WHO) nchini Cuba umri wa wastani wa kuishi kwa wanawake ni miaka 80 na kwa wanaume ni miaka 77.
Si ajabu Rais mstaafu wa Cuba, Fidel Castro, aliandika makala akisema: “Tunamshukuru Ndugu Obama kwa kututembelea, lakini Cuba ni nchi inayojitegemea – hatuhitaji sadaka kutoka ubeberu”.
Je, sisi Watanzania tunathubutu kusema hayo? Au tutaendelea tu na matangazo ya redio kuhusu malaria yanayoletwa kwa “hisani ya Marekani?” Hata matangazo ya redio pia mpaka tufadhiliwe?