Na Tatu Mohamed, JamhuriMedia, Dar es Salaam

WAZIRI wa Afya Zanzibar, Nassor Mazrui amezindua Zanzibar Afya Week 2025 ambapo amesema itakuwa hatua muhimu ya mageuzi katika sekta yetu ya afya na itaendelea kudhihirisha dhamira ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ya kuhakikisha kila Mzanzibari anapata huduma bora za afya kwa wakati.

Kongamano la Zanzibar Afya Week 2025 litafanyika kwa siku saba kuanzia Mei 4 hadi 10, 2025 mwaka huu visiwani Unguja na Pemba.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Aprili 11, 2025 jijini Dar es Salaam wakati uzinduzi huo, Mazrui amesema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inatambua kwamba afya bora ni msingi wa maendeleo ya kijamii
na kiuchumi.

“Zanzibar Afya Week 2025 inahusiana moja kwa moja na vipaumbele vya Serikali vilivyobainishwa katika Dira ya Maendeleo ya Zanzibar 2050 pamoja na Mpango wa Mkakati wa Afya wa Zanzibar III.

“Katika wiki hii muhimu ya afya, tunatarajia kushirikiana na wadau mbalimbali ili kufanikisha malengo makuu mbalimbali ikiwemo kuongeza Uelewa wa Afya kwa Jamii kupitia kampeni za elimu, kambi za afya, na huduma za uchunguzi wa magonjwa bure pamoja na kuhamasisha wananchi kuchukua hatua za kujikinga na magonjwa,” amesema.

Aidha amesema ipo haja ya Kukuza Utalii wa Afya kwani Zanzibar ina nafasi kubwa ya kuwa kitovu cha utalii wa afya ambapo utaongeza mapato ya nchi na kutoa
ajira kwa vijana wengi.

“Kongamano hili la siku saba litawapa wadau fursa ya kujadili matumizi ya telemedicine, mifumo ya kidijitali ya afya, na mbinu nyingine za kisasa katika utoaji wa huduma za afya.

“Kuhamasisha Ushirikiano Kati ya Serikali na Sekta Binafsi (PPP)… tutatumia jukwaa hili kuvutia uwekezaji katika sekta ya afya, kujenga miundombinu bora ya hospitali, na kuongeza upatikanaji wa vifaa tiba vya kisasa,” amesema.

Ameongeza kuwa Zanzibar Afya Week 2025 itakuwa ya kipekee na yenye historia kubwa kwa Zanzibar.

“Hatutakiwi kukosa fursa hii, Kwa heshima kubwa, pia tutatoa tuzo maalum kwa watu waliotoa mchango mkubwa katika sekta ya
afya siku ya kilele cha tukio.

“Napenda kuwaomba wadau wote wa afya, sekta binafsi, mashirika ya kimataifa, vyombo vya habari, na wananchi kwa ujumla
tushirikiane bega kwa bega kuhakikisha Zanzibar inakuwa mfano wa kuigwa katika utoaji wa huduma bora za afya,” amesema.

Naye Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya Zanzibar, Dkt. Mngereza Miraji amesema Zanzibar Afya Week ni wazo la Wizara ya Afya Kwa kushirikiana na Zenji Zuri na Equnox kampuni za Zanzibar, ikiwa na lengo la kuunganisha jamii, sekta binafsi, wadau wa maendeleo, na taasisi mbalimbali katika jitihada za pamoja za kuboresha huduma za afya Zanzibar, kukuza utalii wa tiba, na kuhimiza matumizi ya ubunifu na teknolojia katika mfumo wa afya.

Ameeleza kuwa kauli mbiu ya Zanzibar Afya Week 2025 ni ‘Advancing Health, Innovation, and Wellness in Zanzibar’ ambapo inaakisi dhamira ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ya kuimarisha huduma za afya kupitia ushirikiano wa sekta mbalimbali na uwekezaji endelevu.

“Tukio hili la leo linaashiria uzinduzi rasmi wa maadhimisho haya kwa upande wa Tanzania Bara, na linalenga kuhamasisha ushiriki wa wadau mbalimbali kutoka sekta ya afya, mashirika ya maendeleo, taasisi za elimu, na jamii kwa ujumla,” amesema.

Awali Mkurugenzi wa Jiji la Dar es Salaam, Elihuruma Mabelya: “Tunawahakikishia tutakuwa mstari wa mbele katika kulitangaza jambo hili ili kuhakikisha Zanzibar inakuwa ya mfano wa kuigwa katika sekta hii muhimu ya Afya,”.