SERIKALI imesema wanyamapori waliohamishiwa Hifadhi ya Taifa ya Kitulo, wamechelewa kuzaliana kutokana na kubadili mazingira ya awali, lakini baada ya miili kukubaliana na mazingara hayo sasa wameanza kuzaliana.
Akijibu swali bungeni leo Juni 5, 2024 kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii, Naibu Waziri wa Kilimo, David Silinde, amesema: “Mnamo mwaka 2018 Wizara ya Maliasili na Utalii kupitia Taasisi ya TANAPA ilihamishia pundamilia 21 kwenye Hifadhi ya Taifa Kitulo na kwa sasa wapo pundamilia 24.
“Mwaka 2019 swala 34 walihamishiwa katika hifadhi hiyo na kwa sasa idadi ya swala imefikia 42,”amesema Naibu Waziri huyo akijibu swali la Mbunge wa Makete, Festo Sanga, aliyehoji ni lini Serikali itaongeza wanyama Hifadhi ya Kitulo.
“Hata hivyo, wanyamapori hao walichelewa kuzaliana kutokana na kubadili mazingira ya awali, lakini baada ya miili kukubaliana na mazingira sasa wameanza kuzaliana.
“Mheshimiwa Spika, ili kuweza kuongeza idadi ya wanyamapori katika Hifadhi ya Taifa Kitulo, Wizara ya Maliasili na Utalii kupitia taasisi zake za TANAPA na TAWIRI inaendelea kufanya tathmini, ili kutambua aina ya wanyamapori wengine watakaoweza kustahimili hali ya hewa ya Kitulo na ambao hawataleta madhara kwa ikolojia ya hifadhi hiyo ambayo ni ya kipekee nchini na duniani,” amesema Naibu Waziri.