Kocha Mkuu wa Kagera Sugar, Mecky Mexime, amesema kuwa sare ya 2-2 dhidi ya Azam na sare ya 1-1 dhidi ya Azam anahesabu kuwa kama ni ushindi kwake na amewapongeza wachezaji wake Kwa kucheza mechi mbili kubwa nyumbani na kupata matokeo mazuri.
Mexime amesema kuwa lazima wafurahie sare hizo kama ushindi kwa sababu ya ubora wa vikosi vya Azam na Simba ambavyo ni ndoto ya kila kocha kufundisha. Kocha huyo mzawa amesema timu hizo zina wachezaji wazuri ambapo kila unachofundisha kinapokelewa kirahisi na wachezaji na kufanyiwa kazi.
“Simba, Yanga na Azam zina wachezaji bora kwahiyo ni rahisi kupokea maagizo na kuyafanyia kazi kirahisi. Unapopata sare namna hii dhidi ya Simba inakuwa ni kipimo kizuri cha kikosi chako,” alisema Mecky Mexime katika mahojiano yake na waandishi wa habari baada ya mechi ya Kagera Sugar dhidi ya Simba.
Kocha huyo amesema alipokabidhiwa timu toka kocha mkenya Francis Baraza hakufanya mambo mengi bali aliwaaminisha wachezaji kwamba wana uwezo mzuri wa kushinda na wachezaji walipolipokea hilo timu ukaanza kubadilika na kupata matokeo mazuri na hivyo anaamini tatizo la Kagera Sugar halikuwa uchezaji bali saikolojia za wachezaji.