Hivi karibuni nilisafiri kati ya Dar es Salaam na Iringa. Njiani niliona mengi ya kuvutia, na mengine ya kuhuzunisha pia.

Kilometa chache kutoka Mikumi kama unakwenda Iringa kuna wananchi wanaoishi maisha duni. Kuna biashara ndogo za mapapai na miwa.

Biashara iliyoshamiri ni ya mkaa. Uoto wa asili katika eneo hili lenye milima unaashiria hatari ya kugeuka jangwa. Vijana kwa wazee biashara yao ni ya mkaa. Imekuwa kama dhambi wao kuona miti mikubwa. Malori husimama kupakia mkaa kadiri madereva wanavyotaka.

Sambamba na mkaa, kuna bidhaa nyingine zinazotokana na miti. Kwa sababu ya miteremko na milima mikali, wananchi hawa wameona biashara ya ‘vigingi’ ni nzuri sana kwao maana wenye malori wanavihitaji.

Nilitumia muda kutafakari juu ya biashara hii ya vigingi! Vigingi ni zao linalotokana na miti mikubwa. Huwezi kutumia miti midogo (matawi) kutengeneza hizi bidhaa. Yanahitajika mashima yaliyoshiba kupata vigingi.

Biashara hii ni ishara yetu ya umaskini uliotopea. Umaskini huu si wa hali, bali zaidi ni wa akili. Gharama ya kuumaliza umaskini huu sidhani kama ni kubwa kiasi cha kuishinda serikali na wadu wengine.

Miti inayokatwa kwa ajili ya kutengeneza vigingi, ni mingi. Athari zinazotokana na uamuzi wa kufanya biashara hii ni kubwa na nyingi kuliko faida ndogo wanayopata wakataji wa hii miti. Tunaweza kusema hivyo hivyo kwa watengeneza vinu pia.

Kwa watu wanaopenda na kuheshimu mazingira wangepaswa kubuni mbadala wa miti kutengeneza vigingi. Kunaweza kutengenezwa vigingi kwa kutumia vyuma, au malighafi nyingine tofauti na miti. Kukata mti ulioishi miaka 50 au 100 kwa lengo la kupata vigingi 20 ni umaskini wa mawazo.

Wananchi wa eneo lote hili la milima ya Iyovi hadi Ruaha wangeweza kuelimishwa wakawa wafuga nyuki, maana miti na maji vinapatikana. 

Hawa wakiwa wafuga nyuki bila shaka asali ingewatajirisha zaidi kuliko uharamia huu wa vigingi na mkaa. Sasa hili si suala lao wenyewe. Kunahitajika msukumo wa kimamlaka. Waelimishwe faida za kutunza miti, maana kwa sasa wanachoangalia zaidi kwao ni maisha.

Hii ni kazi ya serikali na asasi za kiraia zinazojihusisha na mazingira. Ni suala tu la kuwabadili kutoka kwenye ukataji miti na kuwa watunzaji wa miti ili iwanufaishe kwa mengi, ukiwamo ufugaji wa nyuki. 

Hatuwezi kuwa jamii ya watu tunaokata miti kwa kigezo tu kwamba sisi ni maskini. Mkaa au vigingi haviwezi kumaliza umaskini wetu, badala yake mambo hayo mawili ndiyo kichocheo cha huo umaskini. Bila ulinzi wa miti tutaangamia. Kasi ya ukataji miti ni kubwa mno. Inatisha.

 Jambo jingine linalostaajabisha ni biashara haramu ya mafuta yanayoibwa kutoka kwenye malori. Kila baada ya mita kadhaa kuna makundi ya vijana wenye vyombo (madumu) mahususi kwa ajili ya kujaza mafuta ya wizi ambayo mara nyingi wanayapata kutoka katika hayo malori. Wao hununua na kuuza pia.

Kwa kulitazama jambo hili unaweza kuona ni maisha ya kawaida, lakini ukweli ni kuwa mamlaka za nchi zimekuwa vipofu katika kukemea na kudhibiti biashara hii ya wizi.

Kinachoendelea kweye hii biashara ni uhujumu uchumi. Wenye malori wanaingizwa hasara kubwa, na pengine ndiyo maana wapo wanaogoma kuwapa mikataba madereva kwa kutambua kuwa wanaibiwa sana.

Mamlaka za nchi zimekaa kimya kana kwamba haya mambo si makosa ya jinai. Ni mambo ya kustaajabisha kuona wezi wanajipanga barabara kuu zote za nchi na wakubwa wakipita wakiwatazama bila kuwachukulia hatua hata za kuwakemea tu.

Nchi ya watu wastaarabu haiwezi kukaa kimya ikiona magenge ya wizi wa mafuta yakiendesha biashara hii haramu bila hofu. 

Tabia za aina hii hazikomei hapo. Mtoto mwenye wazazi wezi wa aina hii wanaotamba hadharani atazuiwa na nini naye asiwe mwizi katika maisha yake? Matokeo yake tuna kizazi cha sampuli ya wizi na udokozi kila mahali.

Tunapojadili uvunjifu wa maadili hatuna budi kutazama mambo kama haya. Watoto wanakua wakijua wizi ni sehemu ya maisha, na matokeo yake kila mahali ni wizi, wizi, wizi na maisha ya ujanja ujanja.

Yote haya tunayatazama kama mambo ya kawaida, japo ukweli ni kuwa si mambo mazuri.