Bila shaka ni jambo la kusubiri na kuona baada ya mawaziri wawili wa Awamu ya Tano kutembelea kwa ziara ya kushtukiza maeneo athirika kutokana na maji yanayodaiwa kuwa na athari kutoka katika mgodi huo.

Kabla ya kuitwa ABG, mgodi huo wenye mashimo matatu ya Nyabirama, Nyabigena na Gokona, yanayotumia leseni mbili tu za SML 17/96 ya Nyabigena na Gokona iliyotolewa na Serikali Februari 7, 2000 na leseni ya 18/96 iliyotolewa na Serikali Agosti 30, 1996, ulichimbwa na makampuni kadhaa.

Makampuni hayo ni pamoja na East Africa Gold Mine, Afrika Mashariki Gold Mine ya Australia, wakati Placer Dome Gold Mine, Barick Gold Mine, African Barick Gold Mine ni ya Canada na inayochimba sasa ya African Barick Gold (ABG).

Walichovuna wananchi wa vijiji hivyo ni athari ya maji ya sumu yanayotoka katika mabwawa ya mgodi huo – Nyabirama na Nyabigena – yanayotiririsha maji machafu katika makazi ya watu.

Kwanza, alikwenda Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira na Muungano), Luhaga Mpina, Januari 12 na 30, mwaka huu na kuchukua sampo za maji na kuwasilisha kwa Baraza la Taifa la Usimamizi wa Mazingira (NEMC), Bodi ya Maji ya Bonde la Ziwa Victoria (LVBWB) na Shirika la Viwango (TBS).

Licha ya kwamba muda wa kufanya uchunguzi huo umepita, lakini wadau wanasubiri majibu na Mbunge wa Tarime, John Heche (Chadema), aliyesema: “Hatua stahiki lazima zichukuliwe na endapo ukweli wa sumu hiyo utabainika mgodi utafungwa.”

Februari 10 na 11, mwaka huu, Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo, alitembelea wananchi wa vijiji vinavyozunguka mgodi huo baada ya kuombwa na Heche kutatuliwa shida za wananchi wa vijiji hivyo na mgodi huo.

Sakata la athari ya maji machafu kutoka mgodini liliibuka mwaka 2008 kutoka katika bwawa la Nyabigena na kuingia Mto Tighite na taarifa zinasema maji hayo yana sumu za kuathiri afya za watu na mifugo.

Maji machafu hayo yakitoka Mto Tighite yanakwenda moja kwa moja Mto Mara ambao ni mkubwa, na kumwaga maji yake Ziwa Victoria.

“Kama maji haya yanaingia Mto Mara na kisha Ziwa Victoria, kiafya tuna hali mbaya,” anasema Israel Marwa Hamba, mkazi wa Kijiji cha Nyangoto, Nyamongo.

Tatizo hilo liliibuka na kuendelea kuathiri kiafya wakazi wa maeneo hayo na kuua zaidi ng’ombe wanaomilikiwa na watu hao katika Kijiji cha Matongo, wa ndugu moja Mang’era Ntora.

Japo uchunguzi unafanyika kwa sasa kuhusu maji machafu yanayotoka katika mgodi huo, wahanga waliodhurika wameshutumu Serikali kuchelewa kutatua tatizo hilo.

Wataalamu kutoka Wizara ya Nishati wanafanya uchunguzi, bila shaka ni baada ya Heche kuwasilisha hoja ya wananchi wa jimbo lake namna wanavyoteseka kwa muda mrefu katika vijiji vinavyozunguka mgodi huo.

Awali, kulikuwa na majibu ya vipimo vya maabara ya Serikali ya Kenya vilivyokubaliwa pia na Mkemia Mkuu wa Serikali hiyo Machi 20, 2015 kuhusu maji hayo na kuthibitika kwamba yana sumu. Majibu hayo yanafanana na taarifa ya LVBWB ya Septemba, 2014.

Matokeo ya maji hayo yameathiri baadhi ya wananchi wakiwamo Mwikwabe Waigama wa Kijiji cha Matongo; Esther Mugusuhi wa Matongo na Anastazia Mwita wa Nyabichune anayetembelea fimbo baada ya kupooza mwili wake.

Pia wamo Debora Marwa Byanda wa Nyakunguru na Kiguha Chacha Kiguha, mwanafunzi wa Shule ya Msingi Nyansangero aliyepo Kitongoji cha Ntarechagini, Kijiji cha Komarera, Kata ya Nyamwaga aliyekabiliwa na ugonjwa wa ngozi.

Maji hayo pia yanadaiwa kuua n’gombe 168 wa familia ya  Mang’era Ntora na wengine wanaomilikiwa na Daniel Ryoba Irondo, Mwenyekiti wa Kijiji Matongo. Pia Ryoba amepoteza mbuzi kadhaa.

Mgodi huo muda wake unamalizika ukiwa umeacha walemavu wa viungo mbalimbali vya miili yao waliovipata kutokana na kupigwa risasi za Polisi, walinzi wa mgodi, kukanyagwa na madampa na kujeruhiana wenyewe kwa wenyewe wakati wakiwa kwenye harakati za kutafuta riziki kwa nyakati tofauti.

Sambamba na kuwapo kwa kumbukumbu zinazoachwa na mgodi huo, pia baadhi ya wananchi katika vijiji hivyo vinavyozunguka mgodi huo na vile vya Wilaya ya Tarime na Mkoa wa Mara kwa ujumla, wanaelezwa kupoteza maisha na familia zao zilibaki yatima muda wote.

Wakazi wa eneo hilo wanadai kwamba walichokubaliana na uongozi wa African Barick Gold (ABG) na sasa Acacia haujatekelezwa inavyotakiwa.

Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri wilayani hapa, Machage Bathromeo Machage, anasema: “Tulikubaliana kuwa mgodi utujengee chuo cha ufundi stadi (VETA), utusambazie maji safi na salama, utuwekee angalau lami kutoka mjini Tarime hadi Nyamongo, na mambo mengine lakini hadi sasa hatuoni kitu.”

Machage, Diwani wa Kata ya Matongo, anasema aliungwa mkono na Profesa Muhongo alipokosoa sifa ya mgodi huo uliojenga Shule ya Sekondari Ingwe kutoweka mbao za kufundishia za kisasa na kuachana na zile za chaki.

“Ninyi watu wa mgodi, mnasifia ujenzi wenu kuwa mmejenga na kuweka mambo ya kisasa shule za sekondari na za msingi mlizojenga, wakati mbao zinatoka kwetu mbao za chaki, hii ni ya kizamani,” anasema Muhongo wakati wa ziara yake Nyamongo.

Profesa Muhongo akaunda kamati yake ya kuchunguza matatizo yaliyopo kwa wananchi na mgodi huo iliyoanza kazi Februari 22, mwaka huu. Kamati hiyo imepewa mwezi mmoja kumaliza kazi yake.

Awali, kikosi kazi cha watu 13 kilichoongozwa na Adamu Yusufu kutoka Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, kilifanya kazi ya kuhakiki na kutathmini wale wote waliotarajiwa kutekelezewa haki hiyo na kisha kulipwa na kuhama maeneo hayo yao.

Kazi ya kikosi kazi hicho kilichoundwa na wahusika wake wa Serikali kutoka idara mbalimbali, kilitangazwa katika mkutano wa hadhara wa wananchi wa Nyakunguru uliofanyika eneo la Nyamichale.

Ilielezwa kuwa chombo hicho kilichangia zaidi kukua kwa matatizo baada ya wananchi hao kusema hadharani kuwa kikosi kazi hicho kiliongeza kero badala ya kutatua baada ya baadhi ya watu wa vijiji hivyo, walipoachwa kwa muda mrefu wakiishi maeneo hayo huku wengine waliojenga hivi karibuni wakitathminiwa na kulipwa na kisha kuhama.

Muhongo alirejeshwa kwenye kauli yake alipotembelea Kijiji cha Nyakunguru mwaka jana aliposema kuwa chanzo cha wananchi kushindwa kulipwa fidia ya kupisha mgodi huo ni baadhi ya watu waliotumia nafasi hiyo kuingiza taarifa za kutakiwa kulipwa watu waliodaiwa kuwa na magorofa mawili walioudai mgodi bilioni 60.

Profesa Muhongo anasema hujuma hiyo imefanywa na baadhi ya watumishi wa Serikali, wananchi na mgodi, na kwamba wananchi walitarajia kuwa kwa vile Serikali ilifahamu hilo, wangelichukuliwa hatua za kiutumishi, na kisha kisheria lakini hadi sasa kimya.

Hadi sasa wananchi walio wengi wanasubiria mgodi huo uliodaiwa kuhusika kwa sehemu kubwa ungeliwajibishwa kisheria kama ilivyo kwa serikali za nchi nyingine – kwa makosa ya kuvunja mkataba wa uchafuzi wa mazingira na kusababisha madhara hayo kadhaa.

Licha ya vyombo kama NEMC, LVBWB, TBS na vinginevyo vya Serikali vilivyokuwa vikionya na kuagiza mgodi huo utekeleze upungufu uliokutwa mara kwa mara, mgodi huo haukuzingatia.

Sakata la maji machafu, mauaji ya mara kwa mara ya wananchi, kushindwa kuhamishwa na mgodi huo makazi yao, kupata mimba kwa baadhi ya akinamama, nyumba kupasuka na nyingine kuanguka limeshika kasi.

Je, kilio cha wakazi wa vijiji mbalimbali vinavyozunguka Mgodi wa North Mara unaomilikiwa na Kampuni ya Madini ya African Barick Gold (ABG) ya nchini Uingereza, kitapata majibu? bila shaka ni jambo la kusubiri na kuona.