Mawaziri wameondoka, Kikwete rekebisha sheria

 

Wiki iliyopita kwa mara nyingine nchi yetu imepata mtikisiko. Imepata mtikisiko kutokana na mawaziri wanne kupoteza nyadhifa zao. Haya yametokea Ijumaa ya Desemba 20, 2013. Mawaziri hawa; Khamis Kagasheki (Maliasili na Utalii), Shamsi Vuai Nahodha (Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa), Mathayo David Mathayo (Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi) na Emmanuel Nchimbi (Mambo ya Ndani), wameacha sura mbili.

Kwanza kabla sijajadili sura zilizoachwa niseme mapema hapa kuwa nimesikitishwa kwa kiwango kikubwa cha uonevu uliofanywa na askari walioendesha Operesheni Tokomeza. Askari hawa tulichapisha habari kadhaa zenye kuonyesha jinsi walivyogeuka miungu watu. Hawa walikuwa wakifika nyumbani kwa mtuhumiwa wanasomba mbao, mahindi, milango, wanapiga mateke hadi mbuzi.

 

Kimantiki unajiuliza uhusiano wa mbuzi kupigwa mateke na msako wa pembe za ndovu au bunduki za kuulia wanyama huuoni. Watu waliofika kwenye eneo la tukio waliniambia kuwa yalifanyika matendo mabaya mno. Matukio ya watu kusokomezwa chupa kwenye sehemu ya haja kubwa, kufungwa mawe kwenye sehemu za uzazi na kuambiwa wasimame na kutembea, yamefanyika.

 

Kimsingi unyama uliofanyika, sitaki kuamini kuwa utaishia tu kwa hawa mawaziri kujiuzulu. Nasema hivyo, kutokana na ukweli kwamba baada ya Kagasheki, Nchimbi na Nahodha kutangaza kujiuzulu, na hatimaye Mathayo uteuzi wake ukatenguliwa, ghafla nilishuhudia sherehe katika baadhi ya mitaa na familia. Ila mimi nasema kuondoka kwa mawaziri hawa si mwisho wa kadhia.

 

Sitanii, hapo juu nimesema suala hili lina sura mbili. Wapo wenye matarajio yao kisiasa waliokuwa wanaona kuwa wakubwa hawa ni tatizo kwao, hawa wamekesha wakinywa na kushangilia. Sura ya pili ni kundi la watu wanaojihusisha na ujangili, hakika hawa wamepata nguvu ya pekee. Wapo walionipigia simu, wakitamba kuwa wako wapi sasa hao waliojifanya watetezi wa tembo.

 

Narudia, sikubaliani hata chembe na hatua ya askari kutesa, kudhihaki na kuua watu, lakini napenda kuweka kumbukumbu sawa kuwa Bunge limefanya uamuzi huu kwa uchungu wa ama watu wetu kuteswa na kuuawa, lakini uamuzi huu umewapa ushindi majangili. Operesheni Tokomeza ilisitishwa, hasa kwa maaskari hawa kujihuisha na vitendo vya uporaji mali za watu ikiwamo mifugo, lakini inabaki kuwa shida kwa taifa.

 

Ikumbukwe hawa si mawaziri wa mwanzo kuondoka. Februari 7, mwaka 2008 Edward Lowassa alijiuzulu uwaziri mkuu kutokana na Bunge kuchunguza likabaini kukiukwa kwa taratibu katika mkataba wa Richmond. Lowassa alipojiuzulu Katiba inasema wazi kuwa Baraza la Mawaziri akiondoka Waziri Mkuu nalo linavunjika papo hapo. Huhitaji baraka au uamuzi wa mtu mara tu Waziri Mkuu anapoondoka.

 

Mei 4, mwaka 2011 mawaziri sita wakiwemo Waziri wa Fedha Mustafa Mkulo, Waziri wa Nishati na Madini William Ngeleja, Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii Dk. Haji Mponda, Waziri wa Maliasili na Utalii Ezekiel Maige, Waziri wa Usafirishaji Omari Nundu, na Waziri wa Viwanda na Biashara Cyril Chami walifukuzwa kazi. Pia manaibu Waziri wa Usafirishaji Athumani Mfutakamba na Naibu Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Lucy Nkya nao walifutwa kazi. Sitamzunguzia Andrew Chenge, mzee wa vijisenti.

Sitanii, Serikali hii ya Awamu ya Nne inawezekana itaingia kwenye rekodi ya kubadili mawaziri mara nyingi. Ila wapo wanaojiuliza kuwa je, mawaziri hawa makosa wanayotuhumiwa nayo wametenda kweli? Je, wanapoondoka mawaziri, tena wakati mwingine bila kupewa fursa ya kujitetea (natural justice) kama Lowassa na Mathayo walivyosema, watendaji waliohusika wanaadhibiwaje?

 

Najaribu kuwaza kwa sauti hapa. Uhalisia, Operesheni Tokomeza ilitangazwa na Rais Kikwete akiwa nchini Marekani. Zipo dhana hapa, kwamba Rais alipoagiza operesheni ifanyike, mawaziri walipaswa kuhakikisha inafanyika vizuri. Ikiwa ni kweli kuwa mawaziri hawa hawakupata kukutana, basi hilo ni kosa la msingi kiutendaji.

Lakini wapo wanaosema mawaziri nao waliagiza vyombo vya dola, na kuna amri ya Mkuu wa Majeshi, Jenerali Davis Mwamunyange, inayoelekeza kuanza kwa operesheni hii. Ndio, nasikitika kuwa raia 13 au zaidi wameuawa na watendaji hawa wasiokuwa na maadili, lakini najiuliza askari 6 waliouawa kwa nini waliuawa? Hawakufia harusini askari hawa, walikuwa kwenye mapambano. Ni vita.

 

Haya yalikuwa mapambano. Narudia, Operesheni iliendeshwa kwa makosa makubwa katika baadhi ya maeneo, lakini imetufumbua macho kuona kuwa maafisa wanyamapori tuliowakabidhi jukumu la kulinda wanyamapori kumbe ndio waliokuwa wakiua wanyamapori. Askari kadhaa walikamatwa, ila kwa kuwa inadaiwa ni sehemu ya mtandao wa wabunge waliogoma kuwataja bungeni, wameachiwa haraka mno.

 

Sitanii, Serikali isahihishe makosa yaliyojitokeza katika Operesheni Tokomeza na operesheni hii irejeshwe mara moja. Tukiruhusu Operesheni hii kusitishwa, hakika tembo tutabaki kuwaona kwenye video. Jingine, ambalo nalo ni la msingi, Sheria ya Utumishi wa Umma Na 8, ibadilishwe. Waziri hana mamlaka yoyote kwa watendaji wa wizara.

Yaani ikitokea Waziri akapigwa kibao na dereva wake, kisheria inabidi apeleke mashitaka kwa Katibu Mkuu, Katibu Mkuu aunde Kamati ya Uchunguzi, Kamati isikilize malalamiko ya Waziri na imhoji dereva, kisha akipatikana na hatia anapewa onyo la kwanza.

 

Kwa mfumo huu wa kisheria, tutashuhudia mawaziri wetu wakiangushwa kila leo, na hasa wizara ya Maliasili na Utalii ambayo tangu mwaka 2005 hadi leo imeongozwa na mawaziri sita. Sheria iwape meno mawaziri, wakishindwa tuwahukumu kwa haki.