Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam

Waziri wa Nishati, January Makamba amesema Mawaziri 6 kutoka Tanzania na Zambia watakutana kwenye kikao kazi kitakachojadili ushirikiano baina ya nchi hizi mbili katika ulinzi na usalama wa Bomba la Mafuta la TAZAMA na sekta ya nishati kwa ujumla wake.

Kikao kazi hiki, kitatathmini utekelezaji wa masuala ya ulinzi na usalama wa bomba la mafuta la TAZAMA kama ilivyokubalika katika kikao cha kwanza cha Wizara hizi tatu kilichofanyika mwezi Desemba, 2022 jijini Dar es Salaam baada ya Serikali ya Zambia kuamua kutumia bomba hili kusafirisha mafuta safi badala ya mafuta ghafi (crude oil).

Bomba la TAZAMA lina urefu wa KM 1,710 kutoka Kigamboni – Dar es salaam hadi Indeni – Ndola Zambia. Changamoto kubwa ni ulinzi na usalama wa bomba hilo baada ya kuanza kusafirisha mafuta yaliyosafishwa badala ya mafuta ghafi.

Katika kikao cha kwanza ilikubalika mikakati mbalimbali itekelezwe ikiwemo ushirikishwaji wa wanavijiji katika sehemu ambapo bomba linapita.

Kwa upande wa Tanzania kikao hicho kitaongozwa na Mhe. January Makamba (Mb.) – Waziri wa Nishati na kuhudhuriwa na Mhe. Innocent Bashungwa (Mb.) – Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa na Mhe. Mhandisi Hamad Masauni (Mb.) – Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi.

Kwa upande wa serikali ya Zambia, kikao hicho kitawahusisha Mhe. Ambrose L. Lufuma- Waziri wa Ulinzi, Mhe. Jacob J. Mwiimbu- Waziri Mambo ya Ndani na Mhe. Mha. Peter C. Kapala- Waziri wa Nishati.

Haya ni mashirikiano mazuri kati ya nchi zetu hizi na pia ni mwendelezo wa mahusiano mema unaofanywa na Viongozi wetu Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mhe. Hakainde Hichilema, Rais wa Jamhuri ya Zambia kama yalivyoasisiwa na Viongozi wetu wa kwanza Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius K. Nyerere na Hayati Kenneth Kaunda.