Mpita Njia (MN) anakumbuka alipokuwa mdogo mama yake alimwambia kuwa ukitaka kujua tabia halisi ya mtu yeyote mpe kimoja, viwili au vyote kati ya hivi: pesa, pombe au madaraka.
Kwa umri alionao Mpita Njia, hahitaji ushuhuda wa maneno hayo ya mama yake. Amekwisha kuyaona mwenyewe na kuyathibitisha.
Kuna mawaziri wawili katika Baraza la Mawaziri la Serikali hii ya Awamu ya Tano ambao baada ya kupata viwili vya uhakika – pesa na madaraka, tayari ‘sura’ zao halisi zimekwisha kujulikana!
Kwa kuwa haya si majungu, Mpita Njia anaona heri awataje tu kwani kwa uzee wake akifa na jambo hili moyoni atakuwa hakujitendea haki.
Mawaziri ambao Mpita Njia amewavulia kofia ni yule wa TAMISEMI, na mwingine ni yule aliyekiri kuokotwa jalalani.
Mawaziri hawa, ama kwa kiburi, au kwa ulevi wa madaraka hawataki kabisa kupokea simu za wanahabari wengi walio katika vyumba vya habari. Malalamiko yamekuwa mengi, lakini hakuna mwenye uthubutu wa kulisema hili.
Mawaziri hawa hata upige simu namna gani, upige usiku, upige mchana, upige jioni, upige asubuhi, hawapokei! Leo uwaziri tu wameota ‘majipu ya kwapa’ wakikwea juu itakuwaje? Hatari sana.
Mpita Njia anajiuliza, kama mwenye nchi anapokea na kupiga simu, hawa mawaziri kiburi hiki wanakitoa wapi? Kwanini hawataki kupokea wala kujibu sms? Je, ndiyo kusema kuwa baada ya kupata madaraka ndiyo wameota majipu ya kwapa na kuwafanya sasa wajione hawana sababu ya kuwasilikiza wenye shida?
Mpita Njia, kwa kuzingatia kuwa hapendi majungu, ameona ni vema akalisema hili hadharani ili ikiwezekana wahusika hawa wawili watambue kuwa tabia hizi za kugoma kupokea simu si za kiungwana.
Lakini pia kama wanagoma kupokea simu kutoka kwenye vyumba vya habari, watapokea simu ya kabwela anayeteseka kwa kukosa msaada kutoka katika ofisi zao?
Mpita Njia anarejea kuuliza, kama rais mwenyewe anapokea, anapiga simu na kujibu sms, mawaziri hawa wamelewa nini cha kuwafanya wawe jeuri? Je, si kweli kwamba cheo ni dhamana kwa maana leo unacho na kesho kipo kwa mwingine? Wajisahihishe.