Na Daniel Limbe, JamhuriMedia, Karagwe

LICHA ya mikakati mikubwa ya serikali kufikisha huduma ya maji safi na salama kwa wananchi waishio mijini na vijijini,baadhi ya wakazi wa vijiji vya Lukole,Ihanda,Rulalo na Chonyonyo, wamelishukuru shirika lisilo la kiserikali ya Mavuno Project la wilayani Karagwe mkoani Kagera,kuimalisha ndoa zao baada ya kusambaza maji ya bomba kwa jamii.

Kupatikana kwa huduma hiyo kunadaiwa kuondoa adha ya muda mrefu ilivyokuwa ikiwakabili wananchi wa vijiji hivyo ambao awali walilazimika kuchangia maji hayo na mifugo kutoka kwenye madimbwi.

Mbali na hilo,baadhi ya ndoa ziliteteleka kutokana na wanawake kuamka usiku wa manane na kuacha waume zao kitandani kwa lengo la kutafuta maji katika umbali mrefu hali iliyokuwa ikisababisha mifarakano ya mara kwa mara katika baadhi ya familia.

Baadhi ya wananchi wa vijiji hivyo wamesema hayo kwa nyakati tofauti baada ya kutembelewa na timu ya Marafiki wa Afrika kutoka nchini Swiden wahandisi wasio na mipaka kutoka Ujerumani na Swiden pamoja na wadau wa maendeleo kutoka Austria ambao ni wafadhili wa miradi inayotekelezwa na shirika la Mavuno.

Hatua hiyo ni kuelekea maadhimisho ya miaka 30 ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya jamii kwa shirika hilo ambayo inahusisha,huduma za maji,kilimo,uhifadhi wa mazingira, umeme jua, umeme utokanao na gesi asilia pamoja na uhifadhi wa chakula.

Tusabe Stephano,mkazi wa kijiji cha Ihanda, amesema awali kabla ya jamii hiyo kupata msaada wa maji safi kutoka shirika la Mavuno walikuwa wakitumia gharama kubwa kupata huduma za afya kutokana na milipuko ya magonjwa yatokanayo na maji machafu.

“Kwa kweli hali ilikuwa mbaya sana kabla ya kuwekewa maji haya na shirika la Mavuno,tulikuwa tunalazimika kutumia maji machafu kwajili ya kunywa, kupikia, kuoga pamoja na kufulia nguo licha ya kwamba tulikuwa tukichangia na mifugo”amesema Tusabe.

Kwa upande wake msimamizi wa miradi wa maji kutoka shirika Mavuno,Hashimu Mohamed,amesema kuwa huduma hiyo imesaidia kupunguza magonjwa yatokanayo na maji machafu ambayo walikuwa wakichota kutoka kwenye madimbwi yanayotumiwa na mifugo.

Pia uwepo na huduma ya maji yenye uhakika imewasaidia kuinua uchumi wa kaya zao baada ya muda waliokuwa wakiutumia kutafuta maji sasa unatumika kuzalisha mali kwa kufanya kazi mbalimbali.

Hata hivyo amesema kuwa maji hayo husukumwa kwa nguvu ya umeme kutoka chanzo chenye urefu wa mita 135 kutoka chini ya ardhi kwa kutumia mashine zenye kiwango kikubwa ambapo hutumia nishati ya umeme wa Tanesco, umeme jua unaozalishwa na shirika la Mavuno pamoja na mashine inayotumia mafuta ya dizeli.

Mkurugenzi wa shirika hilo,Charles Bahati,ameiambia Jamhuri Digital kuwa takribani matenki makubwa 78 yenye ujazo wa maji lita 96000 kila moja yamejengwa kwenye vijiji vya Ihanda,Rulalo,Lukole na Chonyonyo wilayani Karagwe.

Aidha kati yake matenki saba yanatumiwa na jamii kujipatia maji safi na salama ukiachilia mbali taasisi binafsi na zile za kiserikali.

Kadhalika jumla ya matenki 682 yenye ujazo wa lita 16,000 yamejengwa ngazi ya kaya kwaajili ya kuvuna maji ya mvua hatua ambayo imesaidia kunusuru afya za wananchi.

Mbali na matenki, shirika hilo pia limefanikiwa kuotesha miti takribani 4,700,347 katika maeneo mbalimbali katika wilaya ya Karagwe na Kyerwa kwa lengo la kuinua uchumi wa kaya na kudhibiti uharibifu wa mazingira.

“Tumefanikiwa kutoa semina 623 kwa makundi mbalimbali katika jamii kuhusiana namna bora ya kuhifadhi chakula,kutunza mazingira,kuvuna maji ya mvua majumbani na umuhimu wa kuyatumia ambapo takribani wakazi 5,170 wamenufaika na huduma ya maji safi”amesema Bahati.

Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Karagwe,Wallence Mashanda,amekiri kazi kubwa iliyofanywa na shirika hilo kwenye wilaya hiyo,na kwamba pasipo jitihada zao hali ilikuwa mbaya zaidi kwa baadhi ya maeneo ya vijijini ambako Serikali haijawafikishia baadhi ya huduma wananchi wake.

“Ni kweli Mavuno wamekuwa msaada mkubwa sana kwa jamii na kwa serikali yetu hapa Karagwe,maana awali kulikuwa na baadhi ya vijiji watu walikuwa hawaishi kabisa kutokana na ukosefu wa maji,lakini baada ya huduma hiyo kupatikana watu wamejenga na kuendeleza maisha yao kwa amani” amesema

Vilevile amesema serikali itaendelea kushirikiana na taasisi zote zenye lengo la kuihudumia jamii katika nyanja tofauti ili kuharakisha maendeleo ya wananchi hasa waishio vijijini.

Please follow and like us:
Pin Share