Na Zulfa Mfinanga,Jamhuri Media, Arusha
Waziri wa Madini Anthony Mavunde amewaondoa hofu wafanyabiasha wa madini kuwa serikali haina mpango wa kuchukua madini yao yatakayobaki katika minada.
Mavunde amesema kumekuwa na dhana potofu kuwa serikali ilichukua madini ya wafanyabiasha katika minada iliyofanyika mwaka 2017 na kutoa ufafanuzi kuwa madini hayo yamehifadhiwa Benki Mkuu na wakati wowote wenye madini hayo wataitwa na kukabidhiwa.
Akizindua minada ya ndani ya madini ya vito iliyofanyika leo katika mkoa wa kimadini Mirerani Manyara iliyowakutanisha wadau wa madini kutoka ndani na nje ya nchi amesema minada hiyo inaendeshwa na Tume ya madini kwa kushirikiana na soko la bidhaa Tanzania (TMX) kupitia mfumo wa mauzo wa kielektroniki ili kuweka uwazi kwa wadau wote wa madini.
Amesema sekta ya madini imeendelea kukua na kuongeza fedha katika mfuko mkuu wa serikali kutoka shilingi bilioni 161 katika mwaka wa fedha 2015/2016 hadi kufikia shilingi bilioni 753 huku lengo ni kukusanya trilioni moja kwa mwaka wa fedha 2024/2025.
“Makusanyo haya yanatokana na udhibiti mzuri uliowekwa na serikali kwani madini ya vito ni tofauti na madini mengine hivyo kuwa na ushindani mkubwa duniani” amesema Mavunde na kuongeza.
“Pia niwahakikishie kuwa hakuna madini ya mtu yatakayobaki baada ya minada kumalizika yatachukuliwa na serikali, na hata yale madini yaliyobaki mwenye mnada wa mwaka 2017 yapo BoT na wakati wowote wahusika wataitwa kukabidhiwa madini yao”
Naye Mkuu wa mkoa wa Manyara Queen Sendiga ameiomba serikali kuwatenganisha wafanyabiashara wadogo na wakubwa kwenye minada ya madini ili kuhakikisha kila kundi linafaidika na minada hiyo.
Amesema utaratibu uliopo sasa wa kuwachanganya wote kwa pamoja utasababisha baadhi yao kutoka patupu.
Akijibu hoja hiyo Waziri Mavunde amewatoa hofu wafanyabiashara wadogo kwamba minada ya wafanyabiashara wadogo itaendelea kuwepo ili kuweka usawa kwenye soko la ushindani.
Akizungumza kwa niaba ya Mwenyekiti wa kamati ya kudumu ya nishati na madini, mbunge Kirumbe Ng’enda amesema serikali inaendelea kuboresha bajeti ya wizara ya madini ili ifike hatua wachimbaji waweze kuchimba madini eneo lenye uhakika wa upatikanaji wa madini kwani hadi sasa ni asilimia 16 tu ya eneo lenye uhakika wa upatikanaji wa madini nchini.
Naibu Katibu Mkuu wizara ya madini Msafiri Mbibo amesema madini yenye gramu 184.06 yenye thamani ya shilingi bilioni tatu yatauzwa kwenye minada hii iliyowakutanisha jumla ya wauzaji 195.
Amesema minada hiyo ilianza rasmi mwaka 1992 na mwaka 2017 serikali iliisimamisha ili kuangalia namna bora ya uendeshaji ili kuhakikisha wafanyabiasha na Taifa kwa pamoja wananufaika nayo.
Mbunge wa Jimbo wa Simanjiro Christopher Ole Sendeka amemuomba Waziri Mavunde kushughulikia kero ya ukaguzi getini inayosababisha watu kutoka kuanzia saa saba hadi saa nane usiku kutokana na foleni kubwa ambapo Waziri walimuomba Mkuu wa Mkoa kushughulikia kero hiyo.