MBUNGE wa Jimbo la Dodoma Mjini, Anthony Mavunde ameanza ujenzi wa viwanja vya michezo ya mpira wa kikapu (basketball), mpira wa pete (netball) na mpira wa wavu (volleyball) katika eneo la shule ya Sekondari Kiwanja cha Ndege Jijini Dodoma.
Ujenzi huu unatokana na ahadi ambayo aliitoa wakati wa mahafali ya wanafunzi wa kidato cha nne alipokuwa Mgeni Rasmi.
Akizungumza na wanafunzi leo Machi 27, 20234 Mavunde amesema kiwanja hicho ambacho kitatumika kwa matumizi ya aina tatu ya michezo kitakuwa ni cha kisasa na kitasaidia kukuza michezo na vipaji vya wanafunzi wa Dodoma Jiji.
Pamoja na ujenzi huo,pia ameahidi kuweka taa katika uwanja huo ili uwe unatumika muda wote,kugawa seti za michezo na kununua tanki la kuhifadhi maji.
Akitoa taarifa ya maendeleo ya shule,Mkuu wa Shule Sekondari Kiwanja cha Ndege, ameishukuru serikali ya awamu ya sita chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan kwa ujenzi wa madarasa na fedha Sh Milioni 50, umaliziaji ujenzi wa maabara na kwamba kukamilika kwa ujenzi wa viwanja vya michezo shuleni hapo kutasaidia kuimarisha afya za wanafunzi na kukuza vipaji vyao kupitia michezo.
Nae, Diwani wa Kata ya Kiwanja cha Ndege Amos Mbalanga amemshukuru Mavunde kwa ujenzi wa miundombinu ya viwanja vya kuimarisha michezo na kuahidi kusimamia ujenzi wake kukamilika kwa wakati.