Jitihada za serikali kuwatafutia wateja wakulima wa korosho za daraja la tatu mkoani Pwani zimegonga mwamba baada ya wanunuzi hao kupendekeza bei ambayo wakulima wameikataa.
Kutokana na hilo, mnada wa korosho hizo za daraja la tatu uliofanyika wiki iliyopita umeshindwa kutatua tatizo hilo baada ya wauzaji na wanunuzi kushindwa kukubaliana bei.
Mwenyekiti wa Chama cha Ushirika Mkoa wa Pwani, Rajabu Ng’onoma, ameliambia JAMHURI kuwa wanunuzi wa korosho mwaka huu wameshusha kabisa bei ya korosho daraja la tatu hadi Sh 815 kwa kilo, bei ambayo aliikataa kwa sababu haina masilahi kwa mkulima.
“Matokeo yake mnada uliopangwa kufanyika ulifungwa bila ya korosho kuuzwa,” anasema akibainisha kuwa mpaka sasa hawajajua sababu zinazowafanya wanunuzi hao kung’ang’ania kushusha bei kiasi hicho.
Anasema licha ya kufanya vikao kadhaa na viongozi wa serikali ngazi ya mkoa na taifa, bado tatizo hilo halijapatiwa ufumbuzi.
Anasema kutokana na hali hiyo, wameamua kuzikabidhi kamati za wilaya jukumu hilo na kuzitaka zishirikiane na wanunuzi pamoja na wakulima katika kutafuta ufumbuzi ili wakulima wauze korosho hizo, kwani jinsi zinavyokaaa kwenye maghala zinazidi kupoteza ubora wake.
Anasema chini ya utaratibu huo mpya, kamati hizo kwa kushirikiana na vyama vya ushirika katika wilaya, watafanya minada hiyo kwenye wilaya tofauti na sasa, ambapo mnada hufanyika katika ngazi ya mkoa pekee.
Ng’onoma anasema korosho zinazidi kupoteza ubora, hivyo ni vema zikauzwa haraka iwezekanavyo ili kuhakikisha mkulima hapati hasara zaidi.
Anasema kuwa mwaka huu walitarajia kukusanya tani 30,000, lakini kutokana na changamoto za hali ya hewa wamevuna tani 9,000 pekee.
Anadai kati ya hizo, korosho daraja la kwanza na la pili zilikuwa tani 180, ambazo zote zimekwisha kuuzwa na sasa wanahangaika na korosho daraja la tatu.
Akizungumzia tatizo hilo, Naibu Waziri wa Kilimo, Omari Mgumba, amewataka wanunuzi kununua korosho hizo, kwa kuzingatia masilahi ya pande zote mbili ili kuondoa malalamiko.
Mgumba anasema kuwa wafanyabiashara na wakulima waliojumuika katika mkutano huo wametoa kero zao, na serikali imekubali kuzifanyia kazi, hivyo wafanyabiashara wasilete visingizio na badala yake wanunue korosho wanazozitaka kutoka katika minada hiyo bila ya kuwa na wasiwasi na masilahi yao.
Anasema kuwa lengo la serikali ni kuhakikisha hawaharibu taswira katika zao la korosho, na wanataka kumsaidia mkulima na mfanyabiashara wapate haki sawa katika biashara hiyo.