Kwa muda wa miezi miwili sasa Jiji la Arusha na vitongoji vyake limetikiswa na mauaji ya wanawake. Katika kipindi hicho zaidi ya wanawake kumi wameuawa baada ya kubakwa, kisha kunyongwa.
Kwa mujibu wa watu walioshuhudia maiti za wanawake hao, nyingi zilikutwa zikiwa hazina nguo huku kukiwa na dalili za kuvunjwa shingo. Hali hii imewaweka wanawake wengi katika Jiji la Arusha na vitongoji vyake katika hali ya wasiwasi mkubwa.
Watu kadhaa waliozungumza na JAMHURI wanasema kuwa mashuhuda wamekuwa wagumu wa kutoa maelezo ambayo yanaweza kulisaidia Jeshi la Polisi na vyombo vingine vya dola kufanya upelelezi na kuwanasa watuhumiwa. Hilo linawafanya wengi waamini kuwa watu wanaofanya uhalifu huo wanajulikana lakini hawatajwi kwa sababu wanalindwa na familia zao.
“Si kwamba wahalifu hatuwajui, lakini kumeibuka suala kubwa la uhasama. Iwapo utawataja au kumtaja mtoto wa mtu, ni lazima huyo kijana akufuate au hata wazazi wake wakufuate wakutishie maisha, kitu ambacho kinawapa hofu hata viongozi wetu wa chini,” anasema mmoja wa mashuhuda hao ambaye hakuwa tayari jina lake litajwe gazetini.
Wiki iliyopita katika Kata ya Sokoniwani, Mtaa wa Lolovono, Rose Chacha (51), alikutwa akiwa ameuawa kwa kunyongwa, kisha mwili wake kutelekezwa kando ya Mto Burka, jirani na anapoishi ukiwa hauna nguo yoyote.
Kwa mujibu wa shuhuda wa tukio hilo (jina limehifanyiwa), katika msiba huo, ambao pia ulihudhuriwa na Kamanda wa Polisi Wilaya ya Arusha, kuna baadhi ya wananchi waliwataja baadhi ya washukiwa wa uhalifu lakini baadaye walipata vitisho kutoka kwa familia za wazazi wa watuhumiwa.
“Hapa kinachotia woga ni vitisho, maana hata viongozi wa chini ukiwapelekea taarifa wanasema wanaogopa kufuatilia, kwa madai kuwa hata wao wanatishiwa maisha. Pia kuna baadhi ya wanawake wanabakwa lakini nao wanaogopa kutoa taarifa, maana kuna mmoja aliambiwa ukisema tutakuua kabisa kama wenzako, kwa hiyo watu wanabakwa lakini wananyamaza,” anabainisha shuhuda mwingine.
Mjumbe wa nyumba kumi wa mtaa huo, Rapson Singo, amekiri kuwapo kwa vitisho kutoka kwa watu wanaodhaniwa kufanya uhalifu huo, hali ambayo imewatia hofu wananchi kutoa ushirikiano kwa serikali.
“Ni kweli hali si nzuri, na sababu ya yote haya ni kutokana na miundombinu ya eneo hilo kuzungukwa na mito isiyokuwa na madaraja na barabara rasmi, hivyo watu wanatumia njia za panya ambapo ndipo wanapokutana na ukatili huo,” anasema kiongozi huyo wa ngazi za chini na kuongeza:
“Lakini pia ni kweli kuna suala la kutishiwa maisha. Hata sisi viongozi tunatishiwa kwa sababu hili tukio si la kwanza, ninashindwa kuyazungumzia yaliyopita kwa sababu hayajatokea katika eneo langu. Iwapo kungekuwa na jitihada zinazoonekana, matukio mengine yasingeendelea kutokea.”
Katika Kata ya Olasiti nako kunaripotiwa kutokea kwa mauaji kama hayo, ambapo mwishoni mwa mwaka jana wanawake wanane wameuawa kwa kubakwa na kunyongwa, kisha miili yao kukutwa ikiwa haina nguo.
Mmoja wa mashuhuda wa matukio hayo, Anne Kisoi, mkazi wa Mtaa wa Olasiti Kati, anasema ameshuhudia maiti za wanawake wawili kwa nyakati tofauti katika shamba linalojulikana kama ‘shamba la mihogo’, huku akisikia taarifa nyingine za kutokea matukio kama hayo katika maeneo ya karibu ndani ya kata hiyo.
Diwani wa Kata ya Olasiti, Alex Martin, anasema kuelekea mwishoni mwa mwaka jana wanawake wanane waliuawa katika kata hiyo.
Kutokana na mwendelezo wa vitendo vya mauaji katika kata hiyo, Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo, ameagiza kujengwa kituo cha polisi, ambapo tayari ujenzi wake umekwisha kuanza.
Mauaji hayo yamesababisha baadhi ya kina mama waishio kata za Olasiti na Sokoniwani kutaka kufanya maandamano ya kulaani vitendo hivyo, suala ambalo limepingwa na Jeshi la Polisi.
Kina mama hao wameliambia JAMHURI kuwa wameona ni vema kuonyesha kilio chao kwa kufanya maandamano ya amani ndani ya kata hizo na kufanya maombi maalumu kwenye maeneo yote yalikofanyika mauaji hayo.
Katika barua yao ya kuomba kibali cha kufanya maandamano hayo ya Disemba 17, 2019 kwenda kwa Mkuu wa Upelelezi Mkoa wa Arusha, wameeleza nia pamoja na maeneo ambayo maandamano hayo yatapita. Lakini wamejibiwa kwa barua yenye kumbukumbu Na. AR/24/29VOL.IX/148 ya Disemba 19, 2019 inayowataka kukusanyika katika eneo maalumu ambalo watatakiwa kulitaja na si kufanya maandamano kama walivyoomba.
“Kwa kweli sisi lengo letu ni jema sana, tumekuwa tunaishi kwa wasiwasi sana. Wanawake wengine wanashindwa kufanya biashara zao kwa amani kwa kuhofia usalama wao, kwa hiyo sisi tulihitaji zaidi maandamano ya amani kuonyesha kilio chetu, pia kuiombea Kata ya Olasiti,” anasema mmoja wa kina mama hao na kuongeza:
“Bado tuna imani na Jeshi letu la Polisi, ingawa wametutaka kukusanyika tu lakini tutaendelea kuliomba ili tufanye maandamano, lakini ikishindikana, basi tutakuwa hatuna jinsi.”
Akizungumza na vyombo vya habari hivi karibuni, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Jonathan Shana, anasema hadi sasa jeshi hilo linawashikilia watu wanane wanaodaiwa kuhusika na mauaji katika Kata ya Olasiti huku akisema wanaendelea na uchunguzi wa matukio mengine kama hayo.
Kamanda Shana anasema baadhi ya watuhumiwa hao wamekiri kuhusika na matukio hayo, ambapo wengine wamekutwa na vielelezo, zikiwemo simu za mikononi za marehemu na kwamba wanakamilisha upelelezi kabla ya kuwafikisha mahakamani.
“Nipende tu kuwaambia hao baadhi ya wazazi na hata baadhi ya viongozi, wapo pia wanaowaficha wahalifu, kwamba jeshi hili lazima lishughulike nao, kwa sababu wao ni hawalifu kama wengine, sisi tuna njia za kitaalamu za kuchnguza, wao waendelee kulindana, lakini mwisho wao upo,” anasema Kamanda Shana.