Ripoti mpya ya Shirika la Umoja wa Mataifa kuhusu Utamaduni (UNESCO) imethibitisha kuongezeka kwa mauaji ya waandishi wa habari duniani kwa asilimia 38 katika kipindi cha miaka miwili (2022-2023) ikilinganishwa na miaka miwili kabla yake.
Waandishi 162 wameuawa wakiwa kazini, na ripoti hiyo inatoa wito wa kuchukuliwa kwa hatua madhubuti dhidi ya wahusika wa mauaji haya.
Mkurugenzi Mkuu wa UNESCO, Audrey Azoulay, ameonyesha hofu kuhusu ongezeko hili na kusisitiza kwamba ni muhimu kwa mataifa kuchukua hatua kuhakikisha wahusika wanawajibishwa.
Ripoti inaonyesha kuwa Amerika Kusini na visiwa vya Caribbean ndio maeneo yenye mauaji mengi ya waandishi, huku 61 wakiuawa katika miaka miwili. Hata hivyo, Amerika Kaskazini na Ulaya Magharibi yaliripoti mauaji machache zaidi, ikiwa ni waandishi 6 pekee waliofariki.
Mkutano wa UNESCO kuhusu Usalama wa Waandishi Kufanyika Addis Ababa
UNESCO itaandaa mkutano mnamo Novemba 6 katika mji wa Addis Ababa, Ethiopia, kwa lengo la kuzungumzia usalama wa waandishi wa habari hasa wanaporipoti katika maeneo ya mizozo.