*Polisi wasema kijana aliyetaja mtandao ni mgonjwa wa akili
*Yeye asisitiza kuwa kichaa, analazimishwa dawa Muhimbili
*Ndugu waeleza historia, daktari anayemtibu aingia mitini
Jeshi la Polisi nchini limempeleka na kumlaza katika Hospitali ya Taifa Muhimbili, kijana Mohamed Malele, mshirika wa mtandao uliohusika kumuua Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Liberatus Barlow, wakidai ni mgonjwa wa akili.
Inaelezwa kuwa Malele amepelekwa na maofisa wa ulinzi na usalama kulazwa hospitalini hapo siku chache baada ya kujisalimisha kwao, akijitangaza kung’atuka ujambazi.
Awali, ilielezwa kwamba Mkuu wa Jeshi la Polisi, Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP) Said Mwema, amempatia kijana huyo hifadhi maalum huku akilindwa na kupewa huduma muhimu za kibinadamu.
Hata hivyo, uchunguzi zaidi uliofanywa na JAMHURI kwa wiki mbili, umethibitisha bila chembe ya shaka kuwa Malele amelazwa katika wodi ya wagonjwa wa akili Muhimbili na analazimishwa kunywa dawa mbalimbali.
JAMHURI imezungumza na Malele akiwa wodini Muhimbili ambapo amekana kuugua ugonjwa wa akili.
“Kabla ya kuletwa huku maaskari waliniuliza; umewahi kuugua, nikasema sijawahi kuugua, lakini wamenileta hospitali,” amesema Malele na kuendelea:
“Nikawauliza humu hospitali mtanisaidiaje, wakasema wewe nenda hospitali, tuna shaka na wewe utakuwa umetumwa na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema). Huku naletewa dawa natumia kila siku.
“Mama alikuja huku kutoa maelezo kwamba mimi si mgonjwa, na mimi niliwaeleza mbona nilichokisema mlichunguza mkakuta ni kweli, lakini wapi.”
Taarifa ya polisi
Mwishoni mwa wiki iliyopita, polisi walitoa taarifa wakisema Gazeti la JAMHURI linapotosha umma katika suala hili kama ifuatavyo:-
TAARIFA YA JESHI LA POLISI KWA VYOMBO VYA HABARI
Jeshi la Polisi nchini linapenda kutoa ufafanuzi juu ya taarifa ambayo imekuwa ikiripotiwa katika gazeti la JAMHURI la siku ya Jumanne tarehe 21 – 27 Mei, 2013 toleo No. 81 na la tarehe 28 Mei -Juni 3, 2013 toleo No. 83, yenye kichwa cha habari “MTANDAO WA MAUAJI YA BARLOW WATAJWA NA IGP MWEMA AMPA HIFADHI MUUAJI WA BARLOW”.
Taarifa hiyo siyo sahihi, kwa sababu mtu aliyehojiwa na gazeti hilo anayejulikana kwa jina la Mohamed Edward Malele ni mgonjwa wa akili, ambaye mpaka hivi sasa amelazwa katika hospitali ya Taifa Muhimbili kwa matibabu. Mara kadhaa mtu huyo amekuwa na tabia ya kuwatuhumu viongozi na watu mbalimbali juu ya tuhuma zisizo na ukweli wowote kutokana na ugonjwa wake wa akili.
Jeshi la Polisi nchini linatoa rai kwa gazeti la JAMHURI kuwa makini na habari wanazoziandika ambazo hazijafanyiwa uchunguzi wa kutosha, zenye lengo la kupotosha jamii.
Imetolewa na:-
Advera Senso-SSP
Msemaji wa Jeshi la Polisi.
Binamu wa Malele anena
Kwa upande mwingine, binamu wa Malele, ambaye ni mkazi wa Kijiji cha Igoma, alizungumza na JAMHURI kwa sharti la kutotajwa jina, amesema anamfahamu kijana huyo kama mtu mtundu aliyezoea kujichanganya na watu matajiri.
“Huyu Malele tumekua na kucheza naye pamoja, na baada ya baba yake kufariki alichukuliwa na mheshimiwa mmoja mfanyabiashara wa mjini Ngudu (Kwimba) akawa anasimamia miradi yake.
“Huyo mheshimiwa alimwamini sana na amekuwa akimwagiza kwenda kumnunulia bidhaa mbalimbali za dukani,” kimedokeza chanzo hicho cha habari na kuongeza:
“Lakini kwa muda mrefu mpaka sasa hivi, maisha ya Malele ni mjini, huku kijijini [Igoma] huwa anakuja tu kumsalimia mama yake na kumletea matumizi, na ninavyojua kijana huyo bado hajaoa.”
Habari zaidi zilizopatikana kwa mshauri wa karibu wa Malele, zinasema kijana huyo baada ya kuamua kuacha ujambazi, alikwenda kwa ofisa mmoja mwandamizi wa Jeshi la Polisi mkoani Mwanza ‘kuuanika’ mtandao wa ujambazi aliokuwa akiushiriki.
Chanzo hicho cha habari kimenukuu maelezo ya Malele kama ifuatavyo:
“Kamanda huyo alinipongeza na kunipatia shilingi laki mbili, ingawa kumbe siku hiyo mmoja wa maofisa wa polisi aliokuwa nao ofisini alikuwa mmoja wa kundi la majambazi nililomweleza.
“Kumbe nilipotoka askari yule alipiga simu kwa wenzake na kuwaeleza nilivyowafichua, na ndipo wakanisaka na kuniteka, wakanitesa kwa kunipiga, wakaninyang’anya fedha nilizokuwa nazo na kunitishia kuniua.”
Daktari aingia mitini
Kwa wiki nzima gazeti la JAMHURI limekuwa likimtafuta daktari anayemtibu kijana Mlele, lakini kila wakati amekuwa akielezwa kuwa na majukumu mengi hivyo hapati muda wa kuzungumza na JAMHURI. Maofisa Uhusiano Muhimbili pamoja na kuachiwa ujumbe wa maandishi mara mbili ofisini kwao, hadi tunakwenda mitamboni ilikuwa hawajajibu.
Alivyotaka kumnusuru Barlow
Kuna habari kwamba Malele alimwendea kiongozi mmoja wa serikali wa Wilaya ya Nyamagana kumwomba amkutanishe na Kamanda Barlow amwambie ajihadhari asiuawe na kundi hilo la majambazi.
“Siku hiyo niliwasili ofisi ya kiongozi huyo [Mkuu wa Wilaya] wa serikali kwa ajili ya kukutanishwa na Barlow, lakini nilipoona kamanda huyo [Barlow] amefuatana na askari walionitishia kuniua, nilitoroka nikaenda zangu na sikujua kilichoendelea.
“Lengo langu lilikuwa kumjulisha Barlow kuwa na yeye yuko kwenye orodha ya watu wanaokusudiwa kuuawa na kundi lile la majambazi, ili akae chonjo.”
Matukio mengine aliyoshiriki
Pamoja na matukio mengine lukuki ya ujambazi, Malele anakiri kuhusika pia katika tukio la kumuua Mhindi wilayani Igunga, Tabora na kumpora Sh milioni sita.
Pia inaelezwa kijana huyo alishiriki kuwavamia wafanyabiashara ya ng’ombe wilayani Bariadi na kuwapora Sh milioni 10, ambapo yeye alipata mgawo wa Sh milioni mbili.
Katika mazungumzo yake, Malele anasema amekwisha kutanishwa na IGP Mwema na kumsimulia ‘mkanda mzima’. Lakini pia ameahidiwa kukutanishwa na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk. Emmanuel Nchimbi, siku na wakati wowote.
Kijana Malele ana siri nzito juu ya mtandao mpana wa mauaji ndani ya Jeshi la Polisi unaohusisha watumishi wengine kutoka vyombo vya ulinzi na usalama, wafanyabiashara na wanasiasa.
Habari za karibuni kabisa zinasema kwenye orodha ya aliowataja kwenye mtandao wa uhalifu, wamo wabunge. JAMHURI inaendelea kuyahifadhi majina yao kwa kuwa haijafanikiwa kuzungumza nao.
Mtandao huo unatajwa na Malele kwamba ndiyo uliohusika na mauaji ya Kamanda Barlow usiku wa kuamkia Oktoba 13, mwaka jana, katika eneo la Kitangiri jijini Mwanza wakati akimrejesha nyumbani Mwalimu Doroth Moses, aliyekuwa naye katika kikao cha harusi.
Malele alikamatwa Mei 10, mwaka huu, katika lango la Bunge mjini Dodoma wakati akiwatafuta wabunge kadhaa.
Malele anatajwa kuwa mtu muhimu ambaye taarifa zake zinawasaidia viongozi wa juu wa vyombo vya ulinzi na usalama, na serikali kwa jumla, kuutambua na kuufumua mtandao wa uhalifu ndani ya Jeshi la Polisi.
Anasema kwamba kikundi cha maofisa wa ngazi za juu wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza, kinachojihusisha na matukio ya ujangili, kilimtaka ashiriki kwenda kumuua Kamanda Barlow.
Anasema, pamoja na ukweli kwamba ameshiriki matukio mengi ya mauaji, hakutaka kabisa kwenda kumuua Barlow kwa kuwa anamfahamu vema, na kwamba alishafanya kazi nyumbani kwake.
“Nilikataa kwenda kumuua Kamanda Barlow, roho iliniuma sana walipotaka nishiriki mauaji hayo, kwa kweli nilihuzunika sana,” anasema.
Uamuzi wake wa kukataa kwenda kushiriki kwenye mauaji hayo, uliwatia hofu washiriki hao wa uhalifu, hatua iliyowafanya wamkamate Malele na kumpeleka katika Gereza la Butimba, akiwa amebambikiwa kesi ya ujambazi wa kutumia silaha.
Anasema akiwa gerezani, kikosi cha uhalifu ndani ya Polisi, kilikwenda kumuua Barlow, na kwamba siku chache baadaye, akiwa gerezani, alipata taarifa za mauaji hayo.
“Niliposikia Kamanda Barlow kauawa sikushangaa kwa sababu niliwajua wauaji, lakini cha kusikitisha ni pale niliposikia eti kuna Mwalimu amekamatwa akihusishwa na mauaji hayo,” anasema.
Taarifa za uchunguzi zinaonesha kuwa Malele baada ya kukaa gerezani kwa miezi kadhaa, Mkuu wa Gereza aliamua kumwachia kwani hakuona sababu ya kuendelea kumhifadhi mtu ambaye hana chembe ya mashitaka.
Inaelezwa kwamba mtandao wa uhalifu uliposikia taarifa za kuachiwa kwa Malele, ulijiandaa kumuua mara baada ya kurejea uraiani. Hatua hiyo ilimfanya kijana huyo agome kwa muda kutoka gerezani akitambua kuwa angeuawa.
“Nilimweleza Mkuu wa Gereza mambo yote, naamini kwa maelezo yale aliwasiliana na wahusika, sina uhakika, lakini nilidhani hivyo. Kwa sababu hiyo nikaogopa kuwa nikitoka lazima nitauawa. Baadaye nikapata wazo nikitoka gerezani niende wapi,” anasema kwenye maelezo yake.
Malele akimbilia katika Kikosi cha JWTZ
Baada ya kuachiwa kutoka Gereza la Butimba, Malele alikwenda moja kwa moja kujisalimisha katika Kikosi cha Anga cha Jeshi la Wananchi wa Tanzania kilichopo eneo la Uwanja wa Ndege wa Mwanza.
Uchunguzi wa JAMHURI unaonesha kuwa alipojisalimisha, aliwaeleza wanajeshi hao ‘mkanda mzima’ wa mauaji na vitendo vya ujambazi alivyokuwa akivifanya na hatari iliyokuwa ikimkabili endapo kikosi cha uhalifu kingejua yupo uraiani.
Uchunguzi unaonesha kuwa mbunge mmoja aliweza kuzungumza na kijana huyo na kumtaka afike mjini Dodoma ili aweze kusaidiwa. Kuna habari kwamba wanajeshi, kwa huruma na kwa kuzingatia uzito wa maelezo ya kijana huyo, walimsaidia nauli ya basi na Sh 10,000 kwa ajili ya chakula njiani.
Anaswa akiwatafuta wabunge
Malele alipofika Dodoma jioni, alipumzika na kwenda katika Ukumbi wa Bunge asubuhi. Kitendo chake cha kutojua kusoma na kuandika kilimfanya awe na karatasi yenye majina na namba za simu za Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu; na Mbunge Musoma Mjini, Vincent Nyerere.
Maofisa Usalama wa Taifa na Polisi waliokuwa katika lango alilofika walipomwuliza anataka kumwona nani, aliwapa majina hayo na namba za simu. Walipombana zaidi kujua shida yake nini, inasemekana Malele alianza kuwaeleza historia yake na namna alivyofika hapo bungeni.
Polisi waliposikia taarifa hizo, inaelezwa kwamba ziliwashitua, na wakaamua kuwasiliana na viongozi wakuu wa Polisi Mkoa wa Dodoma, ambao waliamuru awekwe rumande. Polisi hao Mkoa wa Dodoma waliwasiliana na wenzao wa Mwanza, na ndipo ikatolewa amri kwamba arejeshwe Mwanza kwa maelezo kwamba “ni mtuhumiwa hatari wa ujambazi”.
Hata hivyo, taarifa zilimfikia mmoja wa mawaziri, na yeye akawasiliana na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, David Misime, na kumtaka asimrejeshe Mwanza kijana huyo.
Uchunguzi zaidi wa JAMHURI unaonesha kuwa baadaye taarifa zilimfikia Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk. Nchimbi, na ndipo ukaandaliwa utaratibu wa kumhoji. Kwenye mahojiano hayo walihusishwa pia maofisa wa Usalama wa Taifa.
Imeelezwa kwamba kabla ya kuhojiwa, alijengwa kisaikolojia kwa kumhakikishia kwamba asingedhurika wala kupigwa. Alipewa chakula na akawa huru kuzungumza.
Habari za uhakika zinasema kwamba Malele alitoa maelezo marefu ya namna alivyoshiriki matukio mbalimbali ya ujambazi katika miji ya Mwanza, Geita, Shinyanga na maeneo mengi ya Kanda ya Ziwa.
Aliweka wazi kwamba yapo matukio mengi ambayo alitumika kama chambo. Miongoni mwa matukio anayoyaeleza kuwa yanamuumiza sana ni la yeye kutumiwa kumwita mama aliyekuwa Kanisa, na kisha kuondoka naye na kwenda kumuua.
“Kwenye mauaji hayo nilimfuata mama kanisani, alipotoka tukamteka na kwenda kumuua. Shida yetu ilikuwa viungo, tulikata maziwa na viungo vya sehemu za siri hivi vinatumiwa na wafanyabiashara,” amenukuliwa akisema.
Matukio ya ujambazi yalivyofanikishwa
Malele anasema ameshiriki matukio mengi – makubwa na madogo – ya ujambazi katika maeneo ya Ukerewe, Kahama, Shinyanga, Mwanza, Geita na kwingineko.
Kwenye mauaji ya Barlow, anasema chanzo hasa kilikuwa kwamba Kamanda huyo aliwahi kuwadhulumu wenzake, na kwamba walipomfuata mara kadhaa awape mgawo, aliwaahidi kufanya hivyo baada ya kupata “kazi nyingine kubwa”.
Anasema kikosi cha uhalifu kinawashirikisha Polisi, maofisa kadhaa wa Usalama Taifa, wafanyabiashara na wanasiasa.
Anawataja wanasiasa wengine kuwa wapo katika Kata ya Mwamayombo, Ngudu mkoani Mwanza. Anasema wapo wanasiasa wawili marafiki ambao mwaka 2010 waligombea udiwani (jina la kata tunalihifadhi kwa sasa) kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Chadema.
Ananukuliwa akisema, “Hawa ni marafiki sana, waligombea vyama tofauti kama kupoteza lengo, lakini walichotaka ni kuhakikisha mmoja wao anakuwa diwani. Kwenye uchaguzi akashinda wa CCM. Hawa ni majambazi, na ndiyo tulioshiriki nao kumuua yule mama wa Geita. Nilikuwa nasimamia miradi yao, nakusanya fedha kwenye maduka yao, waliniamini sana.”
Anasema kwenye ujambazi huwa wanatumia bunduki zilizokamatwa kutoka kwa majambazi wengine. “Bunduki walichukua zile zinazokamatwa kwa majambazi, risasi zilikuwa zinapatikana Polisi,” anasema.
Uamuzi wa kuacha ujambazi
Malele anasema mama yake ni mchungaji, na kwamba ameamua kuachana na ujambazi baada ya kuona anapata fedha nyingi, lakini haoni faida yake.
“Mama yangu ni mchungaji, ameshiriki kuniombea sana niache ujambazi nikawa sitaki, lakini sasa nimeona sina sababu ya kuendelea kwa sababu sioni faida, napata pesa lakini sijui zinakwenda wapi,” amenukuliwa akiwaambia viongozi wa vyombo vya Ulinzi na Usalama mjini Dodoma.
Kauli ya Waziri Nchimbi
Kwa upande wake, Waziri Nchimbi alipoulizwa juu ya Malele, amekiri kuwa na taarifa zake, lakini hakutaka kuingia kwenye undani wa suala hilo akisema ni nyeti.
Awali, uchunguzi wa mauaji ya Barlow ulianza kuelekea katika dhana kwamba zipo sababu zaidi za mauaji hayo.
Kikosi cha uchunguzi kilichoko Mwanza ambacho kilifuatilia, kilibaini kwamba Kamanda Barlow hakuuawa kwa sababu zinazohusiana na mapenzi pekee. Mapenzi inaweza kuwa njia moja ya kutaka kupotosha sababu za kweli za mauaji hayo.
Taarifa za kikosi cha uchunguzi zinasema kuna uwezekano wa mauaji hayo kuwa yamefanywa na vikundi vya kihalifu vya ndani ya Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na mitandao ya kihalifu nje ya Jeshi hilo.