Naandika makala hii muda mfupi baada ya kutoka Mahakama Kuu Kanda ya Iringa. Nimekuja hapa Iringa kusikiliza hukumu dhidi ya muuaji wa Mwandishi wa Habari, Daudi Mwangosi, aliyeuawa na askari Pacificus Cleophace Simon Septemba 2, 2012 akiwa kazini katika Kijiji cha Nyololo, mkoani Iringa. Niliamua kuja Iringa, baada ya kusikia mizengwe ya polisi katika kesi hii.
Sitanii, pengine nisije kusahau na kutokana na ufinyu wa nafasi, naomba kuchukua fursa hii kutoa pongezi za pekee kwa Muhimili wa Mahakama Nchini kupitia kwa wawakilishi wao, Jaji Dk. Paul Kihwelo na Mlinzi wa Amani, Hakimu Flora Mwelela. Kama si wawili hawa kuheshimu taaluma ya sheria na kuamua kutopindisha haki, kesi ya Mwangosi ingekwisha mapema alfajiri.
Ikumbukwe Jaji Dk. Kihwelo aliazimwa kutoka Kanda ya Magharibi, baada ya majaji waliopo Kanda ya Iringa kujitoa kwa kukataa kusikiliza kesi hii kutokana na nguvu kubwa iliyotumika na aina ya ushahidi uliowasilishwa na polisi. Niseme tena hapa, kwamba wakati umefika wa kuwa na waendesha mashitaka binafsi. Haiingii akilini, askari polisi wanaotuhumiwa katika kesi kama hii, ndiyo wawe waendesha mashitaka.
Ni kweli kuwa Jamhuri katika kesi hii iliwakilishwa na Wakili Mwandamizi, Adolfu Maganga, ambaye ni mtumishi wa Serikali, lakini hatari kubwa ni kuwa waandaaji wa ushahidi na waleta mashahidi ni polisi. Kwa kuwaangalia polisi, ambao muda wote walikuwa wakimfunika Pacificus kwa mashuka asipigwe picha, hata baada ya amri ya Mahakama kuwazuia bila kusikia, ingekuwa vigumu hawa kuwasilisha ushahidi makini.
Na kweli, ndicho kilichotokea. Katika kesi hii, Mkuu wa Upelelezi wa Mkoa, aliyekuwa Kamanda wa Polisi wa Mkoa, Michael Kamuhanda, mpigapicha aliyepiga picha iliyochapishwa katika gazeti la Mwananchi Septemba 3, 2012, hawa walikuwa mashahidi muhimu. Kwa bahati mbaya, hawakuletwa mahakamani. Polisi kwa makusudi, hawakumleta hata mtaalamu wa silaha kukagua silaha iliyoua.
Sitanii, ndiyo maana kwa kiburi na ujinga wa kutojua, muda wote walikuwa wakitamba mitaani kuwa wanashinda kesi hiyo ya mauaji ya Mwangosi. Mungu si Athumani na wala hanywi chai ya rangi, yaliyowakuta Julai 25, 2016 hawatasahau. Waliamini kwa kuficha ushahidi na kumshauri Pacificus akane ungamo lake kwa Mlinzi wa Amani, kesi hiyo ingekuwa imekwisha. La hasha, Jaji Kihwelo ameipa heshima taaluma ya sheria.
Julai 25, alimtia hatiani Pacificus kwa mauaji ya kutokukusudia. Hii peke yake iliwakata maini polisi waliokuwa wanatamba. Jaji Kihwelo alitumia ushahidi wa ungamo uliotolewa na Hakimu Mwelela, kuthibitisha kuwa Pacificus alimuua kinyama Mwangosi, kwani ushahidi huo ulipowasilishwa na upande wa Jamhuri, kwa kuwa alijua kuwa ameua kweli, si yeye wala wakili wake aliyeupinga. Baadaye sana, Pacificus akadai alishurutishwa kutia saini ungamo hilo. Maelezo ya kitoto kabisa!
Julai 27, polisi Iringa wakapata mshituko mwingine. Katika maelezo yao, mitaani walikuwa wakitamba kuwa Pacificus angefungwa miaka 3 tu, lakini Jaji Kihwelo akamfunga miaka 15. Hapa hoja si idadi ya miaka, bali kwanza ni kumpata na hatia askari Pacificus na pili kumpa adhabu. Hili ni fundisho kwa askari polisi wote nchini kuwa kumbe ukitumia vibaya silaha, unawajibika binafsi na si Jeshi la Polisi.
Kwetu sisi wanahabari, hukumu na kifungo hicho, pia ni msingi wa kuidai fidia Serikali, kwa makosa iliyofanya kuajiri Muuaji ndani ya Idara nyeti kama Polisi. Hapa kisheria Serikali inawajibika kwa matendo ya mwajiriwa wake (vicarious responsibility). Ni kwa msingi huu, wanahabari kwa kushirikiana na familia, tutaidai fidia Serikali kwa ajili ya familia ya Mwangosi.
Sitanii, hukumu hii imekuwa nguzo ya Haki za Binadamu nchini. Wapo askari ambao hupiga watuhumiwa, hutukana na wakati mwingine kuwatishia kuwapiga risasi bila hata watuhumiwa kukaidi amri zao, sasa hukumu hii ni mwanzo wa kuwawajibisha polisi wakaidi kwa matendo yao yaliyo kinyume na amri halali na kiapo chao cha kazi.
Sitanii, nimesikitishwa na kitendo cha polisi kuondoka na Mfungwa (Muuaji wa Mwangosi) Pacificus badala ya sheria inavyotaka kuwa akihukumiwa kifungo anahamia mikononi mwa askari Magereza. Kamanda wa Polisi Mkoa wa Iringa, atakuwa kwenye nafasi ya kueleza askari wake walimpeleka wapi Pacificus. Je, walimpeleka rumande za polisi, Magereza au nyumbani kwake?
Kwa mujibu wa Sheria ya Magereza ya Mwaka 1967, mtu anakuwa mfungwa tangu dakika Mahakama inapotamka adhabu dhidi yake. Kuanzia wakati huo, popote anapokuwa hugeuka gereza. Polisi wanaodhani wanamwokoa Pacificus asipigwe picha, wanaweza kuangukia katika kosa la kutorosha mfungwa, wakaishia jela pia.
Nilikwishaamua kuwa nitakuwa naandika nusu ukurasa, ila kwa umuhimu wa mada ya leo, naomba univumilie msomaji wangu niandike ukurasa mzima. Kwamba, katika hali isiyokuwa ya kawaida, polisi wa Iringa wamezuia wanahabari kumpiga picha Pacificus, kwa kuweka utaratibu wa kumfunika kwa shuka la Kimaasai, tangu mwanzo wa kesi hadi sasa.
Tunashuhudia katika Mahakama Kuu na Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, watuhumiwa na wafungwa wanapigwa picha. Polisi wa Iringa kwa kiburi tu, wameamua kuvunja Ibara ya 18 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (1977) inayotoa haki ya kupata habari. Nitashauriana na wanataaluma wenzangu kuona iwapo suala hili tulifungulie kesi au tuchukue mkondo wa kiutawala kwa kuwasiliana na wakuu wao wa kazi, wawafahamishe hawa askari waliotenda kosa hili mara nyingi, kuwa wanahatarisha ajira zao.
Wapo wanaodhani hukumu ya kuua bila kukusudia ni ndogo, na kwamba Pacificus amepewa adhabu ndogo kwa kufungwa miaka 15. Si kweli. Kwa Pacificus kufungwa zaidi ya miezi sita tu amepoteza kazi, na kwa kuwa amethibitika kuwa ni Muuaji, atafukuzwa kazi na utumishi wa umma.
Kwa maana nyingine, kuanzia Julai 27, 2012 iwapo wakili wake hatakata rufaa akafanikiwa kufuta adhabu hii, basi milele hawezi kuajiriwa tena, si katika Jeshi la Polisi tu, bali hata idara yoyote ya Serikali. Askari mnapaswa kukaa mkafikiria, yaliyomfika Pacificus yanaweza kukufika wewe pia.
Ingawa ushahidi uliotolewa na aliyekuwa Mkuu wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU), Said Abdallah, haukumtia hatiani Pacificus kwa mauaji, askari waliokuwapo mahakamani na waliosikiliza ushahidi huu wanapaswa kujifunza jambo. Kwamba SP Abdallah alisema bayana kuwa hakuna aliyempa amri Pacificus kufyatua hilo bomu la kishindo.
Hii maana yake ni nini, askari wanapaswa kusikiliza kwa makini wanapokuwa kazini kufahamu amri ipi imetolewa na iwapo amri hiyo ni halali. Kwa faida yenu, kama si nchi kuwa vitani kwa amri ya Amiri Jeshi Mkuu, operesheni maalumu nayo kwa amri ya Amiri Jeshi Mkuu, yaani Rais au mapambano na wahalifu wenye silaha, askari ukiua imekula kwako.
Hata hao wanaoitwa majambazi, ukimuua kwa risasi wakati yeye alikuwa na rungu, imekula kwako. Nadhani wakati umefika sasa kama Muhimili wa Mahakama ulivyofungua milango ya kufundisha somo la Huduma kwa Wateja (Customer Service), somo hili linahitajika katika Jeshi la Polisi.
Sitanii, wapo polisi wanaodhani kazi yao inapaswa kuwa ubabe tu, ila hawa wafahamu kuwa dunia inabadilika, waangalie kinachowakuta polisi wa Marekani wanaoua Wamarekani weusi wanachoozea magerezani. Watu tumeanza kufahamu haki zetu, na tuko tayari kulizinda kisheria. Sitanii, siku za haki za watu kuburuzwa zimekwisha.
Nimemsikiliza mara kadhaa Rais John Magufuli, amekuwa akisema mtu asionewe. Inawezekana wapo wasiotafsiri vyema kauli hii, lakini uhalisia ni kwamba Rais hatamtetea mtu atakayetenda makosa, bila kujali ni raia au askari.
Mwisho, nimeisikia dhana ya kukata rufaa na nia waliyonayo askari hawa kupambana hadi tone la mwisho! Hapa nawashauri kisheria kuwa waiangalie kwa umakini nia hiyo. Jaji Kihwelo tayari amekwishaonesha matundu kesi hiyo ilipoharibikia.
Wakishinikiza kukata rufaa, na Jamhuri inaweza kuomba kesi hii isikilizwe upya (retrial), matundu hayo yanaweza kuzibwa. Yakizibwa, Pacificus anaweza kuishia kupata adhabu ya kunyongwa hadi kufa. Swali ni je, kwa jinsi polisi wanavyotumia nguvu kumficha Pacificus, Muuaji huyu mfungwa atakaa gerezani au usiku atakuwa anaranda mitaani na kula kitimoto?
Mkuu wa gereza na Kamanda wa Polisi, jamii inawaangalia kwa umakini kuona mwenendo wenu katika hili. Pole familia ya Mwangosi, poleni wanahabari, ila huu ni mwanzo wa haki kutendeka sasa, kesho na keshokutwa hakuna askari atakayetamani kuua mwandishi wa habari, maana watafahamu fika kwa atakayeua, yatamfika ya Pacificus au zaidi.