*Nyampala auawa akidaiwa ‘kuiba’ mahindi ya Mkuu wa Gereza
*Mpambe wake anusurika kifo kwa kipigo, alazwa ICU Muhimbili
*RPC agoma kuzungumza, aukana mkoa wake akidai yeye ni RPC Mtwara
Dar es Salaam
Na Alex Kazenga
Wakati taifa likifikiria namna sahihi ya kukomesha mauaji ya mara kwa mara yanayotokea nchini, hali si shwari hata ndani ya kuta za majengo yanayolindwa na vyombo vya dola.
Kwa takriban miezi tisa sasa, kumekuwa kukiripotiwa matukio ya watu kuuana; wakati mwingine wana ndoa, watu wenye uhusiano wa karibu na hata ndugu wa familia moja kiasi cha viongozi wa dini na wa serikali kuwataka watu kurejea kwenye mafundisho ya dini na kuwa wacha Mungu.
Na sasa, askari wa Jeshi la Megereza wa Liwale mkoani Lindi wamejikuta katikati ya tuhuma nzito, ikiwamo kusababisha kifo cha mfungwa mmoja.
JAMHURI linafahamu kwamba kifo cha mfungwa huyo Na. 70/2020 aliyekuwa nyampala, Abdalah Ngatumbara, kilitokea Juni 8, mwaka huu, baada ya yeye na mpambe wake kutembezewa kipigo na askari magereza, wakilazimishwa kuwataja watu walioiba mahindi ya Mkuu wa Gereza.
Kwa bahati nzuri, mpambe wa Ngatumbara, Siaba Mbonjola (Na. 76/2021), alinusurika kifo na sasa amelazwa katika chumba kinachohitaji uangalizi maalumu (ICU), Taasisi ya Mifupa Muhimbili (MOI).
Awali, wafungwa hawa wawili walipelekwa Hospitali ya Wilaya ya Liwale ambapo wataalamu walithibitisha kifo cha Ngatumbara, baadaye Mbonjola akahamishiwa Hospitali ya Mkoa ya Sokoine na kisha kupelekwa MOI.
“Ukweli wa tukio hili unafichwa. Lakini kwa kifupi Mkuu wa Gereza la Liwale anahusika. Yeye ndiye aliyeamuru Ngatumbara na mwenzake wateswe hadi watakapotaja wezi wa mahindi,” amesema mtoa taarifa wetu kutoka ndani ya Gereza la Liwale (jina linahifadhiwa).
Inadaiwa kuwa wizi wa mahindi ya Mkuu wa Gereza, Gilbert Sindani, ulitokea wakati wafungwa wakivuna mahindi kutoka katika shamba la magereza.
“Mahindi yaliyoibwa yalikuwa yamekusanywa barabarani tayari kusombwa na magari kupelekwa ghalani na mengine kwa Afande Sindani ambaye siku hiyo alikuwa safarini Dar es Salaam.
“Akatumiwa taarifa za kuibwa kwa mahindi yake yaliyovunwa. Aliporejea Liwale, akamuita msaidizi wake na kuhoji juu ya taarifa za wizi. Akajibiwa kuwa zipo lakini hazikuwa zimefanyiwa uchunguzi,” amesema mtoa taarifa.
Anasema hadi wakati huo hakukuwa na yeyote anayetuhumiwa kwa sababu hakuna aliyebainika kupelekewa au kukutwa na mzigo wa mahindi.
Taarifa hizo hazikumridhisha Sindani, ambaye kesho yake, Juni 8, mwaka huu, akawaita nyampala wa gereza na mpambe wake na kuwataka wampe taarifa kamili. Wakamjibu kuwa hawajui chochote.
“Palepale akaanza kuwapiga akiwataka wamtaje aliyechukua mahindi na amechukua kiasi gani. Alipochoka, akaona haitoshi, akawaita askari wawili; Sajenti Yusuph Selemani na Koplo Fadhili Mafowadi, wamsaidie kuwapiga hadi watakapotaja wezi,” amesema.
Kipigo hicho hakikuwafurahisha askari wengine ambao waliwazuia Sajenti Yusuph na Koplo Fadhili wasiendelee kuwapiga, wakihoji iwapo wana uhakika kweli kuna wizi umetokea; wengi wakiamini kuwa uchache wa mavuno ya mwaka huu ndiyo sababu ya kudhani kwamba wizi umefanyika.
Baada ya Sindani kubaini kuwa Ngatumbara na Mbonjola wameumizwa sana, akaondoka. Muda mfupi baadaye akarudi na kuwapakia kwenye gari kuwapeleka hospitalini ambako madaktari walibaini kuwa tayari Ngatumbara alikuwa amekwisha kufariki dunia, na hata matumaini ya kupona kwa Mbonjola ni madogo.
Madaktari wakashauri tukio liripotiwe polisi na kupewa ‘PF3’ ili taratibu za matibabu kwa Mbonjola zifanyike.
Ngatumbara alikuwa anatumikia kifungo cha miaka mitano jela kwa kosa la kukutwa na nyama ya nguruwe pori.
Taarifa za tukio zavuja
Jitihada za Sindani kuficha tukio hilo zilishindikana baada ya wasamaria wema ndani ya Gereza la Liwale kuwapa taarifa ndugu wa Ngatumbara, akiwamo Diwani wa Mbaya, kata anakotokea.
Baada ya kupata taarifa walifika hospitalini na kuutambua mwili wa ndugu yao; lakini hawakuridhishwa na sababu walizopewa za kifo chake, wakaenda kwa Mkuu wa Wilaya kutafuta ufafanuzi.
Diwani, askari wanena
Diwani wa Mbaya, Ali Nassoro, analithibitishia JAMHURI kuwa Ngatumbara amefia mikononi mwa Mkuu wa Gereza na kwamba ana shaka kuwa ni kutokana na kipigo.
Anasema baada ya kupata taarifa aliwasiliana na vyombo vingine vya usalama kisha yeye na ndugu waliushuhudia mwili wa Ngatumbara ukiwa umewekwa chumba cha kuhifadhia maiti ukiwa umevunjwa miguu huku ukiwa umeathirika sana mgongoni.
“Hata daktari aliyekuwapo alithibitisha hilo,” anasema Nassoro.
Mmoja wa askari wa Gereza la Liwale (jina tunalihifadhi), anasema kisasi ndicho chanzo cha kifo cha Ngatumbara.
“Kuna watu ambao Mkuu wa Gereza hapatani nao. Kuna askari anawatafutia sababu awafukuzishe kazi. Ni bahati mbaya kuwa askari hao hawakutajwa na Ngatumbara na mwenzake,” amesema na kuongeza kuwa kuendelea kuwa huru kwa Sindani kunaharibu uchunguzi.
Tayari polisi inawashikilia Sajenti Yusuph na Koplo Fadhili ambao wapo mahabusu ya Mkoa wa Lindi wakati uchunguzi ukiendelea.
Simulizi ya ndugu
Mkazi wa Mbaya, Said Mohamed, anasema Ngatumbara alizikwa Juni 10, mwaka huu na kwamba ameacha mjane na mtoto mmoja.
Anasema awali taarifa kuwa Ngatumbara ana hali mbaya walizipata kutoka kwa mtu wasiyemfahamu, aliyewaeleza kuwa amemuona Hospitali ya Wilaya ya Liwale.
“Muda mfupi baadaye tukapigiwa simu na Diwani (Nassoro) akatueleza kuhusu tukio hilo. Siku ile afya yangu haikuwa nzuri, hivyo nikampigia simu Kassim Arafi (ambaye ni ndugu yake) nikamwambia aende hospitalini kuhakiki taarifa,” amesema.
Anasema alipofika hospitalini, Arafi alizuiwa kumuona Ngatumbara kwa maelezo kuwa akatafute kibali kutoka kwa Mkuu wa Gereza.
Kutokana na kizingiti hicho, Arafi aliamua kuulizia taarifa za ndugu yake kutoka kwa watu wengine, ndipo akaelezwa kuwa alifikishwa hospitalini akiwa na mfungwa mwingine, lakini yeye amefariki dunia.
Kutokana na utata wa taarifa na kwa kushauriana na diwani, Mohamed na ndugu zake wakaona ni vema kuwasiliana na Mkuu wa Wilaya aliyewataka wafike ofisini kwake siku inayofuata.
“Tukaenda kuzungumza naye. Akakiri kuwa anazo taarifa za tukio na kuwa amewasiliana na Mkuu wa Mkoa wa Lindi atume vyombo vya dola kufanya uchunguzi.
“Siku iliyofuata tukaitwa na Mkuu wa Gereza akisema tunahitajika kwenda Kipule liliko gereza tukapate maelekezo. Sisi tukamwambia hatuna usafiri. Akatutumia gari. Mimi, Arafi na Omari Mchite tukaenda gerezani ambako tuliwakuta maofisa wa vyombo vya ulinzi na usalama,” amesema.
Miongoni mwa maofisa waliokuwapo ni Mkuu wa Magereza wa Mkoa wa Lindi. Sindani akawaeleza ndugu wa Ngatumbara kuwa kifo cha ndugu yao kimetokana na shinikizo la damu (pressure).
Mohamed anasema walipohoji zaidi, wakaelezwa kuwa katika gereza hilo kuna kawaida ya kutokea wizi wa mahindi na mara nyingi wafungwa wanapoyasomba kutoka shambani hupotea.
“Sindani akadai kuwa askari wasimamizi ndio watekelezaji wa aina hiyo ya wizi. Akatuambia kuwa siku ya tukio yeye alikuwa amesafiri, akamuacha msaidizi wake afuatilie wizi wa mahindi unaofanywa na askari magereza kwa kushirikiana na wafungwa,” amesema.
Mkuu wa Gereza, mbele ya maofisa wengine kutoka mkoani, akawaambia kuwa aliporudi alipewa orodha ya askari wanaohusika, lakini hakutaja majina yao.
Sindani akaendelea kusema kuwa kesho yake aliitisha gwaride rasmi likijumuisha wafungwa wote na askari magereza, na kutamka kuwa wezi wa mahindi wamekwisha kufahamika, akiwataka kutorudia tabia hiyo.
Baada ya onyo hilo, Sindani anasema alipanda gari lake na kuelekea mjini na wakati akiwa njiani ndipo akapigiwa simu na msaidizi wake kumpa taarifa za Ngatumbara kuzidiwa, kupelekwa zahanati, na kwamba walikuwa wanaomba kibali apelekwe Hospitali ya Wilaya.
“Akasema kuwa msaidizi wake alitoa kibali, Ngatumbara akapelekwa hospitalini. Nako hali ikazidi kuwa mbaya hadi akafariki dunia,” amesema Mohamed.
Mohamed na ndugu zake wakayapokea maelezo ya Sindani, wakisema bado hawajaridhika kuwa kifo cha Ngatumbara kilisababishwa na shinikizo la damu.
Baadaye walipata kibali cha Mahakama cha kuufanyia uchunguzi mwili wa ndugu yao; uchunguzi uliofanywa na daktari akiambatana na maofisa wa vyombo vingine vya usalama.
“Ikagundulika kuwa mguu mmoja umevunjwa, mshipa wa nyuma wa mguu mwingine umechanika huku damu ikiwa imeganda maeneo ya mikononi,” amesema.
Taarifa ya daktari, kwa mujibu wa Mohamed, inathibitisha kuwa hakufariki dunia kutokana na shinikizo la damu.
“Daktari alihoji iwapo wakati Ngatumbara na mwenzake wakipelekwa hospitalini walipata ajali ya gari. Mkuu wa Gereza akajibu kuwa hakukuwa na ajali yoyote. Familia tukajua moja kwa moja ndugu yetu kafa kutokana na kupigwa,” amesema Mohamed.
Baada ya hapo wakaombwa kuchukua mwili wa ndugu yao kwenda kuusitiri, wakiahidiwa kuwa hatua zaidi za kisheria zitachukuliwa kwa wote waliohusika.
JAMHURI, limemtafuta Mkuu wa Gereza la Liwale, Sindani, kupata ukweli wa tukio hilo, lakini kwa nyakati tofauti amekwepa kwa makusudi kuzungumza.
Mkuu wa Magereza Mkoa (RPO) wa Lindi, Felscheme Massawe, naye amekataa kuzungumzia tukio hilo.
“Taasisi unayotaka nizungumzie ni taasisi ya usalama, siwezi kuzungumza na wewe wakati sikujui, juzi tu nimetapeliwa kwa njia ya simu, naogopa usije kuwa utapeli kama niliofanyiwa,” amesema Massawe.
Kwa upande mwingine, Mkuu wa Wilaya ya Liwale, Judith Nguli, anakiri kupokea taarifa za kifo cha mfungwa lakini naye hayupo tayari kutolea ufafanuzi wa kina akidai suala hili limo katika uchunguzi.
“Yanasemwa mengi, siwezi kusema kafanywa nini hadi akafariki dunia. Serikali inazidi kufanya uchunguzi kwa kina, kwa vile vyombo vya usalama vinachunguza, tuvipe muda vitakuja na ripoti yenye taarifa za uhakika,” amesema DC Judith.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa (RPC) wa Lindi, Mtatiro Kitinkwi, hakutaka kulizungumzia tukio hilo akidai yeye si RPC wa Lindi ni RPC wa Mkoa wa Mtwara.
“Unataka nikupe taarifa za mkoa usionihusu! Labda nikusaidie kukupa namba za simu za RPC wa Lindi, huyo atakupa ufafanuzi,” amesema Kitinkwi.
Hata hivyo, RPC Kitinkwi hakutuma namba ya simu ya ‘RPC wa Lindi’. JAMHURI linafahamu kuwa hadi mwishoni mwa wiki iliyopita, yeye alikuwa bado ni RPC Mkoa wa Lindi.