Kwa muda sasa, kumekuwapo maneno mengi kutoka kwa Rais Paul Kagame wa Rwanda yakimlenga Rais wetu, Jakaya Kikwete. Chanzo cha yote haya ni mapendekezo ya Rais Kikwete ya kumwomba Rais Kagame aketi na waasi wa kundi la FNBL ili kukomesha mapigano na mauaji yanayoendelea Rwanda na upande wa mashariki kwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).
Kumaliza migogoro kwa njia ya mazungumzo ndiyo njia rahisi zaidi kuliko mapigano yasiyokoma. Mataifa kama Korea Kusini na Korea Kaskazini sasa yanazungumza, seuze Rwanda na waasi? Colombia, Sri Lanka na kwingineko, serikali zimezungumza na waasi na sasa amani inatamalaki.
Kwa mtazamo wetu, kauli ya Rais Kikwete ilikuwa njema kwa sababu nyingi. Mosi, ni kulinda maisha ya wananchi wa mataifa hayo; na pili, ni kwa kuziepusha nchi kama Tanzania na Uganda na mzigo wa kulea wakimbizi. Pia tutaondokana na wimbi hili la silaha haramu zilizoongeza ujambazi nchini mwetu.
Kinyume cha dhamira ya Rais Kikwete, kumekuwapo ripoti nyingi kwenye vyombo vya habari zinazonukuu kauli za Rais Kagame akimkejeli, kumtukana na hata kumshushia heshima Rais wetu.
Kwetu sisi, tunaona kuwa kitendo cha kushambuliwa kwa Rais wetu, ni cha uchokozi na dharau kwa Taifa letu ambalo kwa miaka yote limekuwa mstari wa mbele kuhimiza amani. Tanzania imetumia rasilimali nyingi sana kuyasaidia mataifa mengi, ikiwamo Rwanda kuhakikisha kuwa yanapata amani. Uamuzi wetu umewafanya majirani zetu, wakiwamo Wakenya watucheke kwa sababu wakati sisi tukiyakomboa mataifa ya kusini mwa Afrika, yenyewe yalikuwa yakiendelea kuimarisha uchumi wake.
Tanzania ina mchango mkubwa sana katika ustawi wa Rwanda. Mengi mazuri yamefanywa na Watanzania kwa Taifa hilo dogo. Wasomi wengi wa Rwanda wamepata elimu yao hapa nchini.
Fadhila za punda kweli mateke. Wanyarwanda wamekuwa wakivamia maeneo ya Ngara, Karagwe na Biharamulo na kuua Watanzania huku wakiingiza mifugo yao bila woga.
Uchokozi huu unaweza kuwa si bure, kwani kumekuwapo maneno kwamba Rwanda na marafiki zake wana ndoto za kurejesha Ufalme wa Bahima, wakiamini kuwa sehemu ya magharibi mwa Tanzania ni sehemu ya utawala huo.
Kinachosikitisha ni kuona kuwa chokochoko zote hizi zinafanywa kwa nchi yetu, na sasa zinaelekezwa kwa Rais wetu bila sisi weyewe kuamka na kupinga mambo haya. Rais Kikwete anaweza kuwa hapendwi na Watanzania wote, lakini ni ukweli ulio wazi kwamba anayemshambulia, anaishambulia Tanzania na kwa hiyo hatuna budi kujihami.
Tunatoa wito kwa Rwanda kuacha chokochoko ili tuendelee kuishi pamoja kama ndugu wa damu. Wanachotaka wananchi wa nchi hizi mbili ni maendeleo. Hawataki kuingizwa kwenye uhasama. Tunamsihi Rais Kagame amheshimu Rais wetu, na kamwe asidiriki kurusha matusi, kejeli na mambo yasiyokuwa ya staha.
Watanzania tunapaswa kuweka kando tofauti zetu ili kwa pamoja tuhakikishe tunamtetea Rais wetu na tunailinda Jamhuri yetu. Afrika ni moja. Hatuna sababu ya kugombana, lakini ikibidi kufanya hivyo, hatutakuwa na namna nyingine. Rais wetu anastahili kuheshimiwa na kina Kagame na wenzake.