Na Stella Aron, JamhuriMedia, Dar es Salaam

Tanzania, kama nchi nyingi zinazoendelea, inakabiliwa na changamoto nyingi katika kilimo, ikiwa ni pamoja na uzalishaji mdogo, upotevu mkubwa wa mazao baada ya mavuno, na utegemezi mkubwa wa hali ya hewa.

Hata hivyo, matumizi ya teknolojia za kilimo yanaweza kubadilisha hali hii na kuongeza ufanisi katika sekta hii muhimu.

Matumizi ya teknolojia yana uwezo wa kuongeza uzalishaji na kupunguza upotevu wa mazao baada ya mavuno, hivyo kuboresha maisha ya wakulima na uchumi wa nchi kwa ujumla. Mifumo ya umeme wa jua ni mojawapo ya teknolojia ambazo inaweza kuleta mabadiliko chanya.

Serikali inasisitiza matumizi ya nishati safi ili kulinda afya za Watanzania lakini sekta ya kilimo imeonekana kuachwa nyuma licha ya kuwapo rasilimali jua ambapo sababu kuu ikiwatajwa kuwa ni uelewa mdogo wa matumizi ya nishati hiyo .

Ili kukabiliana na tatizo hilo, wadau wa habari wameshauri taasisi binafsi kushirikiana na vyombo vya habari ili kuongeza kasi ya uandishi wa habari za matumizi ya nishati hiyo ili kuongeza uelewa na na uhamasishaji wa matumizi katika kilimo.

Deodatus Balile, ni Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), alisema kuwa matumizi ya umeme jua yana faida kubwa kwa wakulima, wafanyabiashara na kwa wananchi kwani yanapunguza gharama za maisha ambapo tayari Serikali imezindua matumizi ya nishati safi ya kupikia.

Hayo aliyabainisha wakati uzinduzi wa Ripoti ya Uandishi wa Habari za Nishati ya Umeme Jua Katika Kilimo Katika Nchi za Afrika na Mashariki kwa mwaka 2023 iliyoandaliwa na Shule Kuu ya Uandishi wa Habari na Mawasiliano ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (SJMC) kwa kushirikiana na Kituo cha Ubora wa Vyombo Vya habari Afrika (ACME) ambao ulishirikisha Tanzania, Kenya na Uganda.

Balile ambaye alikuwa mgeni rasmi, alisema kuwa kukosekana kwa taarifa zaidi juu ya matumizi ya umeme jua kwa wakulima umechangia kukosekana kwa maarifa zaidi juu ya ubora wa umeme jua.

“Ukienda baadhi ya nchi kama Asia, China, India utakuta wakuliama wanatumia umeme wa jua kumwagilia na hata kukausha mazao. Sisi hapa Tanzania unatumika lakini kwa umwagiliaji ni jambo ambalo linaonekana kuwa nyuma, mfano wakulima wa zabibu wanaweza kukausha na zabibu ikauzwa duniani kwa kutumia umeme jua au wakulima wa mihogo wangeweza kutumia nishati ya jua kukausha.

“Tunaweza kuhifadhi mazao yaliyokaushwa na kutumika mbele ya safari, zababu na kuuza sehemu mbalimbali duniani, ndizi tungeweza kukausha, ukienda kule Karagwe utakuta ndizi wanakata ndogo ndogo na wanakausha lakini kwa kutumia jua isipokuwa teknolojia iwanayotumia si nzuri.” alisema.

Alisema kuwa mafunzo yatakayotolewa kupitia mradi huo, yatawezesha waandishi wa habari kubobea katika eneo la nishati ya umeme jua na kilimo hivyo kuongeza uwapo wa habari hizo katika vyombo vya habari.

Balile alisema mafunzo hayo yalenge kuwajenga na kujua umuhimu wa umemejua na matumizi yake katika kilimo kama vile kukausha vyakula, na kilimo cha umwagiliaji ili wakaielimishe jamii.

Mhadhiri wa Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam, Dk Elisha Magolanga, alisema kuna haja ya taasisi hizo kushirikiana kuomba fedha za kuendesha miradi ya kuwajengea uwezo waandishi wa habari juu ya uandishi wa habari za nishati ya umeme jua kwenye kilimo.

Alisema waandishi wa habari wanashindwa kuandika habari hizo kwa kina kwa sababu hawana uelewa wa kina juu ya suala hilo na fedha za kutosha kugharamia utekelezaji wake, hasa katika kipindi hichi ambacho vyombo hivyo vinapitia anguko la kiuchumi.

Hali hiyo inasababisha waandishi wengi kuandika habari zinazotokana na matukio yaliyoandaliwa na mashirika binafsi hali inayosababisha kukosekana habari za kijamii katika eneo hilo ambazo ndio zina wasomaji wengi.

Alisema kupitia uhirikiano huo waandishi wa habari watapewa mafunzo na kuwezeshwa kiuchumi na kutembelea maeneo mbalimbali miradi ya umeme jua kwenye kilimo inakotekelezwa na kuandika habari zitakazoleta hamasa kwa wakulima wengine kuiga mfano.

Alishauri pia kuwapo na mafunzo ya ndani ya vyumba vya habari mara kwa mara kwa kushirikisha taasisi zilizojikita katika eneo husika ili kuwapo na waandishi waliobobea na kuandika habari kwa weledi.

Akiwasilisha matokeo ya utafiti huo, Mhadhiri wa SJMC, Darius Mukiza, alisema walichukua sampuli ya habari 63 kutoka kwenye vyombo vya habari maarufu katika nchi za Tanzania, Kenya na Uganda.

Alisema utafiti huo ulionyesha kuwa kati ya vyombo hivyo Uganda waliandika habari 30, Kenya 23 na Tanzania 10. Kati ya hizo kwenye luninga jumla zilikuwa 33, kwenye magazeti 29.

Hata hivyo habari hizo hazikupewa kupaumbele katika kurasa za mbele za magazeti, kwani utafiti ulionyesha kuwa nyingi ziwekwa kuanzia ukurasa wa tano na kuendelea.

Alisema utafiti unaonyesha kuwa sababu za uhaba wa habari hizo kuwa ni waandishi kukosa uwelewa wa sekta hiyo, uhaba wa rasilimali fedha kuwawezesha kwenda kutafuta habari, kukosa soko na wakulima kukosa uelewa wa matumizi ya umeme huo kwenye kilimo.

Mhariri wa Habari wa Gazeti la Nipashe, Salome Kitomari, alisema, kama waandishi wa habari wakiwezeshwa kielimu na kiuchumi, wataandika habari za zitakazoleta uchechemuzi na kuzisaidia jamii za wakulima kusonga mbele kimendeleo.

“ Sisi tunawajibika kuandika habari ili jamii ichukue hatua na serikali ifanye mabadiliko ya sera, sheria na kanuni ili kuweka mazingira rafiki ya matumizi ya nishati ya umeme jua katika kilimo na kuwainua wananchi kiuchumi,” alisema.

Alisema kwa sasa elimu itakayotolewa kwa waandishi wa habari inapaswa pia kuzingatia mabadiliko ya teknolojia ili taarifa zitakazotolewa ziyafikie makundi yote hasa vijana ambao ndio wanategemewa kuwa watumiaji wakubwa wa nishati hiyo kwenye kilimo.

Alishauri pia kuwepo na uandishi wa habari wa ushirikiano katika ya nchi ili kuwapo na mawanda mapana ya walaji wa habari ili vyombo vya habari vinufaike na habari iliyoandikwa kwa kuongeza mapato.

Mhariri Mtendaji wa Gazeti la Mwananchi, Joseph Damas, alisema kwa kuwa baadhi ya habari ikiwamo za nishati ya jua hazitoki kwenye kurasa za mwanzo za gazeti kutokana na kutovutia wateja kuna haja ya utafiti unaofanyika kuonyesha namna ya kuziboresha ili zichangie kuingiza mapato.