Na Mary Gwera, Mahakama-Dodoma

Matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) ndani ya Mahakama ya Tanzania yametajwa kuleta manufaa lukuki ndani ya Mhimili huo ikiwa ni pamoja na kupunguza mlundikano wa mashauri.

Hayo yamebainishwa leo tarehe 18 Septemba, 2024 na Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel wakati akifungua Semina juu ya Maboresho na Uongozi wa Kimkakati katika Mnyororo wa Utoaji Haki kwa Baraza la Uongozi la Chama cha Mawakili Tanganyika (TLS) iliyofanyika katika Hoteli ya ‘African Dreams’ jijini Dodoma.

“Matumizi ya TEHAMA katika Mahakama yamesaidia kupunguza mlundikano wa mashauri kutoka asilimia 10 mwaka jana 2023 hadi kufikia asilimia tatu mwezi Aprili mwaka huu,” amesema Prof. Ole Gabriel.

Amesema kwamba, ili matumizi ya TEHAMA yaendelee kuleta tija ni vyema Wadau muhimu wa Mahakama wakiwemo Mawakili kuunga mkono matumizi ya teknolojia ili wananchi waweze kupata haki kwa urahisi bila mkwamo wowote.

“Mawakili watambue kwamba wao ni Wadau muhimu sana katika utoaji haki, hivyo ni muhimu mtekeleze majukumu yenu kwa mlengo wa kutoa haki kwa wananchi lakini pia ni muhimu kutumia teknolojia kwa kuwa inarahisisha zaidi upatikanaji wa haki,” amesema Mtendaji Mkuu.

Aidha, Mtendaji Mkuu amezungumzia kuhusu matumizi ya Ofisi Mtandao kwamba tangu ianze kutumika mahakamani imesaidia kupunguza gharama za ununuzi wa shajara (stationaries) kwa zaidi ya asilimia 60.

Akizungumzia kuhusu Semina hiyo, Prof. Ole Gabriel amesema kwamba, Uongozi wa TLS ulituma ombi kwa Mahakama ili iwape uelewa/kuwapitisha katika masuala mbalimbali yanayoendelea ndani ya Mhimili huo yanayohusu maboresho ya utoaji haki.

Aidha, Prof. Ole Gabriel ameeleza kwamba, kwa sasa Mahakama ya Tanzania ndio Taasisi ya kwanza inayoongoza kwa matumizi makubwa ya TEHAMA katika shughuli zake.

Amewaeleza Viongozi hao wa Chama cha Mawakili Tanganyika kuhusu mifumo mbalimbali ya TEHAMA iliyopo ndani ya Mahakama ambayo ni pamoja na Mfumo wa Kielektroniki wa Usimamizi wa Mashauri (e-CMS), Mfumo wa Unukuzi na Tafsiri (TTS), Ofisi Mtandao (e-Office), Mfumo wa Mawakili (e-Wakili), Mfumo wa Kijiografia za Mahakama (JMAP), Sema na Mawakili, Maktaba mtandao (e-Library) na mingine.

Aidha, Mtendaji huyo amewaeleza kuhusu maboresho yaliyofanyika ndani ya Mahakama ambayo ni pamoja na uboreshaji wa miundombinu ya majengo yake ikiwemo kujenga na kukarabati majengo mbalimbali lengo likiwa ni kufikisha huduma za utoaji haki karibu na wananchi.

Ameongeza kwa kusema kwamba, maboresho yote yaliyofanywa na Mahakama na yanayoendelea kufanyika yametokana na mchango wa Serikali ikiwemo kutoa fedha ambazo zinaiwezesha Mahakama kutekeleza maboresho hayo.

Naye Rais wa Chama cha Mawakili Tanganyika, Wakili Msomi Boniface Mwabukusi ameishukuru Mahakama ya Tanzania kwa kukubali ombi lao ya kupitishwa katika taratibu/maboresho mbalimbali ya Mhimili huo na kuomba elimu waliyopata itolewe kwa Viongozi na Mawakili wengine ili nao wafahamu maboresho mbalimbali katika mnyororo wa utoaji haki na hatimaye waweze kwenda katika mlengo mmoja wa kutoa haki kwa wakati kwa wananchi.

“Tunaipongeza Mahakama kwa maboresho mbalimbali, sote tunafahamu Mahakama ndio sehemu pekee inayohakikisha amani ya nchi, huduma ya utoaji haki ni huduma ya kiroho, ni huduma ya Kimungu,” amesema Wakili Mwabukusi.

Rais huyo wa TLS ameiomba Mahakama isiwaache nyuma bali ishirikiane nao ili waweze kutumia teknolojia sambamba na kuwezesha mifumo kusomana ili mchakato wa kupata haki uwe rahisi zaidi.

Katika semina hiyo ya siku moja Viongozi hao wa TLS watapatiwa mada tatu ambazo ni Mageuzi ya ki TEHAMA na Matumizi ya TEHAMA katika utoaji haki nchini, Maboresho ya Mfumo wa Menejimenti ya Mashauri (JoT e-CMS) na umuhimu wake katika kuboresha mazingira ya utoaji haki nchini Safari ya Mahakama ya Tanzania katika kuboresha mazingira ya utoaji haki haki nchini: Tulipotoka, tulipo na tunapoelekea na nyingine ni Kuwaza kimkakati kwa ajili ya Uongozi wa Kimkakati.

Aidha, katika semina hiyo, Mahakama ya Tanzania na Chama cha Mawakili Tanganyika (TLS) zitasaini hati ya makubaliano (MoU) kwa ajili ya kuhakikisha kwamba TLS inapata sehemu ya fedha ambazo Mawakili hulipa mahakamani wanapouhisha leseni zao za kila mwaka pamoja na fedha wanazolipa wakati wanapoapishwa.

Takwa hilo ni la kisheria, hivyo, makubaliano hayo yanalenga kuweka utaratibu mzuri wa utoaji wa fedha hizo kwa TLS.

Kadhalika, Viongozi hao wa TLS watatembelea jengo la Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania na Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki (IJC) Dodoma.

…………..

Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel (aliyesismama) akizungumza jambo wakati wa hafla fupi ya ufunguzi wa Semina juu ya Maboresho na Uongozi wa Kimkakati katika Mnyororo wa Utoaji Haki kwa Baraza la Uongozi la Chama cha Mawakili Tanganyika (TLS) iliyofanyika leo tarehe 18 Septemba, 2024 katika Hoteli ya ‘African Dreams’ jijini Dodoma. Kushoto ni Rais wa Chama cha Mawakili Tanganyika (TLS), Wakili Boniface Mwabukusi na kulia ni Mkurugenzi Mtendaji wa Chama cha Mawakili Tanganyika (TLS), Bi. Mariam Othman.

Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel akisisitiza jambo.Rais wa Chama cha Mawakili Tanganyika (TLS), Wakili Boniface Mwabukusi akizungumza jambo wakati wa hafla fupi ya ufunguzi wa Semina juu ya Maboresho na Uongozi wa Kimkakati katika Mnyororo wa Utoaji Haki kwa Baraza la Uongozi la Chama cha Mawakili Tanganyika (TLS). Kushoto ni Makamu wa Rais wa Chama cha Mawakili Tanganyika (TLS), Wakili Laetitia Ntagazwa.Rais wa Chama cha Mawakili Tanganyika (TLS), Wakili Boniface Mwabukusi (aliyesimama) akisisitiza jambo wakati wa hafla fupi ya ufunguzi wa Semina juu ya Maboresho na Uongozi wa Kimkakati katika Mnyororo wa Utoaji Haki kwa Baraza la Uongozi la Chama cha Mawakili Tanganyika (TLS).
Sehemu ya Viongozi wa TLS pamoja na Watumishi wa Mahakama wakimsikiliza Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania (hayupo katika picha) wakati alipokuwa akifungua semina  juu ya Maboresho na Uongozi wa Kimkakati katika Mnyororo wa Utoaji Haki kwa Baraza la Uongozi la Chama cha Mawakili Tanganyika (TLS).

Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel (aliyesismama katikati) akiwa katika picha ya pamoja na Baraza la Uongozi la Chama cha Mawakili Tanganyika (TLS). Wa pili kushoto ni Rais wa TLS, Wakili Boniface Mwabukusi, wa pili kulia ni Makamu wa Rais wa TLS, Wakili Laetitia Ntagazwa na wa kwanza kushoto ni Mkurugenzi Mtendaji wa TLS, Bi. Mariam Othman.
Picha ya pamoja kati ya Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel (aliyesimama katikati) na baadhi ya Viongozi wa Baraza la Viongozi la Chama cha Mawakili Tanganyika (TLS). (Picha na MARY GWERA, Mahakama)

Please follow and like us:
Pin Share